IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
migogoro sasa ameendelea CCM, na kusababisha watendaji wakuu kwenye Jumuiya ya Wazazi na Wanawake kutimuliwa, huku makada saba wa chama hicho wilayani Kyela, Mbeya wakitupwa rumande kwa tuhuma za kufanya fujo na kuharibu mali.
Hali hiyo imetokea wilayani Sengerema, Mwanza ambako makada kata 20 wa chama hicho waliwekwa kitimoto na Kamati ya Usalama na Maadili ya chama kwa tuhumza za kuendesha kampeni za kumwondoa Ngeleja, wakati wilayani Nachingwea mkoani Lindi makatibu 12 wamesimamishwa kazi.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana zimeeleza kuwa CCM imewaondoa madarakani katibu mkuu wa Jumuiya ya Wazazi, Thabit Bushako na katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake (UWT), Husna Mwilima.
Kwa mujibu wa habari hizo, tayari CCM imemteua mwanachama wake mwingine kutoka Visiwani Zanzibar kuchukua nafasi ya Bushako.
Vyanzo kadhaa vya habari ndani ya jumuiya hizo mbili vimedokeza kuwa taarifa za mabadiliko ya katibu mkuu wa Jumuiya ya Wazazi zilianza kusambaa ndani ya ofisi hiyo yenye makao yake makuu Kariakoo jijini Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa mkutano mkuu wa Halmashauri Kuu (Nec), uliofanyika mjini Dodoma.
Ingawa chama hicho hakijatoa taarifa rasmi za mabadiliko hayo, jana Mwananchi ilielezwa kuwa tayari mrithi wa nafasi hiyo ameshawasili jijini Dar es Salaam na juzi alikuwepo kwenye ofisi hiyo akijiandaa kukabidhiwa ofisi.
"Katibu wetu mpya tayari ameshawasili na jana (juzi) alishinda hapa ofisini,"alisema mmoja wa maofisa katika ofisi hiyo ambaye hakutaka kutajwa gazetini na kumtaja aliyeteuliwa kushika wadhifa huo kuwa ni Hamisi Suleman Dadi kutoka Zanzibar.
Wakati hayo yakiendelea kwenye Jumuiya ya Wazazi, nako UWT mambo si shwari baada ya taarifa kueleza kuwa katibu wake mkuu Husna Mwilima, ameondolewa.
Hata hivyo alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, Mwilima alisema kiufupi kuwa: "Mmhh! napata utata kulijibu hilo, lakini niseme, kwa mujibu wa katiba ya UWT kikao cha kamati ya utendaji ndicho kinaweza kuniondoa".
Taarifa zimeeleza kuwa UWT inajiandaa kukutana na waandishi wa habari kutoa tamko rasmi kuhusu suala hilo leo.
Mkuu wa Oganaizesheni na mahusiano kwa Umma wa UWT, Sarah Msafiri aliliambia gazeti hili kuwa viongozi wa jumuiya hiyo wanatarajia kutoa ufafanuzi juu ya suala hilo leo kwenye mkutano wao na waandishi wa habari.
Wakati bundi huyo akizikoroga jumuiya hizo za CCM; taarifa kutoka wilayani Sengerema, zinasema kuwa zaidi ya makada 20 wa CCM wakiwemo wanaotuhumiwa kuendesha kampeni za kumng'oa Mbunge wa Jimbo la Sengerema, William Ngeleja kwa kufanya vikao vya kampeni usiku na mchana kinyume cha katiba ya CCM, waliwekwa kiti moto na kamati ya usalama na maadili ya chama hicho ngazi ya wilaya kwa zaidi ya saa nane.
Taarifa zinaeleza kuwa ajenda kuu za kikao hicho ilikuwa kujadili na kuwahoji wanachama hao kwa kufanya vikao isivyo halali na kuendesha kampeni chafu za kuwanadi baadhi ya wagombea wa ubunge katika Jimbo la Sengerema kabla ya muda, jambo ambalo ni kinyume cha katiba na kanuni za CCM.
Ajenda nyingine ni kuwahoji makada wanaodaiwa kuisaliti CCM wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwaka jana huku baadhi ya wanachama na makada wa CCM wakidaiwa kukisaliti chama kwa kusaidia kambi ya upinzani.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ambaye pia ndiye mwenyekiti wa kikao cha kamati hiyo, Jaji Tasinga alithibitisha kuwepo kikao hicho ofisini kwake na kusema kuwa baadhi ya ajenda zilihusu makada wanaotuhumiwa kucheza rafu kabla ya muda dhidi ya mbunge Ngeleja .
Aidha, Tasinga alikiri kuwepo kwa mahusiano mabaya kati yake na mbunge Ngeleja lakini, akakanusha kuhusika kumpandikizia wagombea kwa lengo la kumng'oa katika uchaguzi mkuu ujao.
Kikao hicho nyeti kimefanyika siku moja tu baada ya Katibu wa CCM wilaya, Marko Kahuruda kukiri kuwa baadhi ya makada wanadaiwa kuendesha kampeni chafu dhidi ya mbunge Ngeleja.
Huko Kyela makada saba wa CCM walikamatwa juzi na kutupwa rumande wakidaiwa kufanya uhalifu na fujo. Hata hivyo taarifa za ndani zinalihusisha tukio hilo na ugomvi uliopo baina ya kambi mbili mkoani humo kati ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile na Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe.
Makada hao walikamatwa juzi na kuswekwa rumande Jumatatu saa 3:00 usiku hadi juzi asubuhi walipofikishwa katika Mahakama ya Mwanzo ya Kyela mbele ya Hakimu Adam Mwanjokolo wakituhumiwa kufanya uharibifu na fujo.
Waliokamatwa na kisha kufunguliwa mashtaka ni pamoja na Mwenyekiti wa kata ya Kyela, Shaaban Mwambambale, Katibu Mwenezi wa kata ya Kyela, Richard Kilumbo, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi, Issa Mwanganya, Katibu tawi la Mikumi, Advent Mwakibinga, Katibu wa tawi la Nkuyu, Daudi Mwangalaba na Katibu wa tawi la Serengeti, Katembo.
Taarifa zilizopatikana baadaye zilieleza kwamba mvutano wa kiuongozi kati ya uongozi wa wilaya na ule wa kata ambao wote umegawanyika kimakundi ulisababisha kundi la makada hao kukamatwa baada ya kuhamisha ofisi yao ya kata na kuitenganisha na ile ya wilaya kama walivyokubaliana katika halmashauri kuu CCM kata ya Kyela.
Huko Nachingwea mkoani Lindi, makatibu kata 12 katika wilaya hiyo wamesimamishwa kazi baada ya kuhoji uhalali wa kulipwa fedha kidogo katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.Katika wilaya hiyo, CCM ina kata 24.
Viongozi hao watendaji wa kata pia wamedaiwa kufanya kikao kujadili suala hilo jambo ambalo uongozi wa wilaya ulilitafsiri kuwa ni kuwakashifu.
"Katibu wa CCM wilaya na Mbunge waliitisha kikao cha kamati ya siasa wilaya wakaamua tusimamishwe kazi, wakaanza kuwasimamisha makatibu 12 kati ya 24 wakidai sisi ni viongozi wa madai hayo," alisema mmoja wa makatibu hao aliyeomba kutotajwa jina gazetini.
Taarifa zinasema kuwa baadhi ya makatibu kata walioondolewa kwa kusimamishwa kazi tangu mwishoni mwa mwaka jana ni pamoja na katibu wa kata ya Nangoe aliyetajwa kwa jina moja la Mungele, Ali Napepa wa kata ya Nambambo na Lalo wa kata ya Namatula.
Wengine ambao pia wametajwa kwa jina moja ni Nkarombe wa kata ya Kiparomelo, Mlaponi wa kata ya Ndomoni, Lipumba wa kata ya Naipanga na Mtawala wa kata ya Mpirunge.
Hata hivyo makatibu hao wa kata tayari wamefikisha malalamiko ya kutoridhishwa na uamuzi huo kwa katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba.
Katika barua yao ambayo Mwananchi imefanikiwa kuiona, walidai uamuzi ni wa kionevu na unaaongeza makundi ndani ya CCM hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Walisema walifukuzwa kazi baada ya kuanza kudasi uhalali wa malipo hayo katika kikao kilichoitishwa na katibu wa CCM wilaya Nachingwea na Mbunge wa jimbo hilo, Mathias Chikawe.
Makatibu hao wamedai kuwa fedha wakati wa uchaguzi huo walilipwa Sh3,000 kila mmoja badala ya Sh5,000 iliyowekwa ili fedha inayobaki itumike kununua pikipiki kwa ajili ya Katibu mwenezi wa CCM wilaya.
Mmoja wa makatibu kata walio kazini aliyeomba kutotajwa gazetini alisema, " Kwa kweli siwezi kusema sana, hali ni mbaya wenzetu bado hawapo kazini kwa muda sasa, tuliwahi kufanya kikao wao wakafukuzwa hili linatupeleka pabaya."
Lakini katibu wa CCM mkoa wa Lindi Isaack Mgumba jana alikanusha taarifa hizo akisema, "Siyo kweli. Lakini mimi ndio nimerudi kutoka mkutano wa Nec Dodoma muda si mrefu, sijafika huko na nimelazwa hospitali kuchunguzwa afya yangu. Kazi ya kuteua makatibu kata ni ya CCM mkoa."
Habari zimeeleza kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba ana taarifa ya mgogoro huo na ameishaiagiza kamati ya maadili kuchunguza suala hilo.
You Are Here: Home - - Makatibu UWT, Wazazi CCM watimuliwa. wengine watupwa lupango
0 comments