Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - MWANASHERIA Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema anaunga mkono muswada wa Simba kumpunguzia Rais madaraka

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema amesema kuwa anaunga mkono muswada wa Sheria ya Baraza la Usalama wa Taifa wa mwaka 2009 akisema si mbaya.

Muswada huo, uliowasilishwa Jumamosi iliyopita na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sofia Simba, ulikataliwa na Bunge kwa hoja kuwa unapunguza nguvu za rais na unamweka rais katika hatari ya kuondolewa wakati wowote na Baraza la Usalama.

Lakini Jaji Werema alisema jana kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma kuwa haoni ubaya kwenye muswada huo.

"Muswada si mbaya, lakini umerejeshwa kutokana na wabunge kutaka baadhi ya vipengele, hasa cha ukubwa wa baraza na Usalama na maamuzi ya mwisho virekebishwe," alisema Werema.

"Hakuna haja ya kujinyonga kwa kuwa muswada umekataliwa, zipo 'altenative' (njia) nyingine. Lakini muswada si mbaya, kazi yangu ni kuwasilisha miswada na kuwashauri mawaziri, si kutunga sheria. Wabunge ndio wana wajibu wa kutunga sheria na wametoa mapendekezo urekebishwe... kamati husika inafanyia kazi na utaletwa tena bungeni," alisema Jaji Werema.

Alisema kimsingi walichokifanya wabunge ni haki yao kama watunga sheria, lakini muswada huo hauna tatizo kama ulivyopitishwa katika michakato yote inayohitajika.

Mchangiaji wa kwanza baada ya muswada huo kuwasilishwa, Brigedia Hassan Ngwilizi alisema kuwa Baraza la Usalama linachukua ukubwa wa baraza la pili la mawaziri, jambo ambalo linatishia usiri wa mambo ya usalama wa nchi.

Ngwilizi pia alisema kuwa kipengele kinacholipa baraza nguvu ya kupiga kura ili kupitisha maamuzi makubwa kama ya kwenda vitani, kinamfanya rais, ambaye ni amiri jeshi mkuu, kuwa katika nafasi sawa na watu ambao wanatakiwa kutekeleza maamuzi yake, jambo ambalo linapoteza maana ya dhana nzima ya usalama wa taifa.

Pia kiongozi wa upinzani bungeni, Hamad Rashid alikwenda mbali zaidi na kuuita muswada huo kuwa wa kihaini kwa sababu linawapa wajumbe wa Baraza la Usalama mamlaka ya kupiga kura ya kumuondoa rais.

Waziri Simba alikubaliana na hoja za kuondoa muswada huo.
Naye Simba aliiambia Mwananchi jana kuwa ameridhika na muswada aliouwasilisha bungeni.

Alisema kupingwa kwa muswada huo kumetokana na makosa ya kiufundi baada ya kutopitishwa kwenye Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama inayohusika na suala hilo na badala yake kupitishwa na kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba tu.

Waziri Simba alitoa kauli hiyo mjini Dodoma jana katika mahojiano na Mwananchi ikiwa ni siku mbili baada ya muswada huo kupingwa na wabunge wakitaka kuondolewa kwa vipengere vinavyoingilia madaraka ya Rais.

"Niliusoma, niliridhika na muswada wa Sheria ya Baraza la Usalama wa Taifa, Siwezi kuleta kitu ambacho sijaridhika nacho," alisema Waziri Simba.

Aliongeza kusema kuwa "kuna tatizo sisi wahusika tuliliona, awali muswada huo haukupitia kamati husika ya Mambo ya nje Ulinzi na Usalama. Kuna tatizo... ofisi ya bunge, ilipaswa kuupeleka katika kamati hiyo ambayo ingepitia kwa pamoja na kamati ya bunge ya sheria na mambo ya katiba."

Hata hivyo, alisema kwa kuzingatia kanuni za bunge na kusikiliza maoni na michango ya wabunge, kwa kutumia busara na taratbu zilizopo aliahirisha hoja hiyo ili atafakari michango ya wabunge.

Wakati huo huo serikali imeahirisha mjadala wa sheria ya udhibiti wa matumizi ya fedha za uchaguzi uliokuwa ufanyike leo hadi Jumatatu ijayo kutokana na marekebisho madogo yanayofanywa katika muswada huo.
Tags:

0 comments

Post a Comment