Swahiba wa Zitto Kbwe ajitoa uanachana Chadema |
Na Ramadhan Semtawa MSHIRIKA wa mkubwa kisiasa wa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe, David Kafulila, ametangaza uamuzi mzito wa kujitoa katika chama hicho huku akidaiwa kujiandaa kukimbilia NCCR Mageuzi. Uamuzi huo ambao unatokana na majeraha ya uchaguzi mkuu wa Septemba, umekuja siku chache baada ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Wilbroad Slaa kutengua ajira ya Kafulila ambaye alikuwa ni Afisa Habari na Danda Juju, aliyekuwa Afisa Mwandamizi wa mambo ya Bunge. Wakati uamuzi huo umeibua hisia na misimamo tofauti ndani ya Chadema huku wenyeviti 11 wakidaiwa kumpinga Dk Slaa, jana Kafulila aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kutangaza msimamo huo wa kujitoa Chadema na kumshambulia Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na Dk Slaa. Ingawa alisita kuweka bayana wapi atakimbilia, lakini habari zilizotufikia zilidokeza kwamba, anajianda kukimbilia NCCR-Mageuzi, ambacho kina nguvu Kigoma Kusini anakotarajia kuwania ubunge mwakani. Hata hivyo, Kafulila alisema alifikia uamuzi huo baada ya kuona lengo lake la kujenga upinzani imara linahujumiwa na Dk Slaa kwa kumwekea uzio asiweze kuchaguliwa. Akitangaza uamuzi huo alisema: "Kwa dhamira yangu binafsi, baada ya kukaa kufikiria na kisha kujiridhisha na kupata ushauri kwa watu ninaowaheshimu sana, nimeamua kujitoa Chadema kuanzia leo, ... mimi si mwanachama wa Chadema," alitangaza Kafulila na kufanya ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo kuzizima na kuongeza: “Ni uamuzi mzito, lakini roho yangu ni nyeupe, sina kinyongo na mtu nimefanya uamuzi huu kwa nia ileile na sitatoka nje ya mstari,... lengo ni kujenga Strong Opposition (upinzani imara) nchini. "Sijasukumwa na mtu, ni uamuzi ambao umeanzia katika nafsi yangu mwenyewe, ikaja ngazi ya familia na kuendelea juu. "Nimeondoka Chadema, ila natoa rai kwa wanachama hasa vijana wenzangu kwamba, uhai wao ndani ya chama hicho utategemea sana utiifu wao wa, zidumu fikra za Mwenyekiti Mbowe na Katibu Mkuu Slaa. “Nataikumbuka Chadema kwa kuwa mnamo Desemba7, 2008, damu yangu ilimwagika wakati wa utumishi wangu katika kazi ya ujenzi wa chama hicho." Kafulila mwenye uwezo mkubwa wa kujenga hoja, kuchapa kazi, alisema uamuzi huo umeangalia mbali kutokana na kuona dhahiri amenyang'anywa fursa ya kuchaguliwa na kubakiziwa ile ya kuchagua tu. Kafulila ambaye aliwahi kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Taifa la chama hicho (Bavicha) katika uchaguzi wa chama hicho hivi karibuni ambayo matokeo yake yalibatilishwa, alidai kuwa hatua ya Dk Slaa ilimuondolea nafasi ya kuchaguliwa na kufifisha ndoto yake ya kujenga upinzani imara nchini. "Lengo langu limekuwa ni kujenga upinzani imara, lakini niliondolewa fursa hii ndani ya Chadema, katiba ya Chadema inataja mwanachama anaweza kuondoka kwa kujiondoa au kuondolewa kwa kifo kama Chacha Wangwe, sasa mimi nimejiondoa mwenyewe siyo kifo," alifafanua Kafulila. Alidia kwamba, alifukuzwa uanachama kwa siri ikiwa ni kwasababu ya uongozi mbovu Mbowe. " Si mwanasiasa (Mbowe) ni mfanyabiashara, yuko radhi abaki na wabunge wawili ili aangalie biashara zake, lakini si maslahi ya chama." Kafulila aliongeza kwamba, kiutaratibu wanachama wote wa Chadema wako chini ya uongozi wa chama, lakini yeye akatakiwa awe nje ya uongozi wa chama. Alisema kuwa chuki na baadhi ya viongozi hao wa juu, kwamba inatokana na msimamo wake wa kuhoji matumizi ya fedha za chama, zikiwemo Sh35 milioni, za ruzuku ya Desemba ambazo mpaka sasa hazijulikani zilipo. Alifafanua kwamba, watia saini katika hundi za kuchukua fedha za ruzuku ya chama ni Mbowe, Dk Slaa na Anthony Komu, na kuhoji Mwenyekiti kuwa mtia saini wakati yeye ndiye anapaswa kuiwajibisha Sekretarieti endapo itafanya ufisadi. Kafulila alimtaka Mbowe kujiondoa kwenye orodha ya watiaji saini, kwani huko ni kukiuka taratibu za uendeshaji taasisi. “Ajifunze kwa CCM, NCCR, CUF. mbona Lipumba (Ibrahim), Mbatia (James) si watia saini; kwanini yeye ang'ang'anie?" alihoji na kudai: "La kushangaza watia saini katika fedha za mfuko wa kuchangia chama kwa njia ya SMS pia ni Mbowe na Komu tu; hata hivyo, watu hawa wawili hawakuteuliwa na kikao chochote kufanyakazi hiyo". Alisema Mkurugenzi wa Fedha (Komu), ndiye mwamuzi kwa kiasi kikubwa katika hatua zote za kuandaa bajeti, kuchukua fedha benki, kuidhinisha matumizi na kufanya maamuzi. " Hii ni kinyume na utaratibu wa kanuni za matumizi ya fedha za taasisi," alidai Kijana huyo ambaye aliwahi kuanguka kutoka ghorofa ya kumi akifanya kazi ya kuimarisha Chadema, alisema aliwahi kuhoji fedha hizo, lakini akazimwa na kuelezwa kwamba, yeye ni mwandishi wa muhtasari wa vikao na si mjumbe hivyo akae kimya. "Nilimwambia Dk Slaa, siwezi kukaa kimya kuzungumzia mambo ya msingi, ni bora niende kuwa mfagiaji kuliko kuzuiwa kusema ukweli unaohusu chama," alidai. Kafulila aliongeza kwamba, alishangazwa pia na mwendelezo wa chuki dhidi yake ambao ulikuwa ukifanywa na Dk Slaa, kwa kutaka kumchukulia hatua kwa madai ya kumpigia kampeni Zitto, wakati uchaguzi ulikwishapita. "Dk Slaa alinihoji na kutaka kunichukulia hatua kwasababu nilishiriki kumfanyia kampeni Zitto Kabwe. Lakini John Mrema, John Mnyika, Komu na Benson Kigaila waliokuwa wakimfanyia kampeni Mbowe hawakuhojiwa," alidai na kuongeza: "Haki haikutendeka kwa kuwa sisi sote tulikuwa watendaji wa makao makuu ya chama. Moja ya sababu kuu iliyonishawishi kumuunga mkono Zitto ni hoja yake aliyotoa bungeni kutaka CAG akague matumizi ya fedha za ruzuku za vyama vya siasa. Ni Ukweli usiopingika inawezekana Chadema kuwa kati ya vinara katika taasisi zenye matumizi mabaya ya ruzuku". Hii ni hatua nyingine ya Chadema kupita katika wakati mgumu kisiasa, baada ya kukumbwa na hali kama hiyo wakati wa akina Dk Amani Walid Kabourou ambaye alijitoa Chadema kutokana na kutoelewana na baadhi ya viongozi wa juu. Kujitoa kwa Kafulila ni matokeo ya majeraha ya uchaguzi wa Septemba, ambayo Baraza la Wazee wa chama hicho wakiongozwa na mzee Edwin Mtei, ambao waliokoa jahazi katika uchaguzi uliopita kwa kumshauri Zitto amwachie Mbowe nafasi ya uenyekiti taifa. |
You Are Here: Home - - wwalionyang;anywa vyeo Chadema mmoja wao akiacha chama. kukimbilia NCCR
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
0 comments