Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - CUF yaridhia kura ya maoni Zenji

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
HATIMAYE Chama cha Wananchi (CUF), kimeridhia hoja iliyokuwa ikikwamisha utekelezaji wa makubaliano ya muafaka namba tatu kati yake na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhusu kufanyika kwa kura ya maoni ya wananchi juu ya hoja ya kuundwa kwa serikali ya mseto.

Kwa muda mrefu chama hicho cha upinzani, kimekuwa kikipiga chenga hoja hiyo kama tiketi ya kuundwa au kutoundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa katika visiwa vya Zanzibar, kwa madai kuwa huenda CCM itatumia hila, kuvuruga matokeo ya kura hizo.

CCM kupitia Halmashauri Kuu ya Taifa ilipitisha uamuzi wa kutaka kuitishwa kwa kura ya maoni, ili kutekeleza hoja ya kuundwa kwa serikali ya mseto visiwani humo, kama ilivyokubaliwa katika muafaka namba tatu.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu kutoka Zanzibar jana, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema chama chake kimeelewa suala ya kura za maoni.

"Suala la kura ya maoni sisi tumeshalielewa sasa, pale mwanzoni tulilikataa kwa sababu halikuletwa katika vikao vya mazungumzo ya muafaka baina ya pande mbili husika," alisema profesa Lipumba.

Alisema kwa sasa hilo limeeleweka ndani ya CUF kwa kuwa limewasilishwa mapema na kwamba halina nia mbaya kama ilivyokuwa katika muafaka namba tatu.

"Kwa hiyo sisi tumekubali kufanyika kwa kura ya maoni," alisema kiongozi huyo wa CUF.

Alisema, kura hizo za maoni kupata ridhaa ya wananchi kuhusu kuundwa kwa serikali ya mseto visiwani Zanzibar, zitafanyika kabla ya uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika, baada ya kumalizika kwa kipindi cha Rais Aman Karume.

"Malengo ya pande zote mbili ni kufanyika kwa kura za maoni kabla ya uchaguzi mkuu, ili serikali ya mseto iweze kuundwa kabla ya uchaguzi huo," alisema Profesa Lipumba.

Alisema hoja ya kura ya maoni iliyoibuliwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya Tauifa ya CCM huko Butiama mwaka 2008, haikuwasilishwa katika vikao vya pamoja na kwamba ilikuwa na lengo la kuipiku CUF, jambo ambalo walilipinga.

Profesa Lipumba ambaye alienda Zanzibar juzi, alisema amekua akifuatilia kwa makini mjadala kuhusu hoja binafsi ya kiongozi wa kambi ya upinzani katika Baraza la Wawakilishi, Abubakar Khamis.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo mjadala huo haukuwa mkali na wala haukugonganisha vichwa vya wajumbe wa baraza la wawakilishi.

"Mjadala nimeufatilia vya kutosha tangu jana (juzi) nipo hapa Zanzibar na haukua mkali, wala hakuna tatizo lolote la msingi la kukwamisha hoja binafsi ya mheshimiwa kiongozi wa kambi ya upinzani."

"Wawakilishi wote waliochangia na hata wale wachache walionekana kupinga baadaye waliunga mkono baada ya kujiona wako pekoe yao, lakini hata wajumbe wengi wa baraza la mawaziri wa Zanzibar wameonyesha kuunga mkono," alisisitiza Lipumba.

Kuhusu kauli ya waziri Mkuu Mizengo Pinda kwamba serikali ya Muungano inasubiri uamuzi wa CCM kuhusu suala la maridhiano ya Zanzibar na kwamba serikali hiyo, inapongeza hatua ya kufikiwa kwa maridhiano baina ya wazanzibari, Profesa Lipumba alisema kwa vile Rais Jakaya Kikwete ameridhia suala hilo hana wasiwasi.
Tags:

0 comments

Post a Comment