Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Sasa imekuwa ni Kama T.S.U. ni kupigana waraka kwa kwenda mbele...

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Waraka wasambazwa kuitafuna CCM 2010,kanisa Katoliki laukana
Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa. CCM kimeundiwa zengwe la kusambazwa kwa waraka wenye lengo la kupotosha jamii ili wananchi wasikichague mwakani

SASA WAANZA KUWASAKA WANAOSAMBAZA

Daniel Mjema

IKIWA imebaki takribani miezi 10 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu, waraka mzito unaodaiwa kuwa wa Kanisa Katoliki umeanza kusambazwa nchini ukiwahamasisha waumini wake kutoichagua CCM.

Waraka huo unadai suala la kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na serikali kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC) ni mambo yaliyokataliwa na kanisa, lakini serikali ya awamu ya nne imepuuza kauli hiyo ya kanisa.

Kadhalika waraka huo unaenda mbali na kudai kuwa vyama vya CCM na CUF kwa sasa havifai kwa kanisa kwa kuwa vimekuwa mithili ya mbwa mwitu aliyejivika ngozi ya kondoo, huku ukitahadhariha kuwa Mahakama ya Kadhi na OIC ni hatari kwa Ukristo.

Hata hivyo, rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Mhashamu Askofu Yuda Thadei Ruwa'ichi ameukana waraka huo akisema ni 'feki' na kutaka vyombo vya dola kuwatafuta na kuwakamata wanaousambaza.

"Oktoba mwaka huu lilishafanyika jaribio la kusambaza misikitini waraka feki kama huo, lakini sisi kama kanisa tunasema kama ni waraka wa Wakristo hauwezi kusambazwa misikitini bali makanisani," alisema Askofu Ruwa'ichi alipoongea na Mwananchi.

Askofu Ruwaichi alisema kama ulivyokuwa waraka ule wa Oktoba ambao aliuelezea kuwa haukuwa wa kanisa hilo, waraka unaosambazwa sasa pia si wa kanisa na kuwataka Watanzania kuwa makini na watu wasiolitakia mema taifa.

Rais huyo wa TEC alisema wapo watu wanaojaribu kuchezea waraka halali uliotolewa na kanisa hilo ambao mtu yeyote akiusoma ataona kanisa halina shida na mtu mmoja mmoja wala halina mgogoro na dini nyingine.

"Nawaomba wananchi ambao tayari waraka huo umefika mikononi mwao, wauchunguze vizuri na wamchunguze vizuri mtu anayewapitishia karatasi hatari kama hiyo, kwa sababu ana lengo la kuwapotosha kwa maslahi yake," alisema.

Waraka huo wenye kurasa tatu ambao Mwananchi imefanikiwa kupata nakala yake unatanguliwa na maandishi yanayosomeka: "Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC). Huduma ya Kichungaji katika jamii kuelekea uchaguzi mkuu 2010."

Kwa mujibu wa maelezo ya waraka huo, ambao inadaiwa kuwa umetolewa na Tume ya Haki na Amani ya TEC, unasambazwa kwa siri kwa maaskofu, mapadre na wachungaji kote nchini na inadaiwa kuwa mtu wa kawaida haruhusiwi kuupewa.

Waraka huo ambao umesambazwa pia katika misikiti mbalimbali wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro, umegusia suala la vita dhidi ya ufisadi ukisema kuendelea kuikumbatia CCM ni hatari kubwa kwa kanisa.

"Kama kanisa litakuwa kimya bila kulidhibiti, basi kanisa litachafuliwa kwa njia moja au nyingine," unasema waraka huo ukisisitiza kuwa huu ni wakati wa kanisa kushika hatamu ya uongozi wa nchi.

Waraka huo unaendelea kudai kuwa chini ya awamu ya tatu ya Rais Alli Hassan Mwinyi, kanisa liliweza kudhibiti na kurudisha heshima yake lakini katika awamu ya nne kumekuwa na udhalilishaji wa kanisa wa kiwango cha juu.

"Mwelekeo wa kanisa kwa sasa ni kuelekeza nguvu zetu kwa wakristo wote Tanzania kwa chama chetu cha CHADEMA katika uchaguzi ujao ili maslahi ya kanisa yarudi kama zamani,” unadai waraka huo.

Waraka huo umevuja zaidi katika misikiti mbalimbali ya Jimbo la Mwanga linaloongozwa na Profesa Jumanne Maghembe.

Habari za uhakika zilizopatikana jana zimelidokeza Mwananchi kuwa Desemba 20 mwaka huu, waraka huo ulisomwa katika harambee ya kuchangia ujenzi wa msikiti katika eneo la Tingatinga lililo Kifaru mkoani Kilimanjaro.

Hata hivyo, Prof. Maghembe anayedaiwa alikuwepo katika harambee hiyo amekana kuufahamu au kuuona na kuna habari kuwa sumu yake imeanza kutafuna kampeni za chini za ubunge wilayani Mwanga.

"Sijauona huo waraka kama uko Mwanga nitaupata," alisema Profesa Maghembe ambaye pia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi katika ujumbe wake mfupi wa maandishi alioutuma Mwananchi alipoombwa ufafanuzi.

Mwanasiasa mkongwe nchini, Peter Kisumo jana alithibitisha kuuona waraka huo na kueleza kwamba umeshasambaa maeneo mengi ya wilaya ya Mwanga, lakini akasema anavyouona si waraka rasmi wa kanisa.

"Hata kama Kanisa litasema ni feki lakini 'damage' (uharibifu) ni mkubwa umeshasambaa na ni hatari sana… linatakiwa jicho la karibu sana kwa sababu mwelekeo huo ukiachiwa unaweza kusababisha umwagaji wa damu," alisema.

Mwenyekiti wa CCM mkoani Kilimanjaro, Vicky Nsilo Swai hakutaka kuzungumzia suala hilo alipoulizwa na Mwananchi kama ana taarifa na waraka huo, badala yake akataka Mwananchi iwasiliane na Kanisa Katoliki kwa kuwa ndilo linaguswa.

"Kauli ya kanisa katika hilo ni 'very important'(muhimu sana ); wakubwa hao ndio wanatakiwa waseme kwa sababu linagusa kanisa lakini ifahamike pia Tanzania haiendeshwi kidini tuna katiba na sheria zetu," alisema.

Mpaka jana mchana ilikuwa haijaweza kufahamika sababu hasa za waraka huo kuanza kusambaziwa Mwanga, japo maudhui ya waraka wenyewe umeelekezwa kwa maaskofu, mapadre na wachungaji nchi nzima.

Tags:

0 comments

Post a Comment