IKIWA imebaki miezi tisa kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu, joto linaonekana kupanda huku baadhi ya wabunge wakiamua kuanza kampeni kabla ya wakati kuhakikisha wanaendelea kubaki madarakani.
Wakati wengine wameamua kupiga kambi majimboni na kushiriki katika kazi mbalimbali za maendeleo na wapiga kura, wengine wamefikia hatua ya kuchapisha nyaraka na kuzisambaza kabla ya filimbi ya kampeni kuanza.
Mbunge wa Jimbo la Kalambo mkoani Rukwa, Ludovick Mwananzila ni mmoja wa wabunge walioamua kuchapisha kalenda za Chama Cha Mapinduzi (CCM) zenye picha yake, zikiwahamasisha wananchi wamchague yeye na chama chake katika uchaguzi mkuu ujao.
“2010 ni mwaka wa uchaguzi, chagua CCM, chagua Ludovick Mwananzila (Mb), Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Rukwa na Wilaya ya Sumbawanga”, “Maendeleo ya Jimbo la Kalambo yataletwa na wananchi wenyewe, chagua mpenda maendeleo Mwananzila,” hayo ni maneno yaliyopo katika kalenda hiyo yenye nembo na rangi za chama hicho tawala pamoja na picha ya Mwananzila.
Mmoja wa wananchi (jina tunalihifadhi) alilipasha Tanzania Daima Jumatano kwamba mbunge huyo ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wakati wa uteuzi wa kwanza wa serikali hii ya awamu ya nne, amekuwa akizisambaza bure kalenda hizo kwa wapiga kura wake.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano kuhusiana na madai ya kuanza kufanya kampeni kabla ya wakati, mbunge huyo alikiri kuhusika na kalenda hizo na kwamba amefanya hivyo kwa makusudi kwa ajili ya kukisaidia chama chake.
“Ninakisaidia chama changu, ndiyo nimeandika hivyo kwani nikifanya hivyo kuna ubaya gani? Nakisaidia chama changu. Mbona CHADEMA wanafanya hivyo, mimi nikifanya hivyo ni vibaya?” alizungumza kwa ghadhabu mbunge huyo.
Tanzania Daima Jumatano ilipotaka kujua iwapo anajua anatenda kosa kwani hata chama hakijaridhia usambaji wa vipeperushi kabla ya kampeni, hakutaka kuzungumza chochote zaidi ya kusema kwamba anajiandaa kumpokea Waziri Mkuu, Mizengo Pinda hivyo hana nafasi ya kujadili suala hilo.
“Kwanza sina muda wa kuongea, nina shughuli nyingi, tuko kwenye maandalizi ya kumpokea Waziri Mkuu,” mbunge huyo alisema na kukata simu.
Hata hivyo, Katibu wa CCM Mkoa wa Rukwa, Kapteni F. Kiwango alipotafutwa kuelezea suala hilo, alikiri kusikia taarifa hizo na mhusika wa kalenda hizo (Mwananzila) amemthibitishia kuwa ni zake.
Alisema CCM mkoani humo hairuhusu kampeni kabla ya wakati bila kufuata utaratibu na kuahidi kwamba kwa nafasi yake ataitisha mkutano kujadili suala hilo mara moja.
“Taarifa hizo nimezipata, lakini kalenda zenyewe sijaziona. Niliwasiliana na Mwananzila mwenyewe na kunithibitishia kwamba ni yeye anayehusika. CCM hairuhusu kampeni kabla ya wakati. Ni jukumu langu kama katibu wa mkoa kushughulikia jambo hili,” katibu huyo alilieleza Tanzania Daima Jumatano kwa njia ya simu.
Alibainisha kuwa mbunge huyo hapaswi kufanya hivyo kwani alichaguliwa afanye kazi hadi kipindi chake kitakapomalizika ndipo aanze kampeni.
Kwa upande mwingine uongozi wa ofisi ndogo ya makao makuu ya CCM, Dar es Salaam walipoonyeshwa kalenda hiyo, ulionyesha kustushwa nayo kwa madai kuwa chama hakina programu hizo kwani hilo pia ni jukumu la Tume ya Uchaguzi (NEC).
Mmoja wa maofisa katika kitengo cha propaganda makao makuu yaliyopo Lumumba jijini Dar es Salaam, Violet Mzindakaya alilieleza gazeti hili kuwa katika ngazi zozote zile, CCM haina mgombea kwa sasa.
“CCM haina mgombea katika ngazi yoyote ile kwa sasa. Si bara wala Zanzibar. Angalau Rais Jakaya Kikwete anaweza kusema kutokana na utaratibu uliopo ndani ya chama chetu ambaye naye hajitangazi,” Mzindakaya alisema.
Uchunguzi wa Tanzania Daima Jumatano umebaini kwamba kinyang’anyiro cha kupata wabunge na madiwani mwaka huu kitakuwa kigumu sana kutokana na mikakati ambayo wabunge walioko madarakani wamejiwekea huku wanaowania nafasi hizo nao wakijipanga kuhakikisha wanaingia bungeni.
0 comments