Mwenyekiti wa chama cha TLP,Augustino Mrema ambaye amedai Chama Cha Jamii CCJ ni zao la lililotokana na kongamano lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere inayoongozwa na Joseph Butiku |
MWENYEKITI wa TLP, Augustine Mrema amesema Chama Cha Jamii (CCJ) kimeanzishwa ikiwa ni matokeo ya kongamano lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere inayoongozwa na Joseph Butiku, ambaye ameyaelezea madai hayo kuwa "upuuzi".
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mrema alisema vigogo wa CCM waliozungumza kwenye kongamano hilo na kutamka wazi kuwa Rais Jakaya Kikwete ameshindwa kufanya maamuzi magumu, ndiyo waanzilishi wa CCJ.
CCJ ni chama kipya cha kisiasa ambacho kuanzishwa kwake kunahusishwa na mkakati wa vigogo na baadhi ya wabunge wa CCM ambao hata hivyo hadi leo hawajajitokeza hadharani.
Mrema, ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kabla ya kutofautiana na mawaziri wenzake mwaka 1995 na kujiunga na chama pinzani cha NCCR Mageuzi, alidai kuwa ametumia mbinu zake za usalama wa taifa kuwatambua vigogo hao.
Bila kuwataja kwa majina, Mrema alisema vigogo hao wanatumia mwamvuli wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere kuandaa makongamano kwa nia ya ya kumtukana na kumhujumu Rais Kikwete.
"Wanatumia mwavuli huo kumtukana rais kwamba anazungukwa na wezi na kwamba hana maamuzi magumu wakati wenyewe hawana maamuzi hayo," alisema Mrema.
"Ni aibu kwa vigogo hao wa CCM tena wanaojifanya kuwa wapo chini ya mwamvuli wa Tasisi ya Baba wa Taifa kuandaa makongamano ya kumtukana rais wetu hadharani wakati wenyewe pia hawana mamuzi magumu na kama wanayo basi wajitangaze hadharani kuwa wao ndiyo CCJ," alisema Mrema.
Mrema, ambaye alikuwa nchini India kwa matibabu na ambaye alikanusha kuwa safari yake ilidhaminiwa na Kikwete, alisema: “Kumwambia rais maneno makali kama hayo tena hadharani ni kutaka wananchi wamdharau na kumwona mwizi pia na kimsingi huu ni uhaini.
"Nimetumia uzoefu wa taaluma yangu ya Usalama wa Taifa na kubaini machafu yanayofanywa na vigogo... simtetei Kikwete bali natetea rais yeyote wa taifa hili siyo Kikwete tu kama wanavyosema nipo kwenye mtandao wa Kikwete na wengine kudai kuwa nimenunuliwa.
"Kikwete hawezi kuninunua; mimi ni mtu wa gharama sinunuliki, ila kwenye ukweli panastahili kuzungumzwa; natumia taaluma yangu kutetea taifa, siwezi kuona taifa linayumba halafu nikae kimya; mimi na mkurugenzi mstaafu wa Usalama wa Taifa bwana."
Hata hivyo, hakueleza alikuwa mkurugenzi wa kitengo gani cha Usalama wa Taifa.
Mrema aliongeza kusema: "Siingii jikoni kupika, lakini nina utaalamu wa kupika. Ninataka wale vigogo wanaomhujumu rais kwa maneno ya kijeli, kama wana uwezo na kujiamini wajitokeze hadharani wasema wao ndiyo wenye CCJ."
Hata hivyo mwenyekiti wa taasisi hiyo, Joseph Butiku alipuuza madai hayo ya Mrema akisema hawezi kuzungumzia upuuzi.
"Sitaki kuulizwa maswali yasiyo na maana; nenda kamuulize aliyekwambia upuuzi huo," alisema Butiku.
Katika hatua nyingine wakati Mrema akitoa tuhuma hizo nzito, CCJ imeanza mapambano kupigania usajili wake kwa kumhoji Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa sababu za kushindwa kuwapa usajili wa muda.
Tamko hilo la CCJ kwa Tendwa limekuja katika kipindi ambacho Msajili amekuwa akisisitiza kuwa uwezekano wa chama hicho kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 haupo kwa sababu muda hautoshi kwa chama hicho kukamilisha taratibu zote ili kipate usajili wa kudumu.
Usajili wa muda, ambao unahusisha chama kipya kitafuta angalau wanachama 200 kutoka mikoa 10 au zaidi, huchukua miezi sita ambayo hufuatiwa na uhakiki unaofanywa na Msajili kabla ya kupata usajili wa kudumu.
Tendwa alisema hata kama chama kipya kitakamilisha sharti hilo la kwanza katika muda mfupi, sheria ya miezi sita inabakia kama ilivyo.
Ndani ya kipindi hicho cha usajili wa muda na uhakiki, Tume ya Uchaguzi itakuwa imeshaanza taratibu za uchaguzi kwa kuruhusu wagombea waliopitishwa na vyama vyao kuanza kuchukua fomu.
Lakini uvumilivu uliwashinda CCJ ambao jana walimshukia Tendwa wakidai kuwa anadhofiisha mipango hiyo ya kukipa chama usajili wa muda kwa malengo anayojua mwenyewe.
Renatus Muabhi, ambaye ni katibu mkuu wa CCJ, alitoa tamko linalosema: "Hali iliyopo sasa imesababisha viongozi pamoja na wanachama watarajiwa wa CCJ kuwa katika hali ya utata na kuhofia mustakabali mzima wa upatikanaji wa usajili wa muda wa CCJ.
"Tunapata taarifa za maelezo ya msajili wa vyama vya siasa nchini yanayokinzana na wajibu wake kupitia vyombo vya habari pasipo sisi kuwa na taarifa yoyote inayoonyesha hatua ipi imefikiwa juu ya usajili wa CCJ.
"Kwa mfano, tarehe 26/01/2010 siku ya Jumanne gazeti la Daily News lilichapisha maneno ya msajili ambayo kwetu sisi yanatuingiza katika utata na hofu juu ya usajili wa chama chetu."
Tamko hilo linaendelea kueleza kuwa Tendwa anakwenda kinyume na taratibu pamoja na dhamana aliyopewa na kuhakikisha kwa vitendo ya kwamba nchi ya Tanzania ni ya kidemokrasia na inayofuata mfumo wa vyama vingi, badala ya kuwa mstari wa mbele kuhamasisha watu kuunda na kujiunga katika vyama vya siasa ili kuleta demokrasia ya kweli.
Linamtuhumu Tendwa kuwa anakatisha tamaa na kuwavunja moyo Watanzania kuhusu tafsiri ya kuanzishwa kwa CCJ hasa pale anaposema chama hicho ni sawa na vyama vingine vilivyopo.
0 comments