IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
NDANI ya wiki mbili tangu Chama Cha Jamii (CCJ) kipewe usajili wa muda, kimefanikiwa kupata maelfu ya wanachama, 4000 wakiwa wa mkoa Dar es Salaam pekee.
Mbali na Dar es Salaam, chama hicho kimeungwa mkono kwa kasi mikoani, kiasi kwamba katika mikoa 10 ambayo wanachama wake wamekwishaifikia, Tanzania Bara na Tanzania Visiwani, kadi 700 walizokuwa wamepanga kwa kila mkoa zimechukuliwa zote. Kwa sababu hiyo, chama kimelazimika kuchapisha kadi nyingine.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, katibu wa chama hicho, Renatus Muabhi, alisema chama hicho kimeanza vizuri kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi, hasa wa Dar es Salaam.
“Kwa Dar es Salaam pekee tumeshapata wanachama 4200 na katika mikoa mingine 10 tuliyopeleka kadi zetu ambazo kila mkoa tulipeleka 700 mpaka jana tuliambiwa zimekwisha na wameomba tuwapelekee nyingine. Morogoro wanataka tuwapelekee kadi 3000,” alisema Muabhi.
Mikoa iliyopelekewa kadi ni Mwanza, Dodoma, Morogoro, Iringa, Mbeya, Shinyanga, Tabora, Pwani, Zanzibar na Pemba. Chama hicho kilipatiwa usajili wa muda Machi 2 mwaka huu.
Jumatatu ijayo wanatarajia kuwasilisha maombi ya kupatiwa usajili wa kudumu katika ofisi za Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, baada ya kuwasilisha idadi ya wanachama wadhamini.
“Hii ni rekodi ya kipekee ambayo CCJ imeweka kwani haijawahi kutokea katika historia ya Tanzania na hasa tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe, kwa kwa chama kuomba usajili wa kudumu ndani ya siku 20 tangu kianzishwe,” alisema.
Katibu Mkuu huyo alisema haitakuwa jambo la busara kuchelewa kupeleka maombo hayo wakati kwa mujibu wa sheria, idadi inayotakiwa ya wanachama 200 katika mikoa 10 imeshafikiwa na kuvukwa.
“Ili tupate usajili wa kudumu, sheria inatutaka tuwe na wanachama 2000 katika mikoa 10 kwa maana ya wanachama 200 kila mkoa ikiwamo miwili ya Tanzania Visiwani. Sasa sisi tuna wanachama zaidi ya 2000, hivyo hatuna sababu ya kusubiri kwa muda mrefu kupeleka maombi yetu,” alisema.
Alisema kuwa chama hicho kimekubalika kwa muda mfupi kutokana na wanajamii wengi kuhitaji mabadiliko na kwamba imefikia mahala baadhi ya watu wametoa nyumba zao kuzifanya ofisi za CCJ.
Aidha, katibu mkuu huyo aliwashukuru Watanzania wote ambao wamejitokeza na wale wanaoendelea kujitokeza kuomba uanachama, ili kuhakikisha CCJ inatimiza malengo yake na hivyo kuingia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCJ Taifa, Richard Kiyabo, alisema CCJ itafanya uzinduzi rasmi wa ofisi na shughuli zote za chama Machi 21 mwaka huu katika viwanja vya CCJ Makao Makuu, Mwananyamala, Dar es Salaam.
“Tumeshafanya taratibu zote...sasa tunataka kukitambulisha rasmi chama kwa jamii na kuwaeleza kuwa hiki ni chama chao, hivyo wanapaswa kuguswa na CCJ. CCJ imedhamiria kurudisha hadhi ya taifa ambayo imeasisiwa na Mwalimu Nyerere,” alisema Kiyabo.
Alisema katika uzinduzi huo watapokea wanachama wapya mbalimbali wakiwamo waliowahi kushika madaraka makubwa ndani ya vyama vingine vya siasa.
“Tanzania inahitaji mabadiliko ya kweli. Ni vizuri kuondoa unafiki, siasa, uongo, ubinafsi na rushwa. Tutoke huko kwani inawezekana; hii si Tanzania ya umaskini tuna rasilimali zinazotutosha. Watanzania milioni 20 tunawakaribisha kujiunga na CCJ. Tanzania mpya inakwenda kuzaliwa kupitia CCJ,” alisema.
Mwenyekiti huyo alieleza kuwa baada ya kuwasilisha mambo ya usajili wa kudumu wanatarajia kuzuru katika kaburi la hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na baadaye kufanya mazungumzo na familia yake.
“Kwa kuwa CCJ inautambua, inaukubali na kuunga mkono mchango wa Baba wa Taifa katika kumkomboa Mtanzania, tumeona itakuwa jambo la busara kabla ya kufanya mambo mengine ya uzinduzi na kupeleka maombi ya usajili wa kudumu, tutaitembelea familia ya Mwalimu Nyerere na kuona pale alipolala; lakini kubwa zaidi ni kupata baraka za famlia hiyo,” alisema Kiyabo.
Kwa mujibu wa Kiyambo, ziara hiyo itafanyika Machi 16, ni moja ya ziara mbalimbali zinazofanywa na viongozi hao ili kupata baraka toka kwa waasisi wa taifa na viongozi wa dini.
Aidha, wakiwa mkoani Mara watafanya mkutano eneo walilochinjwa watu 17 mkoani humo pamoja na kuzungumza na wananchi na viongozi wa eneo hilo.
“Pia tutakwenda kuwapa pole na kutoa wosia wetu, kwani tuna sababu na makusudi ya kujijenga sisi wenyewe,” alisema.
CCJ, ambayo ilipewa usajili wa muda mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka huu, inahusishwa na baadhi ya vigogo wanaokerwa na mwenendo wa mambo ndani ya CCM, ambao wanatarajiwa kujiunga nacho wakati wowote kabla ya uchaguzi mkuu.
Baadhi ya wachambuzi wa kisiasa wanasema chama hiki ni mmeguko za CCM, na ndiyo maana imekuwa rahisi kupata wanachama wa kukidhamini katika muda mfupi, kwani wengi ni wana CCM wenyewe.
You Are Here: Home - - CCJ yazoa maelfu Dar
0 comments