Usalama wazidi kuzorota nchini Yemen.
Majeshi ya Yemeni yalimzingira mtu alietuhumiwa kuwa kiongozi wa Al- Qaeda na yaliwateka wapiganaji watatu.Maafisa wa usalama wa Yemeni wamearifu kuwa tukio hilo lilitokea karibu na mji mkuu, Sanaa.
Majeshi hayo yameanzisha operesheni yenye lengo la kuwafagia magaidi wa Al-Qaeda ambao Yemen imesema walikuwa wamefanya mipango iliyosababisha vitisho vilivyozifanya balozi za nchi za magharibi zifungwe kwa muda.Hatahivyo balozi hizo ,za Marekani, Ufaransa na Uingereza zimeshafunguliwa tena.
Majeshi ya usalama yamesema yaliizingira sehemu moja katika mji wa Arhab, kilometa 60 kaskazini mashariki ya mji mkuu, Sanaa, ambapo mtu aliekuwa anatuhumiwa kuwa kamanda wa Al-Qaeda alikuwa amejificha katika nyumba moja.
Maafisa wa serikali ya Yemeni wamearifu kuwa mtuhumiwa huyo, Mohammad al Hang, ambae ni kiongozi wa ngazi za juu, alilengwa katika shambulio lililofanywa mapema wiki hii.
Wapiganaji watatu waliojeruhiwa mapema wiki hii walikamatwa baada ya kuonekana katika hospitali moja.
Hali nchini Yemen imezidi kuwa mbaya kiasi cha kutushia usalama wa eneo la Bara -Arab na dunia nzima. Hayo amesema katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.
Habari zinasema afisa mmoja na polisi wawili wameuwa kusini mwa nchi.
Wakati huo huo, habari zaidi zinasema harakati za wanaotaka kujitenga zinatokota kusini. Katika mji wa Aden, kusini mwa nchi, polisi walimtia ndani bwana Hisham Bahraheel, mhariri wa gazeti la Al Ayyam .Gazeti hilo limepigwa marufuku kutokana na kuchapisha habari juu ya harakati za wanaotaka kujitenga. Ofisi ya gazeti hilo palikuwa mahala pa harakati za upinzani ambao umekuwa unafanyika kwa siku kadhaa.
Askari mmoja na mlinzi waliuawa.
Mnamo siku nne zilizopita Yemen imekuwa inapeleka majeshi kushiriki katika operesheni dhidi ya Al-Qaeda katika majimbo matatu ya nchi hiyo.Yemen, ambayo sasa inakabiliwa na kupungua kwa mafuta, na wakati ambapo inakabiliwa na mgogoro wa maji, imeimarisha usalama kwenye pwani yake ili kuwazuia wapiganaji kutoka Somalia kuingia nchini humo
Serikali ya Yemen imekiri kwamba inahitaji msaada wa Marekani katika kupambana na magaidi lakini serikali ya nchi hiyo imesema haina raslimali inazohitaji ili kuweza kupambana na umasikini jambo linalowawezesha Al-Qaeda kuwaandikisha wapiganaji nchini humo.
0 comments