IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta amesema mgogoro wake na Mbunge wa Igunga Rostam Aziz, utamalizwa na kamati ya Mzee Mwinyi.
Sitta aliyasema hayo jana katika mahojiano na gazeti hili baada ya kutakiwa kueleza kwama kama anaamini kamati ya Mzee Mwinyi inaweza kumaliza migogoro baina ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Sitta alisema migogoro mingine baina yake na wanaCCM, itamalizwa na kamati maalum ya CCM iliyoundwa kufanya kazi hiyo.
Kauli ya Spika Sitta imekuja wakati kamati ya mzee Mwinyi iliyoundwa kutafuta chanzo na suluhisho la migogoro na chuki za wabunge hao, ikiwa imebakiza takriban mwezi mmoja kumalizika muda wa nyongeza uliotolewa na CCM.
Tayari kamati hiyo, imewasilisha taarifa yake katika kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) katika kikao chake cha mwezi uliopita mjini Dodoma na hivyo kuongezewa miezi miwili ili ikamilishe kazi yake.
Siku moja baada ya mkutano wa Nec, Makamu Mwenyekiti wa CCM bara, Pius Msekwa alisema Sitta na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa ndio chanzo cha mpasuko ndani ya chama hicho.
Mwananchi jana ilitaka kujua kama Spika Sitta anaamini kama kamati ya Mwinyi italeta suluhu ya kumaliza tofauti na mpasuko ndani ya CCM baina yake, Rostam na wanaCCM wengine.
Wakati Spika Sitta akizungumza na gazeti hili, alisema; " kuhusu tofauti zetu, itategemea kamati ya mzee Mwinyi, sisi wengine tunataka tuwe na amani."
"Lakini nina hakika na watu wale watatu, Mzee Mwinyi, Pius Msekwa na Abdulrahman Kinana, hekima zao zitamaliza hiyo migogoro na mpasuko ndani ya CCM. Sisi wengine tunataka amani," alisisitiza Spika Sitta.
Hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari vilikaririwa vikieleza kuwa mzozo baina ya Spika Sitta na Rostam Aziz umeendelea kufuka moshi huku Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwaagiza viongozi wa CCM mkoani Tabora kuumaliza kupitia vikao vya chama.
Katika kikao hicho, Pinda aliyekuwa ziarani Tabora aliwataka viongozi wa CCM mkoa kuandaa ajenda ya kumaliza mvutano huo kwa mazungumzo kuanzia ngazi ya kamati ya siasa ya wilaya hadi mkoa.
Aliwataka watumie njia iliyotumiwa na wenzao wa CCM Mkoa wa Rukwa kumaliza mvutano uliokuwepo baina ya Mbunge wa Sumbawanga, Paulo Kimiti na Mbunge wa Kwela, Christant Mzendakaya miaka ya nyuma.
Alisema viongozi wa CCM Rukwa walitumia vikao vya ndani kumaliza ugomvi huo na sasa chama kipo imara mkoani humo.
"Huu mvutano uliopo baina ya Spika Sitta na Mbunge Rostam inabidi umalizwe na nyinyi viongozi wa CCM wa mkoa huu, tumieni busara kutatua mvutano huu ili kukipa uimara chama chetu.
"Mvutano wa aina hii, uliwahi kutokea mkoani Rukwa baina ya Mbunge Mzindakaya na Kimiti, lakini kwa busara za viongozi wa CCM mkoani Rukwa waliumaliza na shughuli za kichama zinakwenda vizuri tofauti na ilivyokuwa awali," alisema Pinda.
Mbali na hatua hiyo, baadhi ya viongozi wa CCM waliiambia gazeti hili kuwa ni vigumu mvutano huo kumalizwa na viongozi wa mkoa huo kwa vile wamegawanyika makundi mawili hasimu.
Mvutano baina ya Sitta na Rostam uliibuka mwaka 2008 baada ya kuibuliwa kwa sakata la Richmond bungeni.
Sakata hilo, lilisababisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa pamoja na mawaziri Nazir Karamangi na Ibrahim Msabaha kujiuzulu.
Kikao cha 18 cha Bunge kilichomalizika hivi karibuni kilifunga rasmi mjadala wa Richmond na kuiagiza serikali itekeleze maazimio matatu kati ya 23 ya bunge.
Akizungumzia hatua ya mwenyekiti wa TLP kumwandikia barua akimtaka amwombe radhi na kumlipa Sh1bilioni baada ya siku saba, Sitta alisema amelisikia suala hilo, kupitia vyombo vya habari na hana taarifa rasmi.
"Nipo jimboni kwa ziara ndefu, ninatembelea na kukagua ahadi za uchaguzi kuona mwitikio na utekelezaji hasa mradi wa Sh500 milioni wa zao la Alizeti uliofadhiliwa na Denmark. Hilo la Mrema nasikia tu kupitia vyombo vya habari sina maoni mpaka nitakaporejea Dar es Salaam," alisema Spika Sitta.
You Are Here: Home - - Sitta: Mwinyi atamaliza mgogoro wangu na Rostam
0 comments