Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Mdogo wa Kingunge amponda Sofia Simba

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Mdogo wa Kingunge amponda Sofia Simba
Na Fidelis Butahe

KADA wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Enock Ngombale, ameibuka na kumshutumu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sofia Simba kuwa ni miongozi wa viongozi wasiofaa katika utawala wa serikali ya awamu ya nne.

Ngombale ambaye ni mdogo wake mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru alienda mbali na kudai kuwa kuwepo kwa viongozi wasiofaa kunatokana na serikali kuwa dhaifu katika suala zima la kuteua viongozi.

Akizungumza katika Ofisi za Mwananchi jana, Ngombale ambaye aliwahi kuwa Naibu katibu uenezi taifa wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) mwaka 1996-2002 alisema kitendo cha Waziri Simba kuwatetea mafisadi na kuwaponda wale aliowaita kuwa wako mstari wa mbele katika vita hiyo amedhihirisha kuwa ni miongoni mwa viongozi wasiofaa ndani ya serikali ya rais Kikwete.

Hivi karibuni waziri Simba alitoa tuhuma nzito kwa Mbunge wa Same Mashariki, Anna Kilango pamoja na John Malecela na kudai kuwa licha ya kuwa wanapambana na ufisadi, lakini katika harusi yao walipewa fedha na mafisadi.

Katika tuhuma hizo waziri Simba hakuishia hapo aliwarushia makombora vinara na wapambanaji mahiri wa ufisadi nchini akiwemo mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi pamoja na Mbunge wa Kyela, Harrison Mwakyembe.

“Mama Kilango, Spika wa Bunge, Samwel Sitta, ni miongoni mwa viongozi walio mstari wa mbele kupambana na ufisadi , lakini inasikitisha anapotokea mtu mwenye nyadhifa ya utawala bora nchini anapoibuka na kuwapinga watu kama hawa na kuanza kuwatetea mafisadi, nasema huyu ni mmoja wa viongozi wasiofaa ndani ya serikali ya Kikwete” alisema Ngombale na kuongeza;

“Serikali nayo inatakiwa kuwa na maamuzi makini kwa sababu kamati ya Bunge iliundwa na ilitoa ripoti ya uozo uliokuwepo katika Kampuni hewa ya Richmond, lakini maazimio yake serikali inasuasua kuyatekeleza hadi mtu mmoja ambaye anatuhumiwa katika kashfa hiyo anadiriki kusema iundwe tume huru ya majaji kuchunguza upya sakata hilo”

Akizungumzia kamati ya rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi iliyoundwa kwa ajili ya kuchunguza mpasuko ndani ya CCM, Ngombale alisema kamati hiyo haina manufaa yeyote na kudai kuwa imeundwa kwa ajili ya kuwadhoofisha vinara wa kupambana na ufisadi.

“Kamati ya Mwinyi imeundwa kwa makusudi ya kudhoofisha wabunge wanaopambana na ufisadi ili kuwapa mwanya wabunge wanaokumbatia ufisadi wapate nafasi ya kuwapaka matope wale wanaopambana na ufisadi, kamati inasaidia nini mbona mpasuko bado mkubwa, tujiulize mpasuko umekwisha au chuki ndio inashamiri” alisema Ngombale

Alisema kundi la viongozi wasiofaa katika serikali ya awamu ya nne kama likipita katika uchaguzi mkuu ujao ni wazi kuwa taifa litaelekea katika hatua mbaya na kuwataka watanzania kusoma vizuri Waraka wa kanisa katoliki unaoonyesha sifa za kiongozi bora ili waweze kufanya uchagua sahihi katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa Oktoba 2010.

Tags:

0 comments

Post a Comment