Ivory Coast: Tutalipeleka kombe mlima Kilimanjaro | |||||||
KOCHA wa Ivory Coast, Vahid Halilhodzic amesema endapo atafanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Angola, watarudi Tanzania na kulipandisha kombe hilo kwenye mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu zaidibarani Afrika. Ivory Coast (The Elephants) ipo nchini na leo itacheza mchezo wa kirafiki na timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam kuanzia saa 1:30 usiku. Halilhodzic alisema watapanda mlima Kilimanjaro kwa sababu ndiyo mlima mrefu barani Afrika na wao wakiwa mabingwa itamaanisha wapo juu ya Kilimanjaro, juu ya Afrika. Alisema,"Tumefikia katika hoteli ya Kilimanjaro Kempinski na tunahisi tumeishafika juu ya mlima Kilimanjaro, tukirudi na kombe tutapanda nalo katika mlima huu mrefu barani Afrika na lazima nirudi na kombe kwa sababu Rais Laurent Gbagbo wa Ivory Coast amenitaka nirudi na kombe." Kocha huyo wa Ivory Coast ambaye ni raia wa Bosinia alisema,"Watanzania wengi wameonyesha kuiunga mkono Ivory Coast, lakini wamekuja Tanzania kwa ajili ya maandalizi tu, ila lengo lao kuu ni mashindano ya mataifa ya Afrika yatakayofanyika Angola." Halilhodzic alisema wachezaji wake wapo tayari kwa pambano la leo, ingawa walisafiri karibu siku nzima kutokea Ivory Coast mpaka kufika Dar. Alikiri kuwa wachezaji wake wanacheza mechi nyingi katika klabu zao na alikishangaa chama cha soka England FA kwa kuruhusu mchezaji mmoja kucheza mechi nyingi kwa wakati mmoja mfano Didier Drogba ambaye amecheza mechi nyingi kwa wakati mmoja, lakini alisisitiza mafanikio ya Ivory Coast yatatokana na wachezaji kuwa salama, kucheza bila kuumia. Alipoulizwa kama timu hiyo itakuja tena kuweka kambi itakapokuwa inajiandaa na fainali za Kombe la Dunia. Kocha huyo alisema,"Hapana, kwa sababu zipo fulsa nyingi, zipo nchi nyingi ambazo tunaweza kwenda, lakini bado hatujaamua, lakini tuliahidi kuja Tanzania na tumekuja na tutacheza mechi mbili." Naye kocha wa Taifa Stars, Mbrazil Marcio Maximo akiuzungumzia mpambano dhidi ya Ivory Coast, alisema mchezo huu ni muhimu kwa wachezaji wa Tanzania kwa sababu utawafunua kufahamu mambo mengi pamoja na mashabiki. Maximo alisema,"natarajia kuona soka nzuri, soka ya kiwango cha juu na soka ya haki, hii ni fulsa kubwa kwa mashabiki wa soka pia, kwa sababu Stars imewahi kucheza mchezo wa haki dhidi ya New Zealand, Ghana na Cameroon ambazo zote hivi sasa zipo kwenye fainali za Kombe la Dunia." Naye raisi wa Shirikisho la soka nchini Ivory Coast FIF, Jacques Anouma alisema,รข€tupo Tanzania kwa ajili ya maandalizi ya fainali za mataifa ya Afrika, kwa hiyo tunataka wachezaji wetu wawe watulivu na makini kwa ajili ya maandalizi." Alisema,"timu yetu imeshindwa kufanya mazoezi asubuhi kwa sababu ya mvua inayonyesha, ndiyo maana nahodha wa timu yetu Didier Drogba ameshindwa kuja kuzungumzia mchezo kwa sababu hivi sasa anafanya mazoezi ndani ya hoteli na wenzake." Pia rais wa Shirikisho la soka Tanzania TFF, Leodeger Tenga alisema wanajitahidi kuhakikisha timu hiyo yenye wachezaji wenye hadhi ya juu wanahudumiwa vizuri katika kipindi chote timu hiyo itakapokuwa nchini. Alisema,"Hii ni timu ambayo ipo katika viwango vya juu kabisa katika viwango vya ubora vya Fifa, ila natarajia vijana wa Stars wataionyesha dunia kuwa ni timu itakayokuja kuwa bingwa siku za usoni." Nahodha wa Stars, Shadrack Nsajigwa alisema,"wachezaji wa Ivory Coast hawajaja tu kufanya mazoezi kuna kitu kingine wamekiona kwa wachezaji wengine, tutawapa mazoezi mazuri, kwa sababu tutawapa upinzani na wala hatuwaogopi." |
You Are Here: Home - - Ivory Coast: Tutalipeleka kombe mlima Kilimanjaro
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
0 comments