Rais Jakaya Kikwete ameahidi kuwa kama akijaliwa kupata kipindi cha pili cha kuiongoza Tanzania, atafanya jitihada kubwa kuubadilisha uongozi kuwa wa vijana.
Akizungumza na vijana kutoka nchi kadhaa za Afrika juzi jijini Dar es Salaam, Rais Kikwete pia alisema vijana ndiyo Tanzania ya kesho, na kama nchi haitawekeza vya kutosha kwa vijana na maendeleo yao, basi itakuwa haiwekezi katika hali yake ya baadaye.
Katika mkutano huo wa Mpango wa Kulea Uongozi wa Afrika ambao unadhaminiwa na Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa Anglikana wa Afrika Kusini, Desmond Tutu, Rais Kikwete alisema anauthamini mpango huo na kusisitiza kwamba kadri miaka inavyokwenda ni lazima rika la wazee lipishe lile la vijana.
“Kwenye uchaguzi mkuu ujao kama nitajaliwa na nikapata bahati ya kuchaguliwa tena, nitahakikisha kuwa naubadilisha uongozi wa Tanzania kwa kuufanya uongozi wa vijana zaidi," alisema.
Aliongeza: “Wale viongozi wa rika langu, lazima waanze kuwaachia nafasi vijana. Tunahitaji wakuu wa wilaya vijana zaidi, wakuu wa mikoa vijana zaidi, na hata mawaziri vijana zaidi. Ndivyo ilivyotokea kwetu sisi wakati tukiwa vijana.”
“Vijana ndiyo matumaini ya nchi hii katika miaka ijayo na kama hatukuwekeza kwa vijana wetu, basi ni dhahiri kuwa hatuwekezi ipasavyo katika miaka ijayo ya taifa letu,” alisisitiza.
Baraza la Mawaziri la sasa la Rais Kikwete lina jumla ya mawaziri na manaibu mawaziri 51.
Katika baraza hilo, mawaziri wenye umri kuanzia miaka 60 na kuendelea ni 14 wakati wenye umri kati ya miaka 50 hadi 59 ni 25. Mawaziri na manaibu mawaziri wenye umri chini ya miaka 50 ni 12.
Waziri mwenye umri mkubwa kuliko wote ana miaka 67 akifutiwa na mwenye umri wa miaka 66.
Akijibu maswali ya vijana hao kutoka nchi mbalimbali za Afrika zikiwamo Tanzania, Nigeria, Kenya, Afrika Kusini na Uganda, Rais Kikwete aliwaeleza vijana hao jinsi gani alivyojikuta anaingia katika siasa.
Akijibu swali kuhusu maendeleo ya karibuni katika siasa za Zanzibar, Rais Kikwete alisema ni jambo la kufurahisha kwamba vyama vya siasa Zanzibar vimeamua kuachana na siasa na mazoea ya zamani na kuanza ukurasa mpya.
“Nawatakia heri sana katika mwelekeo mpya na sahihi kabisa katika uendeshaji wa siasa. Ni mwelekeo ambao sote tumekuwa tunautafuta kwa muda mrefu,” alisema.
Katika siku za karibuni, Chama cha Wananchi (CUF) kimeamua kumtabua Rais Amani Abeid Karume kama Rais halali wa Zanzibar, hatua ambayo imefungua kila aina ya uwezekano wa kupatikana maelewano na mwafaka Tanzania Visiwani.
0 comments