Ripoti ya Goldstone yaidhinishwa
Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa leo limeiidhinisha ripoti ya Gaza inayozituhumu Israel na wapiganaji wa kundi la Hamas kuhusika katika uhalifu wa kivita.
Katika kikao maalum, miongoni mwa wajumbe 47 wa baraza hilo la haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa, 25 walipiga kura kuidhinisha ripoti hiyo inayoikosoa Israel kwa kushindwa kutoa ushirikiano kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulioongozwa na Jaji wa Afrika Kusini, Richard Goldstone. Wajumbe wengine sita, ikiwemo Marekani na baadhi ya mataifa ya Umoja wa Ulaya walipiga kura kupinga kuiidhinisha ripoti hiyo na wajumbe 11 hawakupiga kura.
Israel na Palestina zakataa tuhuma
Zote Israel na Palestina zimekataa tuhuma hizo zilizoko kwenye ripoti ya Goldstone yenye kurasa 575, ambayo inaikosoa zaidi Israel kwa vitendo vyake katika vita vya kuanzia Desemba, mwaka uliopita hadi Januari, mwaka huu. Ripoti hiyo inatoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupeleka suala hilo katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita kama Waisrael au Wapalestina watashindwa kuchunguza tuhuma zinazowakabili wao wenyewe.
Marekani ilisema itapiga kura ya kupinga kuidhinishwa ripoti hiyo iliyoandaliwa na Wapalestina kwa msaada wa Misri, Nigeria, Pakistan na Tunisia kwa niaba ya nchi zisizofungamana, na mataifa ya Afrika, Kiislamu na Kiarabu. Msemaji wa Wziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, amesema kuwa Netanyahu amemuomba Brown kuifanya Uingereza ipige kura kuipinga ripoti hiyo na siyo kutopiga kura kama ilivyotarajiwa kufanya hivyo.
Akizungumza kabla ya kuipigia kura ripoti hiyo, Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Aharon Leshno Yaar, amesema ripoti hiyo ni ya upendeleo kwani inazingatia zaidi upande mmoja na imeshindwa kushawishi kufanyika majadiliano ya amani katika Mashariki ya Kati.
Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa lilikubaliana wakati wa mkutano wake wa mwisho wa kawaida kuahirisha majadiliano ya ripoti hiyo ya Gaza kufuatia shinikizo kutoka kwa Marekani ikijaribu kuyafufua mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati baina ya Israel na Wapalestina.
Israel na Hamas kufanya uchunguzi wao
Israel imesema tayari imeanzisha uchunguzi, huku msemaji wa serikali ya Hamas huko Gaza, Taher al-Nono, akisema Hamas itafanya uchunguzi juu ya ripoti hiyo, lakini haijasema chochote kuhusu tuhuma dhidi yake ambazo ziko katika ripoti hiyo. Taher alisema kuwa serikali ya Palestina imepokea uidhinishaji wa ripoti ya Goldstone na amezishukuru nchi marafiki ambazo zimepiga kura kuiidhinisha ripoti hiyo.
Ripoti hiyo inasema kuwa wakati wa mapigano hayo huko Gaza, Wapalestina 1,400 waliuawa, wengi wao wakiwa raia, huku Israel ikishuhudia vifo vya raia wake watatu na wanajeshi 10.
0 comments