Mwenyekiti wa kamati ya bunge ya Nishjati na Madini, William Shelukindo akiwasilisha bungeni dodoma jana taarifa ya Serikali kuhusu utekelezaji wa azimio la Bunge, juu ya mchakato wa zabuni ya mradi wa kuzalisha umeme wa dharula ambao ilipewa kampuni ya Richmond Development. |
BUNGE limefunga rasmi mjadala wa mkataba tata wa Kampuni ya Richmond Development (LLC) na Tanesco na kuacha serikali iendelee kutekeleza maazimio yake huku wabunge wawili Christopher Ole Sendeka na Dk Willibrod Slaa wakipambana hadi mwisho.
Dk Slaa na Sendeka wakionyesha ujasiri katika mapambano, sehemu kubwa ya wabunge wakiwemo wanaojipambanua kupambana na ufisadi jana walionekana kumezwa na kushindwa kung'ara huku Kamati ya Nishati na Madini yenye dhamana na sakata hilo, ikionyesha utiifu mkubwa kwa maamuzi ya serikali.
Tofauti na ilivyokuwa kwenye mkutano wa 16 wa Bunge na viapo vya baadhi ya wabunge kutaka kufa na Richmond, mjadala huo wa taarifa ya serikali kuhusu utekelezaji wa maazimio ya kampuni hiyo, ulianza kwa kupooza huku Mbunge wa Viti Maalumu (Ruvuma) Mhandisi Stella Manyanya, akiamua kuvirushia makombora vyombo vya habari na kusifia serikali na mawaziri wa serikali waliojiuzulu.
Lakini, Dk Slaa, ambaye alikuwa mchangiaji wa pili kwa mchana baada ya Juma Kilimbah, alianza kurusha makombora mazito akihoji ripoti kushindwa kubainisha mambo mengi ya msingi ambayo yalikuwemo kwenye taarifa kama hiyo iliyotolewa kwenye Mkutano wa 16 wa Bunge.
Kwa mujibu wa Dk Slaa, hakuelewa mantiki ya kukosekana majina ya watu muhimu waliopaswa kuwajibishwa kama aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini (Arthur Mwakapugi), kuachiwa hadi wanastaafu na wengine kutowajibishwa kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mbunge huyo wa Karatu na Katibu Mkuu wa Chadema, alihoji pia mantiki ya Kamati ya Nishati na Madini kumwacha Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Dk Edward Hoseah, kwa sababu nyepesi ya uchunguzi wa posho mbili unaofanywa na taasisi hiyo dhidi ya wabunge.
"Kuna mambo mengi ya msingi humu kwenye ripoti hayamo, kumwacha Hoseah kisa eti anafanya uchunguzi wa posho mbili dhidi ya wabunge ni jambo ambalo halina maana, kwa sababu hivi ni vitu viwili tofauti kabisa," alifafanua Dk Slaa.
"Kama ni uchunguzi wao kuhusu posho mbili waendelee na yeye kama ni kuwajibishwa hilo ni jambo jingine, kuliacha jambo hili katika mamlaka ya juu wakati Bunge ni chombo chenye nguvu na kushusha heshima ya Bunge."
Dk Slaa aliongeza kwamba, :"Uchunguzi wao waendelee kama mimi nimekula posho mbili wanichunguze waje wanikamate, lakini kuogopa uchunguzi wa Takukuru kuna walakini, nilikwishasema uchunguzi wa Takukuru usije ukafunga watu midomo."
Katika kuonyesha msisitizo, Dk Slaa aliweka bayana kwamba Dk Hoseah alionywa kwa kutokuwa makini na kutaka serikali ifafanue kama kosa hilo adhabu yake ya mwisho ni onyo au vinginevyo.
Mbunge huyo ambaye amejizolea sifa kutokana na kupambana na ufisadi, alihoji pia serikali kujaribu kusafisha hata wajumbe watano wa Timu ya Mashauriano ya Mikataba Serikalini (GNT), wakati walikuwa ni sehemu ya ushauri katika mkataba huo ambao uliitia serikali hasara.
Makombora hayo ingawa yalikuwa ya wabunge wawili, lakini yalitikisa Bunge, baada ya Sendeka kupata nafasi na kuhoji kama dhima za Bunge la kidemokrasia linavyoweza kufanya katika kusimamia rasilimali za taifa zisiporwe na watu mbalimbali wakiwemo wageni kwa kisingizio cha uwekezaji.
"Tumejiuliza kama mabunge ya wenzetu ya kidemokrasia yanafanya nini katika kusimamia rasilimali za taifa, sauti ya wanyonge na kupigania haki bila hofu na kufanya mambo kwa ujasiri?"
Sendeka ambaye huwa na kawaida ya kuzungumza kwa ujasiri mkubwa aliongeza kwamba, Bunge la Tanzania chini ya Spika Samuel Sitta, limekuwa makini la viwango na kizalendo ndiyo maana, liliwahi kusimamia vema wajibu wake na kumfanya waziri mkuu (Lowassa) akajiuzulu.
Alitia ngumu akisema:, "Bunge dhaifu siyo tu linakuwa si la kizalendo la kimamluki au la, bali ni Bunge ambalo linajiandalia kifo, lakini Bunge letu ni makini, linaongozwa na Spika jasiri ndiyo maana limekuwa likifanya mambo yake kwa umakini."
Mbunge huyo wa Simanjiro, aliweka bayana kwamba, wao wamekuwa wakipachikwa majina mbalimbali ikiwemo makamanda wa ufisadi, mgambo, wapambanaji na sasa hivi wanaitwa wapambe wa Spika Sitta na kuongeza: "Lakini, tatizo tumekanyaga maslahi ya wakubwa. Tutaendelea kukanyaga."
Alisema Bunge mamluki haliwezi kuwa la kizalendo, kutetea haki za wananchi na kuwa sauti ya wanyonge na kusisitiza kwamba, kamwe hawatakubali kulifanya Bunge hilo kuwa mamluki na lisilo la kizalendo hata siku moja.
Sendeka katika kuonyesha kumtega Rais Kikwete, alisema: "Serikali yetu ni sikivu, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano Jakaya Mrisho Kikwete ni mtu mwenye dhamira njema ndiyo maana ameruhusu kujiuzulu waziri mkuu (Lowassa), tusiiseme serikali yote ina mafisadi, mafisadi ni mtu mmoja mmoja, na kama ni huyo Hoseah naamini Rais Kikwete atamwajibisha tu."
Sendeka aliongeza kwamba, kumekuwa na magazeti mengi yanayoanzishwa mahususi kumchafua Spika Sitta kutokana na kazi yake nzuri anayofanya na kuweka bayana,: "Hata wachapishe magazeti elfu mbili na kununua wahariri wote, hatutarudi nyuma kwani hawawezi ku-corrupt akili za Watanzania wote, kama ni fisadi ni fisadi tu."
Katika hatua nyingine, Spika Sitta amemshauri Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz akisema amefunga mjadala wa Richmond na kwamba hata hoja yake ya kutaka jopo la majaji kuchunguza mkataba huo haina nguvu na haiwezekani na kuonya atakayeendelea atachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni.
Hata hivyo, Rastam akiongea na Mwananchi alisema: Nakubali kwamba jambo hili limefungwa. Tumepoteza sana muda kwa jambo ambalo lingeweza kumalizwa kwa wiki moja, lakini likadumu kwa miaka miwili kwa kuwa liliendeshwa kisiasa. Ni jambo la kusikitisha kwamba tumewanyima wananchi ukweli,â€
Awali, Taarifa ya Kamati ya Nishati na Madini, ilionekana kumgwaya Dk Hoseah kwa kushindwa hata kuhoji kwanini mamlaka ya juu (Rais) imeshindwa kumwajibisha katika hilo.
Taarifa hiyo iliweka bayana kwamba, kamati imeamua kumwacha DK Hoseah mikononi mwa mamlaka ya juu tofauti na maneno yake ambayo alikuwa akiyatoa nyuma na hata yale yaliyotolewa na kamati hiyo katika mkutano wa 16.
Akizungumzia kwanini wameamua kutotaka kujadili tena azimio namba tisa kuhusu Dk Hoseah, alisema ni kwa sababu ya uchunguzi ambao umekuwa ukifanywa na Takukuru dhidi ya wabunge.
“Kamati yangu haikuweza kulizungumzia hili kwa sababu mkurugenzi wa Takukuru ameanzisha zoezi la kuwachunguza wabunge. Kamati imeona haitakuwa haki kutolea maelezo au majibu kwa serikali kuhusu azimio hili,â€alisema Shellukindo.
Shellukindo aliyeanza kusoma taarifa hiyo saa 5:55 hadi saa 6:23 kuhusu azimio namba 8 na 14 alisema, kamati hiyo imependekeza kuendelea kwa hatua hiyo na ikikamilika itoe taarifa kwenye Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo aliweka bayana utata mwingine wa malipo ya gharama za kuingiza mitambo ya Kampuni ya Dowans ambayo ilirithi mkataba wa Richmond Development (LLC), ambao awali, ulionyesha kuwepo dola 4.8 milioni ambazo ni kwa gharama ya ndege.
Akifafanua, alisema baada ya ukaguzi kufanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ilibainika kuwepo gharama nyingine tata za dola 3.9 milioni, ambazo zilionyesha kuingiza mitambo kwa njia ya meli na kuagiza zirejeshwe serikalini.
Awali, Azimio Namba 10 lilihusu malipo hayo ya dola za Marekani 4.8 milioni kwa Dowans, lakini, uchunguzi wa kina wa BoT, ulibaini kiasi hicho cha fedha kilikuwa ni halali kwani kililipwa kwa ajili ya kuingiza mitambo kwa ndege.
Kuhusu azimio linalotaka Bunge lishirikishwe tangu awali katika mikataba mikubwa ya kibiashara ya nchi, alisema tayari utafiti wa pamoja kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kuona namna mabunge mengine ya Jumuiya ya Madola (CPA), yanavyofanya kazi hiyo umeanza.
Akichangia taarifa hiyo, Mbunge wa Mkanyageni (CUF) Habib Mnyaa, alihoji kuchelewa kwa uchunguzi dhidi ya mawaziri hao wawili wakati maazimio ya Bunge yalitolewa tangu mkutano wa 10 wa Bunge, Febrauri mwaka 2007.
"Hivi mheshimiwa Spika huu muda wote bado uchunguzi unafanyika, Kamati yako Teule ilichunguza kwa muda mfupi tu, lakini serikali yenye kila aina ya nyezo hadi leo inasema inafanya uchunguzi, ni uchunguzi gani huo?" alihoji Mnyaa.
Aliongeza kwamba, hata kushuka huko kwa gharama hizo za maunganisho ya umeme kumekuwa kukichelewa tangu mwaka 2005 na kuongeza kwamba, hata kama sasa hivi gharama zimeshuka hadi dola 1.8 milioni kwa mwezi bado serikali inapaswa kulipa Sh 21bilioni kiasi ambacho bado kingeweza kufanya mambo makubwa na mengi kama zingetumika kwenye maendeleo.
0 comments