Zitto Kabwe ataka serikali kutaifisha mitambo ya Dowans | |||||||
MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe, ambaye aliwahi kupendekeza kununuliwa kwa mitambo ya Kampuni ya Dowans Tanzania Limited, sasa anaitaka serikali iitaifishe, ili kuepukana na athari za mgawo wa umeme unaoitafuna nchi kwa sasa. Kabwe aliamsha maswali mengi dhidi yake wakati alipoelezea umuhimu wa serikali kuinunua mitambo ya Dowans hata kama ingekuwa ni kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004, akisema kuwa matatizo yanayolikabili taifa kutokana na mgawo huo ni makubwa. Wakati huo, Zitto aliomba kamati yake ikutanishwe na ile ya Nishati na Madini kuzungumzia suala hilo na kupata ufumbuzi wa tatizo la umeme baada ya Tanesco na Wizara ya Nishati na Madini kuelezea uwezekano wa nchi kutumbukia kwenye giza mwishoni mwa mwaka huu. Lakini Spika wa Bunge, Samuel Sitta alimjibu kuwa msimamo wa Kamati ya Nishati na Madini (wa kutaka mitambo hiyo isinunuliwe kwa kuwa imechoka na ununuzi utakiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma) ndio msimamo wa Bunge na kwamba, hawezi kuzikutanisha kamati hizo, huku akiitaka Tanesco na wizara husika kuwa makini katika suala hilo. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Zitto aliibuka na hoja mpya akiitaka serikali ifumbe macho na kuitaifisha mitambo hiyo ambayo ilizimwa Julai mwaka jana wakati Tanesco ilipoeleza kuwa, mkataba ambao kampuni hiyo iliurithi kutoka Richmond Development LLC, una matatizo. "Mitambo ya Dowans ni mizuri kwa kuwa ukiweka gesi na kuwasha tunapata megawati 125, hivyo ni bora itaifishwe ili tuondokane na giza na kushuka kwa uchumi wetu," alisema Kabwe, ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini. Alisema kuwa serikali haiwezi kununua mitambo hiyo kutokana na mazingira yalivyo, lakini akasema nchi haiwezi kuendelea na mgawo wa umeme wakati mitambo ya kuzalisha megawati zilizopungua ipo. Mitambo hiyo iko eneo la Ubungo jijini Dar es salaam na imezuiwa na serikali kutokana na Dowans kufungua kesi kwenye mahakama ya usuluhishi ya Paris, Ufaransa baada ya mkataba wake uliokuwa umalizike Novemba mwaka huu, kukatishwa mwaka mmoja kabla ya kumalizika. "Serikali ifunge macho na ndani ya wiki moja mitambo ichukuliwe halafu tutakutana na Dowans mahakamani, huu si wakati wa kupiga siasa bali ni wakati wa kukabiliana na tatizo," alisema. Kabwe alisema anashangaa kwa nini serikali haitilii maanani tatizo lililopo la mgawo wa umeme na kwamba, hata alipokutana na Kamati ya Nishati na Madini haikutoa majibu yanayoeleweka. Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Dowans ilikanusha madai kuwa jenereta zake (nne aina ya TM2500 zenye uwezo wa kuzalisha megawati 20 kila moja na moja aina ya LM6000PD yenye uwezo wa kuzalisha megawati 40) zimechoka na kueleza kuwa zina uwezo wa kufanya kazi kwa miaka 25 zaidi. Tanesco ilitangaza kufuta mpango huo wa kununua jenereta hizo zinazohamishika Februari 6 mwaka huu, baada ya kampeni zake kupitia kamati hizo mbili za Bunge kugonga mwamba. Akitangaza uamuzi wa Tanesco kufuta mpango huo, mkurugenzi wa shirika hilo, Dr Idris Rashid alisema asibebeshwe lawama iwapo nchi itaingia gizani kutokana na kutokuwa na ziada ya umeme. Wakati akitangaza uamuzi wa serikali kukatisha mkataba wa Dowans ulioligharimu taifa dola milioni 172.5 za Kimarekani mwezi Juni mwaka jana, Dk Rashid aliwaambia wahariri kuwa mkataba na Richmond ulikuwa batili kwa sababu ulikiuka Sheria namba 21 ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004 na kwamba, uamuzi wa kuuhamishia kwa Kampuni ya Dowans Holdings ya Afrika Kusini na baadaye Dowans Tanzania Limited haukufuata taratibu za kisheria kama ilivyotakiwa. Pendekezo la kutaifishwa kwa mitambo ya Dowans si la kwanza kwani lilishawahi kutolewa na mbunge wa Karatu, Dk Willibrod Slaa wakati mjadala wa ununuzi wa mitambo ya Dowans ulipopamba moto mapema mwaka huu. Dk Slaa alisema wakati huo kuwa badala ya kupiga porojo za jinsi ya kuitumia, serikali ilipaswa iitaifishe kwanza ili kuondokana na tatizo la umeme. Awali Tanesco ilisemekana kupanga mkakati wa kuishauri serikali kuongeza mkataba wa Dowans hadi mwaka 2012 kutokana na serikali kutokuwa na uwezo wa kununua mitambo yenye uwezo wa jumla ya megawati 250 katika kipindi cha miaka miwili. Kuhusu mitambo ya IPTL, Kabwe alisema ni muhimu serikali ikamaliza mazungumzo na kampuni hiyo, lakini wakati mazungumzo hayo yanaendelea IPTL wawashe mitambo ili megawati 100 zipatikane. "Hatuwezi tukawa na serikali ambayo haiwezi kuchukua maamuzi magumu wakati uchumi unateketea. Serikali itaifishe mitambo ya Dowans na mitambo ya IPTL iwashwe tuondokane na mgawo huu," alisema Kabwe, ambaye mkoa wake wa Kigoma uliahidiwa kupata umeme na serikali katika kikao cha bunge la bajeti, ifikapo mwezi Septemba mwaka huu. Alisema hivi sasa Tanesco inapata hasara ya Sh198milioni kila siku kutokana na mgawo huo, kitu ambacho kinalirudisha nyuma shirika hilo. "Viongozi wanapaswa kujali madhara yanayotokana na mgawo na si kubaki na hadithi za kutatua tatizo," alisema Kabwe. Akizungumzia madhara ya mgawo unaoendelea hivi sasa, Kabwe alisema katika sekta ya ujenzi gharama za uzalishaji zimepanda sana. "Kwa mfano kampuni ya Twiga Cement hutumia dola 10 za Kimarekani kuzalisha tani moja, lakini hivi sasa inatumia dola 40 za Kimarekani kuzalisha tani hiyo moja ikimaanisha gharama zimeongezeka mara nne," alisema. Alisema benki zimeathirika sana akitolea mfano CRDB ambayo alisema kuwa kwa sasa inatumia Sh400 milioni kwa mwezi wakati Barclays inatumia Sh 210 kinyume na wakati umeme unapokuwepo. Wakati huohuo, Kabwe alimmwagia sifa mkurugenzi anayeondoka Tanesco, Dk Idris Rashid akisema kuwa hajawahi kuona mkurugenzi bora kama yeye. Alisema Dk Rashid ni bora kwa kuwa aliikuta Tanesco ikiwa inapata hasara chini ya kampuni ya menejimenti ya NetGroup Solutions, lakini hivi sasa shirika hilo linapata faida. "Si mnakumbuka hasara iliyokuwa ikipatikana chini ya NetGroup, lakini hivi sasa tunapata faida chini ya uongozi wa Dk Rashid," alisema. |
You Are Here: Home - - Zitto Kabwe ataka serikali kutaifisha mitambo ya Dowans
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
0 comments