WATOTO wa ajabu waliozaliwa Zanzibar wakiwa wanatumia moyo mmoja na kuungana matumbo, wamefariki dunia baada ya umeme kukatika ghafla katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja.
Uchunguzi wa Tanzania Daima umegundua vifo hivyo vimetokea muda mfupi baada ya jenereta inayosambaza umeme katika hospitali hiyo kuzimika ghafla.
Watoto hao waliishi kwa saa 11 kabla ya kufa wakiwa wamehifadhiwa katika kifaa maalumu cha kisayansi kinachoongeza joto na kuwapa hewa ya oksijeni kama walivyokuwa wakiishi tangu walipozaliwa kwa njia ya upasuaji Januari mosi mwaka huu.
Vifo hivyo vimetokea huku watoto hao wakiwa hawajatenganishwa tangu walipozaliwa kwa njia ya upasuaji uliochukua zaidi ya saa 1:30.
Daktari mmoja katika hospitali hiyo alisema watoto hao wamekufa kwa kukosa hewa ya oksijeni na kuelemewa na joto baada ya umeme kukatika.
“Tunasikitika kukuambia kuwa watoto hao wamekufa kabla ya kutenganishwa baada ya umeme kukatika ghafla,” alisema daktari huyo ambaye alikataa kutajwa jina kwa kuwa si msemaji.
Alisema chombo maalumu kinachoongeza joto pamoja na kusaidia kupumua ndiyo nguzo pekee iliyokuwa ikishikilia uhai wa watoto hao, lakini walifariki dunia baada ya kuzimika kwa umeme.
Daktari huyo alisema ilikuwa vigumu kuokoa uhai wa watoto hao, kwa kuwa jenereta la dharura kwa hospitali hiyo ni moja na ilikuwa vigumu kutafuta mbadala wa umeme baada ya kuzimika.
Awali, menejimenti ya hospitali hiyo kupitia daktari wake Mwana Omar ulisema uwezekano wa kuwaokoa watoto hao ulikuwa mdogo kutokana na kutumia moyo mmoja na walikuwa wakifikiria kukaribisha utaalamu zaidi ikiwemo kutoka nje.
Suala la watoto hao limezua mjadala mkubwa katika Manispaa ya mji wa Zanzibar ambapo baadhi ya wananchi wanataka maeneo nyeti ikiwemo hospitali hiyo kuwepo na majenereta ya ziada kutokana na umuhimu wake.
Zanzibar ipo gizani kwa siku ya 25 kufuatia vifaa vinavyopokea umeme kutoka gredi ya taifa Kidatu kulipuka katika Kituo cha Fumba na kusababisha huduma muhimu za kijamii kuathirika.
0 comments