Maafisa wa serikali ya Korea Kusini wanasema kilomita za mraba 1,000 zitaendelezwa, ambapo nusu ya mazao yatakayopatikana yatakuwa kwa ajili ya matumizi ya wananchi wa Korea na nusu kwa ajili ya wakulima wa eneo hilo.
Hata hivyo serikali ya Tanzania imesema bado swala hilo lipo katika hatua ya majadiliano.
Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Waziri wa kilimo, chakula na ushirika, Stephen Wasira, alisema ni kweli serikali imepokea maombi kutoka Korea Kusini lakini bado hakuna mkataba uliosainiwa.
"Walituarifu, walituambia wakati tukiwa pale. Siwezi kusema kwa sasa hivi, kama ni jema au si jema. Kwasababu kitu hii bado hata details zake hazijawa worked out", alisema Bw Wasira.
Bw Wasira aliongeza kuwa: "Lakini kwamba tunakaribisha investors kwenye agriculture, ni policy iko very clear, sasa unawakaribisha kwa conditions gani? Hizo ndiyo zinatakiwa ziwe worked out na mwekezaji pamoja na serikali ya Tanzania", alibainisha Bw Wasira.
Nchi kama China, Saudi Arabia, Korea Kusini na Kuwait zina upungufu wa ardhi yenye rutba na zimekuwa zikitafuta kuwekeza katika sekta ya kilimo Afrika.
Kampuni inayomilikiwa na serikali ijulikanayo kama Korea Rural Community Corporation imesema mkataba wa ushirikiano utasainiwa nchini Tanzania mwezi ujao.
Mkataba huo wa Tanzania na Korea Kusini umeafikiwa wiki mbili baada ya Waziri mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda, kuzuru Seoul ambako nchi zote mbili zimeahidi kuimarisha ushirikiano.
Korea Kusini pia ilisaini mkataba mwaka jana kuweza kukodisha eneo kubwa la Madagascar
Lakini hatma ya makubaliano ya Madagascar - ambayo yangetoa fursa kwa eneo kubwa kwenye kisiwa hicho kutumika kulima mazao kwa manufaa ya Korea Kusini, haijulikani.
Serikali ya Madagascar iling'olewa katika mapinduzi mapema mwaka huu na viongozi wapya wamesema watasitisha mpango huo, ambao ulielezwa kuwa sehemu ya machafuko ya kisiasa nchini humo.
0 comments