Uchina imemwita balozi wa Marekani mjini Beijing kulalamikia juu ya mpango wa Marekani wa kuidhinisha mauzo ya silaha kwa Taiwan, kisiwa ambacho Uchina inakitambua kama sehemu ya nchi yake.
Silaha hizo ambazo zinajumuisha ndege za helicopter aina ya Black Hawk, makombora aina ya Patriot, na tiknolojia ya mawasiliano ya kijeshi zitagharimu zaidi ya dola billioni sita.
Naibu Waziri wa mambo ya kigeni wa Uchina, He Yafei, alimwambia balozi wa Marekani, Jon Huntsman, kuwa mauzo hayo yanaweza kuwa na athari mbaya kwa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili tayari unagubikwa na mzozo kuhusu biashara na udhibiti wa mtandao wa internet.
Marekani imesema kuwa ina wajibu kisheria kuisaidia Taiwan kujihami, kulingana na sheria iliyopitishwa mwaka wa 1979.
0 comments