Subscribe to receive latest Updates
Stories: 3163
Comments: 284

Online :

You Are Here: Home - - Waanzilishi wa CCJ watishiwa maisha. Waambiwa wajifunze kwa Sokoine na Kolimba

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter VIONGOZI wa chama kipya cha siasa kinachojulikana kama Chama cha Jamii (CCJ), wamedai kupokea simu za vitisho kutoka kwa watu wasiofahamika.
Mwenyekiti wa chama hicho, Richard Kiyabo, ambaye aliitisha mkutano wa waandishi wa habari mjini hapa, alisema tangu ameanza kupokea simu hizo zilizokuwa zikipigwa kwa namba zisizosomeka (Private Numbers) ni muda wa wiki sasa.
Hata hivyo alisema kuwa pamoja na vitisho hivyo hawakwenda kuripoti polisi, lakini kwa hali ilivyo sasa, lazima wawataarifu polisi.
“Hivi sasa tumeanza kupokea simu za vitisho zisizoeleweka, simu hizo zinapopigwa watu wanaopiga hutuambia, ‘Mnamfahamu Sokoine na Kolimba,’ na kwa kuwa tuna fahamu sahihi tunaelewa kinachofanyika.
“Kwa ujumla tunaishi katika hali ya wasiwasi kwani tunafuatiliwa hadi nyumbani wakati hatujavunja Katiba na tulisharidhia mfumo wa vyama vingi,” alisema Kiyabo ambaye aliambatana na Katibu Mkuu wa muda wa chama hicho, Renatus Muabhi.
Kuhusu habari mbalimbali zinazozungumzwa katika vyombo vya habari kuhusu CCJ ikiwemo ya chama hicho kuundwa na mafisadi na vigogo wengine, viongozi hao kwa nyakati tofauti walisema ni tafsiri potofu.
Kuhusu kupatiwa usajili wa muda viongozi hao walisema wameshaahidiwa na Msajili wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa, ambaye walifanya naye mazungumzo juzi mjini hapa.
Kwa mujibu wa viongozi hao, Tendwa aliahidi kufanya hivyo pindi atakaporejea Dar es Salaam.
“Katika mazungumzo yetu na msajili ameahidi kutupatia usajili atakaporejea Dar es Salaam hivyo wananchi wasiwe na hofu kuhusu usajili wetu huu wa muda,” alisema Kiyabo.
Aliongeza kuwa baada ya chama hicho kusajiliwa watafanya mambo ambayo wataagizwa na Tendwa na baadaye kuendelea na shughuli nyingine.
Walipoulizwa iwapo watasimamisha mgombea katika uchaguzi wa ngazi zote utakaofanyika Oktoba mwaka huu, viongozi hao walisema kuwa dhamira yao ni kusimamisha wagombea wote akiwemo wa ngazi ya Urais.
“Tumedhamiria kuweka mgombea pindi tukipata cheti, tutaweka watu safi wanaokubalika na ambao ni wazalendo. Alisema Kiyabo.
Kuhusu kutumwa na mtu kuanzisha chama hicho, Muabhi (Katibu Mkuu) alisema hawajatumwa na fisadi wala kigogo yeyote bali wameazisha chama hicho kwa utashi wao ili kuwakomboa wananchi.
“Chama Cha Mapinduzi kimekuwa kikizungumza mambo mengi kuhusu chama chetu na kudiriki kusema kuwa hatuna hata boti, badala ya kuzungumzia mambo mengi yanayolikabili taifa, waendelee kusema lolote hatuna haja ya kuwajibu,” alisema Muabhi.
Kwa mujibu wa viongozi hao, chama hicho kimekuja kwa malengo maalumu na si kwa nia ya kufanya porojo na kwamba wanaamini warithi wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyeyere na Waziri Mkuu wa zamani, hayati Edward Moringe Sokoine watatoka katika chama hicho.
Viongozi hao walibeza kwamba hadi sasa hakuna chama pinzani nchini kwa sababu vyama vilivyopo vinaishabikia serikali na kwamba moto walionao kwa sasa ni mara mbili na uliokuwepo awali.
Viongozi hao wamesema lengo lao ni kupata wanachama milioni 20 kutoka nchi nzima ambao watakuwa hawajajiunga na vyama vingine na kwamba hawataki kuchukua wanachama kutoka katika makapu (vyama) vya watu wengine.
Walipoulizwa sababu iliyowafanya kuchelewa kukianzisha chama hicho viongozi hao walisema kwamba mipango yao ilikuwa bado haijakamilika kwani walikuwa wakifanya utafiti kwanza kwani kila kitu kinaanzishwa kwa mipango.
Pamoja na mambo mengine waliweka wazi kwamba hawana ugomvi wowote na Rais Jakaya Kikwete wala vyama vingine na kwamba wanaweza kukaa na vyama hivyo na kujadili mambo mbalimbali yahusuyo mustakabali wa nchi.
Walisema wameanzisha chama hicho kwa kuwa wameguswa na mambo mengi ya nchi yasiyoshughulikiwa hasa vijijini ndio maana wakaamua kujitokeza kutetea mambo hayo.
Tags:

0 comments

Post a Comment