IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
SERIKALI imekiri kuwa mpaka kati ya Tanzania na Malawi ni suala lenye utata unaosababisha mvutano unaohitaji ufumbuzi wa haraka.
Kukiri huko kulifanywa jana bungeni na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alipokuwa akijibu maswali ya papo kwa papo.
"Anachosema mbunge ni kweli kwamba kumekuwa na mvutano au ubishi kati ya upande wa Malawi na sisi juu kuhusu mpaka hasa uko wapi, ni kati au pembeni mwa ziwa au pembeni mwa Tanzania," alisema Pinda.
Waziri mkuu alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Ludewa Profesa Raphael Mwalyosi, aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na serikali, kulipatia ufumbuzi tatizo la mpaka kati ya Tanzania na Malawi .
Pinda alisema tatizo hilo ni la muda mrefu na kwamba lina historia ndefu, lakini alisisitiza kuwa litashughulikiwa kwa njia ya mazungumzo kati ya Tanzania na Malawi, kupitia taratibu za za kimataifa.
"Ni suala refu na lina historia ndefu, lakini taratibu za kimataifa zipo na bahati nzuri zaidi Rais wa Malawi ndiye Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) kwa sasa, hivyo hilo linazungumzika," alisema Pinda.
Alibainisha katika kushughulikia hilo, amemwandikia barua Katibu Mkuu Kiongozi ili aanzishe mazungumzo ya kitaalam hasa kipindi hiki ambapo Rais wa Malawi ni Mwenyekiti wa AU.
"..Nimemwandikia barua Katibu Mkuu Kiongozi ili aanzishe mazungumzo ya kitaalam, kwa bahati nzuri Rais wa Malawi ndiye Mwenyekiti wa AU,"alisema Pinda.
Pinda alisema masuala yote ya shughuli za maendeleo na uhakika wa mpaka ni za muhimu.
"Kwa bahati nzuri mambo yote ni mazuri. Shughuli za maendeleo hasa upande wa Tanzania ni muhimu na suala la kuwa na uhakika wa mpaka pia ni muhimu pia," alisema Pinda.
Alilishukuru Bunge kwa kuona mambo mazito na kuyaweka katika mwelekeo wa kuridhia hatua zake.
You Are Here: Home - - Mzozo waibuka mpaka wa Tanzania na Malawi
0 comments