Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - NCCR :Kafulila, Danda hawana ubavu wa kukigawa chama

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
NCCR :Kafulila, Danda hawana ubavu wa kukigawa chama

Fidelis Butahe na Salim Said

CHAMA cha NCCR-Mageuzi, kimesema makada wake wapya, David Kafulila na Danda Juju, walioteuliwa kushika nyadhifa katika mkutano wa Halmashauri Kuu uliofanyika kati ya Desemba 4 na 5 mwaka jana, hawana ubavu wa kukigawa chama hicho, kama ilivyoripotiwa jana katika gazeti moja la kila siku (si Mwananchi).

Kabla ya kujiunga na chama hicho, makada hao walikuwa katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kafulila akiwa Ofisa Habari na Danda akiwa Ofisa Mwandamizi wa Masuala ya Bunge.

Kuhamia kwao katika NCCR Mageuzi, kulikuja baada ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa, kuwaondoa katika nyadhifa hizho mwishoni mwa mwaka jana kwa maelezo kuwa walikuwa wakivujisha taarifa za chama katika vyombo vya habari.

Katika chama hicho walichohamia, Kafulila ameiteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Habari na Uenezi na Danda ameteuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi wa Organaizesheni na Uchaguzi.

Hata hivyo gazeti moja lilidai kuwa kitendo cha makada hao wageni ndani ya chama hicho kuteuliwa kushika nyadhifa hizo, kimewakera baadhi ya maofisa wa NCCR kiasi cha kusababisha mpasuko uliofikia hatua ya kuathiri utendaji wa pamoja ndani ya chama hicho.

Lakini akizungumza na Mwananchi jana, Katibu Mkuu wa NCCR , Samwel Ruhuza, alisema habari hizo ni za kinafiki na kwamba zimepangwa na baadhi ya watu.

Ruhuza alisema mpasuko ndani ya chama hicho ulikwisha tangu mwaka 1999.

"Tangu Mrema ang’oke NCCR mwaka 1999 hakuna tena mpasuko na hauwezi kutokea, hizo habari zimepangwa na wahuni tu wanaotaka kuona chama chetu kinayumba na hilo halitawezekana kwa kuwa tuko imara na tunafanya mambo kwa kufuata vikao na katiba ya chama," alisema Ruhuza

Akizungumzia uteuzi huo, Ruhuza alisema yeye ndio aliyewateua na kuyapeleka majina yao katika mkutano wa Halamshauri Kuu ambayo iliyapitishwa bila kupingwa.

Alisisitiza kuwa makada hao wangekuwa hawakubaliki wangepingwa na wajumbe wa mkutano wa Halmashauri Kkuu na kusisitiza kuwa suala la ugeni wa mtu ndani ya chama haliwezi kusababisha asiteuliwe kushika wadhifa wowote.

Tags:

0 comments

Post a Comment