Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Zitto aibuka tena, amvaa Dk Slaa aapa kumsaidia Kafulila

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Zitto aibuka tena, amvaa Dk Slaa aapa kumsaidia Kafulila
NAIBU Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe ambaye ameibuka na kudai kuwa kamwe hata acha kumsaidia Kafulila katika mapambano yake ya kisiasa.

ASEMA SIASA SI CHAGUO LAKE

Salim Said na Fidelis Butahe

NAIBU Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe ameibuka tena na kutonesha majeraha ya mgogoro uliokuwapo ndani ya chama chake, akisema haridhiki na uamuzi wa chama hicho kuwaengua David Kafulila na Danda Juju.

Ingawa Kabwe hakutaja jina, kauli yake kupinga maamuzi ya kuwavua madaraka wanachama hao; imeonyesha kumzungumzia Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willibrod Slaa kwa vile ndiye aliyesema Kafulila na Danda si kitu ndani ya chama hicho na kwamba, anaweza kuwashughulikia bila vikao vya chama.

"Mimi sipendi siasa za kinafiki, uamuzi wa kuwavua nyadhifa zao kina Kafulila haukuniridhisha kwa sababu haukuwa mzuri, ingawa ulipitishwa na mamlaka husika, katika vikao husika," alisema Kabwe katika kipindi cha Jambo Tanzania kilichorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC1) jana asubuhi na kuongeza:

"Unajua unaweza ukawa na maamuzi yaliyofanywa katika vikao halali, lakini yasikuridhishe, pia unaweza ukawa na maamuzi katika vikao hivyo hivyo yakakuridhisha. Lakini mimi sikuridhishwa na mamuzi ya kina Kafulila kuvuliwa nyadhifa zao."

Mwanasiasa huyo kijana, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mahesabu ya Mashirika ya Umma, alisema siku zote haridhishwi na siasa za kinafiki, ndio maana siasa haikuwa chaguo lake tangu mwanzo.

"Chaguo langu la kwanza lilikuwa ni ualimu na nilifundisha sana mimi, lakini pia napenda sana kusoma, kuandika na kutafiti, hivyo Watanzania wajue hilo kwamba siasa sio chaguo langu," alisema Kabwe.

Katika kile kinachoweza kuelezwa kuwa kuthibitisha kauli yake ya kutoshabikia siasa za kinafiki, Zitto alisema uamuzi wake wa kumsaidia Kafulila, umetokana na uwezo alionao kushika nafasi ya ubunge kupitia upinzani.

"Mimi naamini kuwa kujenga upinzani imara ndio tutaleta mageuzi ndani ya nchi, kwa hiyo nimeamua kumsaidia Kafulila kwa sababu ameingia upinzani, lakini, kama angeingia CCM nisingemsaidia," alisema Kabwe na kuongeza:

"Pia nilimwona ni kijana mwenye ‘commitment’ (mchapakazi). Mimi siamini kwamba Chadema pekee inaweza kuleta mabadiliko ndani ya nchi, bali kwa kujenga upinzani imara kuleta mabadiliko ni rahisi sana."

Zitto alikanusha madai kwamba, ndiye aliyemwingiza Chadema na kueleza kuwa alichofanya ni kumwandaa mwanasiasa huyo kijana kugombea ubunge jimbo la Kigoma Kusini.

"Namsaidia kwa sababu nilimwandaa kuwa mbunge, baada ya kumkuta makao makuu ya chama nikamchagua kuwa msaidizi wangu katika shughuli zangu za ubunge na hakuwa pekee alikuwa na wenzake, nikamuona anafaa kuwa mbunge," alisema Kabwe na kuongeza:

"Mimi nilipata safari ya kwenmda Ujerumani kusoma; kwa bahati mbaya huku nyuma akavuliwa nyadhifa zake ndani ya chama. Ingawa kuna watu wanasema alikuwa ameajiriwa; si kweli kwa sababu ndani ya Chadema hatuajiri."

Kabwe alifafanua kuwa aliamua kumsaidia Kafulila kwa sababu katika Jimbo la Kigoma Kusini ambalo kijana huyo anatarajia kugombea ubunge, kila mwaka wa uchaguzi kura zinagaiwa baina ya vyama vya CCM, NCCR na Chadema.

"Ninamsaidia Kafulila na nitaendelea kumsaidia kadri ya uwezo wangu, hilo naweka wazi kabisa," alisema Kabwe.

Kufuatia kauli na msimamo wake kuhusu maamuzi yaliyofanywa ndani ya Chadema, wadau mbalimbali wa masuala ya siasa walibahatika kutuma ujume wao wa maneno katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na TBC1, walitafsiri kuwa mwanasiasa huyo huenda anataka kuhama chama au kuacha siasa.

Zaidi ya jumbe fupi 100 zilizomuhusu Kabwe, zilitumwa TBC1 ambapo zilisomwa moja kwa moja na mtangazaji wa kipindi hicho jana, Marine Hassan Marine.

Yussuf Msaliko wa Tabora alisema, inavyoonyesha asilimia 80, Kabwe anaelekea kuhama ndani ya Chadema au kuacha siasa.

Samuel Thomas kutoka Arusha, alimtaka Kabwe kutoacha siasa na kumtaka aangalie vizuri chama chake kwani kimejaa ‘umimi’.

Mchangiaji mmoja kutoka Bukoba ambaye hakutaja jina lake, alimueleza Kabwe kuwa kuachana na siasa si mwisho wala njia ya kuepukana na maumivu ya serikali ya CCM.

Mchangiaji mwengine kutoka Tabata jijini Dar es Salaam alimueleza Kabwe kupitia ujumbe wake kuwa, “Kwa vile umeonyesha kutoridhishwa na maamuzi ya vikao vya chama chako, hapo hakuna ushirikiano na viongozi wenzako.”

Wachangiaji wengi walimuomba Kabwe kutoachana na siasa kwa sababu mchango katika sekta hiyo unahitajika ili kulipeleka mbele taifa changa la Tanzania, huku wengine wakimtaka aingie CCM.

Majina ya Kafulila na Zitto yalitawala vyombo vingi vya habari mwishoni mwa mwaka jana, baada ya Katibu Mkuu wa Chadema kuwavua nyadhifa zao Kafulila, aliyekuwa Ofisa Habari wa chama hicho na Danda Juju aliyekuwa Ofisa Mwandamizi wa Masuala ya Bunge.

Dk Slaa alinukuriwa akisema Kafulila na Juju ni sisimizi tu ndani ya Chadema. Aliwatimua kwa madai kuwa walikuwa wanavujisha taarifa za ndani ya chama kwa vyombo vya habari, jambo ambalo liliwafanya wanasiasa hao kuhamia NCCR-Mageuzi na kupata mapokezi makubwa na ya heshima.

Zitto aliondoka juzi usiku kwenda masomoni Ujerumani na anatarajiwa kurejea mwisho wa mwezi huu kuendesha vikao vya Kamati ya Bunge anayoingoza.

Tags:

0 comments

Post a Comment