Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Karume kutoongezewa muda wa urais

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema haitowezekana kumwongeza muda wa urais kwa vipindi vitatu, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Amani Abeid Karume. Pia kimesema ni ruhusa kwa wanachama wake kuanza kuonesha nia za kuwania nafasi za uongozi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu kwa kuwa hiyo ndiyo dalili ya vuguvugu la kisiasa nchini. Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa, alisema chama hicho kinaongozwa na kuendeshwa kwa mujibu wa Katiba ambayo imeonesha wazi kuwa Rais wa pande zote mbili anaweza kushika wadhifa huo kwa vipindi viwili tu kwa miaka mitano kila kipindi. “Katiba zote mbili zinazungumza wazi, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Zanzibar na tufahamu kuwa nchi yetu inaongozwa na Katiba hizi na sheria, hivyo jambo hili haliwezakani labda Katiba zibadilishwe,” alisema Msekwa jana ofisini kwake, Dar es Salaam. Alisema wadau wa siasa hawakatazwi kutoa maoni yao, lakini suala hili haliwezi kutekelezeka bila kubadilisha Katiba ambayo ubadilishwaji wake una mchakato mrefu. “Wananchi wote haijalishi itikadi zao, watambue kuwa haya mawazo hayana makosa ila kwa mujibu wa Katiba zote tunazozifuata sasa hayatekelezeki,” alisema. Alisema utaratibu wa kubadilisha Katiba utahitaji kushirikisha Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na Bunge, ambapo vyombo hivyo viwili kila kimoja kwa wakati wake kitabidi kikae na kujadili na kupitisha uamuzi na hata hivyo, lazima na vikao vya chama navyo vishirikishwe na kusikilizwa. Baadhi ya wanasiasa maarufu wa CCM na viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) hasa upande wa Zanzibar, hivi karibuni katika mkutano ulioandaliwa na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET), walitoa mapendekezo ya Rais Karume kuongezwa muda wa urais ambao kwa mujibu wa Katiba kipindi hiki kinachoishia mwaka huu ndicho cha mwisho kwake. Kati ya sababu ambazo zilitajwa na wanasiasa hao ni pamoja na upeo mkubwa alioanao Rais Karume kwa kuleta amani visiwani humo na hatua yake ya kushauri iundwe Serikali ya mseto itakayohusisha vyama vyote vya siasa nchini. Mkurugenzi wa Mambo ya Ndani wa CUF, Ismail Jussa, alikaririwa akisema kuwa kuna haja ya kiongozi huyo kuongezwa muda kwa ajili ya kushughulikia masuala ya amani visiwani humo. “Hakuna sababu ya kutompa nafasi ya kumalizia alichoanza, pia suala la maridhiano ni muhimu kuliko hata uchaguzi, kwani tumekuwa na uchaguzi mara nyingi, lakini umetugawanya tu badala ya kutuunganisha,” alisema. Pamoja na hayo, Msekwa alisema kwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu, wananchi wengi kuonesha nia zao za kuwania ubunge, udiwani na urais ni vizuri na ni ishara kuwa Tanzania mfumo wa siasa uko hai. “Hata hao ambao kwa sasa wameshika nafasi hizo wakilalamika kutokana na hawa walioanza kuonesha nia zao, pia ni sehemu ya vuguvugu la kisiasa, lakini mwisho wa siku unafahamika kupitia utaratibu wetu wa mchujo kwa hiyo hakuna haja ya kuwa na hofu,” alisema. Alisema utaratibu wa CCM ni ule ule wa miaka yote ambapo hata wakijitokeza wagombea 10 wa chama hicho kuwania nafasi moja, utafanyika mchujo na kubaki mmoja ambaye huungwa mkono na wote. “Hata wenyewe si mliona katika uchaguzi wa mwaka 2005 nafasi ya urais walijitokeza waombaji 11 lakini alipatikana mmoja kwa hiyo hii ni kawaida,” alisema. Kuhusu maandalizi ya chama hicho katika mwaka huu wa uchaguzi, Msekwa ambaye aliwahi kuwa Spika wa Bunge, alisema kutokana na uzoefu wa chama hicho katika uchaguzi hakina papara na tayari kimeshanunua magari kwaajili ya shughuli hiyo. Wakati wa uongozi wa Dk Salmin Amour ‘Komandoo’ aliyeongoza katika awamu ya tano visiwani humo – 1990 – 2000 -, liliwahi kujitokeza wqazo kama hili la kuongezwa muda lakini likazimwa kwa sababu kama hizi hizi.
Tags:

0 comments

Post a Comment