IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
ASEMA MARIDHIANO HAYAONDOI IMANI YAKE KATIKA KUPAMBANA NA UFISADI
SPIKA wa Bunge Samuel Sitta amesema yupo tayari kwa hukumu yoyote itakayotolewa na chama chake CCM, iwapo msimamo wake wa kupinga ufisadi, rushwa na maovu ndani ya chama hicho, utaonekana ni tatizo.
Sitta alitoa msimamo huo jana katika mahojiano maalumu na gazeti hili ambapo pia alibainisha kuwa hatua zilizochukuliwa na CCM kupitia kamati maalumu ya Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi kwenye kikao cha Nec, itasaidia kupunguza uhasama ndani ya chama hicho.
"Nasema uhasama ni suala la moyo wa mtu na la kibinadamu kabisa na mifano ni mingi tu. Lakini, watu wanapokuwa na uhasama, imani inabaki vile vile. Mimi nitaendelea kukemea ufisadi, rushwa na kama hilo ndilo litakuwa ni tatizo kwa CCM, basi nitakuwa tayari kwa hukumu yoyote ya Chama Cha Mapinduzi," alisema Spika Sitta na kuongeza:
"Kama nikikemea ufisadi au nikisema kwamba lazima tuwe wakali zaidi ni tatizo kwa CCM, basi nipo tayari kwa hukumu yoyote, eeh".
Sitta pamoja na baadhi ya wabunge waliojipambanua kama wapambanaji wa ufisadi amekuwa akitajwa na baadhi ya vyombo vya habari waziwazi kuwa na uhasama na aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa na Mbunge wa Igunga Rostam Aziz huku ikielezwa kuwa chanzo cha uhasama huo ni kashfa ya Richmond.
Kashfa ya Richmond ndiyo iliyomfanya Lowassa na mawaziri wengine wawili, Nazir Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha, kujiuzulu.
Uhasama ulisabisha CCM chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete kuunda kamati maalumu ya watu watatu kutafuta chanzo na suluhu ya mgogoro huo.
Kamati hiyo inaongozwa na Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi na wajumbe wake ni Abdulrahman Kinana na Makamu Mwenyekiti wa CCM bara, Pius Msekwa.
"Msimamo wangu dhidi ya ufisadi, maovu na rushwa bado upo palepale, kilichopunguzwa na CCM juzi kupitia Kamati ya Mzee Mwinyi ni uhasama kati yangu, Rostam na Lowassa, si wanatajwa kila siku?
"Tulikosana kisiasa ndani ya chama chetu CCM lakini, hilo la kutupunguzia uhasama haliondoi imani yangu wala msimamo wangu kuhusu kupambana na ufisadi."
Akitolea mfano wa maridhiano ya rais wa Zanzibar, Aman Abeid Karume na katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharrif Hamad, Sitta alisema hao walikuwa mahasimu wamefikia maridhiano lakini, hawakubadili msimamo na imani zao.
"Hivi ndivyo ilivyo kwangu kwamba, hatua hiyo ya kupunguza uhasama haiondoi wala kubadili msimamo wangu dhidi ya mapambano ya rushwa na ufisadi," alisisitiza.
Alisema: "Seif alisikilizana na Karume lakini, hawakubadili imani wala vyama. Mnaweza kukubaliana kuondoa uhasama lakini, imani ikabaki palepale".
Aliongeza: "Hata Ireland, taifa la kikristo lililopigana kwa zaidi ya miaka 30, baadaye waliunda chombo kwa maslahi yao wote mapigano yakaisha. Lakini kila mmoja akabaki na imani yake, Wakatoliki na imani yao, Waprotestanti walibaki na imani yao ingawa wote wanaamini katika Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu."
Aliongeza kuwa ndivyo ilivyo kwake, anaamini kuwa Katiba ya CCM inamruhusu na kumpa nafasi ya kuendelea kukemea rushwa na ufisadi jambo ambalo alisema ataendelea kulitekeleza.
Alibainisha kuwa suala la kupungua uhasama baina yao kama viongozi ndani ya CCM ni la heri, linahitaji muda na vitendo halisi ndiyo sababu hata kamati ya Mzee Mwinyi imeongezewa muda ili kufanyia kazi baadhi ya mambo.
"Hata rais alisema, uhasama ni hatari, ukialikwa katika sherehe, ukitaka kuinuka una hofu kuacha glasi yako mezani, kupunguza uhasama ni heri, lakini hili halibadili imani ya mtu. Kuondoa uhasama inachukua muda, lazima vitendo vya kurejesha imani viwepo:
"Hili litachukua muda ndio maana hata Kamati ya Mwinyi imeongezewa muda, uhasama ni suala la kibinadamu kabisa." alisema Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki.
You Are Here: Home - - Sitta: Nipo tayari kwa hukumu yoyote CCM
0 comments