IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Jakaya Kikwete amewataka viongozi wanaokipeleka chama hicho nje ya misingi yake wajing'oe wenyewe au wanachma wawaondoe.
Rais Kikwete alisema hayo jana katika mwanzao wa ziara yake ndefu ya kichama mkoani Dar es Salaam ambapo anatembelea wilaya zote na kuzungumza na makundi mbalimbali hadi na viongozi wa shina.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete imekuja katika kipindi ambacho CCM kinapita katika changamoto kubwa kisiasa kutokana na kukumbwa mlolongo wa mambo yanayokitikisa.
Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na kushamiri kwa makundi ndani ya chama hicho, tishio chama kumeguka na kuibuka kwa CCJ ambayo imeitisa CCM kutokana na fununu kwamba, baadhi ya vigogo wake wanakiunga mkono.
Akizungumza na mamia ya wanachama wa CCM katika Ukumbi wa Vijana Kinondoni, Rais Kikwete alisema chama hicho hakiongozwi kwa matakwa ya mtu binafsi.
Huku akishangiliwa kwa nguvu na wanachama, Kikwete alisema chama ni tofauti na serikali, ndiyo maana hata yeye hawezi kufanya maamuzi ya hovyo kwa ubinafsi.
"Kuna viongozi wanaweza kupeleka chama kubaya. Viongozi wa namna hii mnapaswa kuwakataa, waambieni unakokipeleka chama siko; akikataa anapaswa kushushwa kwenye uskani,"alisema.
Alisema chama kinaongozwa kwa taratibu ambazo maamuzi yake ni vikao halali. "Mimi serikalini naweza kuamua jambo kwa sababu nina mamlaka makubwa kikatiba, ninao mawaziri ambao ni washauri tu, lakini nikisema fanya hivi anafanya, tofauti na chama."
Alianisha kwamba, CCM inapaswa kushinda uchaguzi lakini ili kufanikiwe lazima kuwe na umoja, upendo na mshikamano.
"Nimepata taarifa ya chama chetu hapa Dar es Salaam, nimefurahishwa. Kuna maeneo hali ni mbaya watu wanafikia hata kutaka kuuana, hii ni hatari, tabia hiyo ikomeshwe mara moja,รข€ alisisitiza na kutahadharisha kwamba, uadui utadhoofisha chama hicho.
Kwa mujibu wa Kikwete, CCM inapaswa kuendeshwa kwa uwazi, bila majungu.
"Naijua CCM tangu TANU ni chama kinachoendeshwa kwa ukweli, sasa kutetana kutadhoofisha umoja. Mseme mtu kwa ukweli, kwanini mumtete?" alihoji
Katika mkutano huo ambao aliambatana na watendaji mbalimbali kwaajili ya kujibu maswali na kero za wananchi, Rais Kikwete alisema ndiyo maana hata chama kimeamua kutanua wigo wa kidemokrasia katika kupata viongozio ili kupunguza rushwa, fitina na ulofa.
Aliongeza kwamba, CCM ni chama makini hakitaki watu wa wanaonunua wapiga kura kwa kuwafungia gesti na kuwapa bia mbili mbili na vipapatio vya kuku.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete amewaweka kitimoto watendaji mbalimbali wa CCM mkoani na kuwataka wajibu maswali ya wananchi.
Miongoni mwa kero kuu zinazochefua wananchi ni huduma mbovu katika mahospitali.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo leo, Rais ataanza ziara yake kwenye kata ya Sandali na kupokelewa na viongozi na wanachama wa wilaya ya Temeke na kupewa taarifa fupi ya ujenzi wa ofisi ya kata.
Kwenye ratiba hiyo, inaonyeshwa Rais atafungua ofisi mpya ya CCM kata ya Sandali na kusalimiana na wanachama na kwenda ofisi ya chama hicho tawi la Mgulani ambako atafungua tawi jipya la Chuo Kikuu -DUCE.
Baada Kikwete atakwenda hadi kata ya Mbagala Kuu ambako atawatembelea wananchi walioathirika na mabomu kutoka kambi ya Jeshi la Ulinzi wa Wananchi (JWTZ) na kisha katika ukumbi wa PTA (sabasaba) ambako atazungumza na viongozi wa mashina, matawi, Kata, Mabaraza ya Jumuiya na Baraza la Wazee wa chama.
Kwa mujibu wa ratiba, baada ya hapo Rais ataondoka kuelekea kata ya Vingunguti ambako atapokelewa na viongozi wa chama kisha kupokea taarifa fupi ya mradi wa uwekezaji kati ya chama na Kampuni ya Kobil na kuuufungua rasmi.
Rais baada ya hapo msafara wa Rais utakwenda ukumbi wa Korea ambako atafanya mazungumzo na viongozi wa kata, matawi, mashina, Jumuiya na wazee wa chama.
Februari sita, Rais atakuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo ya miaka 33 ya kuzaliwa CCM, lakini kabla ya hapo ataongoza matembezi ya mshikamano hadi viwanja vya Mnazi mmoja.
Uamuzi wa kusogeza mbele maadhimisho hadi Jumamosi umelenga kutoa fursa wananchama na wananchi wengine kuhudhuria sherehe hizo, kwa kuwa Februari 5, ambayo ni Ijumaa ni siku ya kazi.
You Are Here: Home - - JK acharuka, adai wenye nia mbaya na CCM wang'oke
0 comments