Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Wanafunzi vyuo vikuu na ushirikiano wa kinafiki

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Na Peter Zakhayo Daily News; Thursday,December 18, 2008 @20:00
Wanafunzi wa CBE wakati wa mahafali ya mwaka huu
Habari nyingine
  • Wanafunzi vyuo vikuu na ushirikiano wa kinafiki
  • Ziwa Tanganyika lina viumbe 500 adimu
  • Chunya na mfano wa yatima wanaofuja mali za urithi
  • Lugha nyepesi ni muhimu katika uandishi wa vitabu vya watoto
  • Elimu inahitajika kukomesha mila potofu
  • Mafanikio na changamoto za Taasisi ya Kilimo Arusha
  • Elimu sahihi inahitajika kwa watoa huduma kupunguza kifua kikuu
  • Barabara ya lami yaanza kuinua uchumi wa Lindi, Mtwara
  • Liwale imejaa fursa za kibiashara
  • Kukatika kwa umeme kulivyoathiri uchumi Mbeya
  • Jumamosi iliyopita, mdogo wangu wa kike alikuja nyumbani kwangu huku akibubujikwa machozi. Kwa bahati nzuri nilikuwapo nyumbani, hivyo nilimkaribisha na kuanza kumhoji ili kujua kilichomsibu.Baada ya dakika kumi hivi, alisema hivi, “Kaka, leo nimetoka kwa baba kumweleza masuala yangu ya chuo lakini jibu alilonipa sijui kama nitarejea nyumbani kwa siku za hivi karibuni.” Baada ya kujibiwa hivyo, nilijua nini kimetokea kwa kuwa naelewa kabisa misimamo ya mzee wetu pale yanapojitokeza mambo ya kipuuzi, hasa katika suala la elimu. Kwa maana hiyo basi, nilimwomba atulie ili anieleze vizuri kilichotokea ili nami niweze kumsaidia. Baada ya kutulia, kwa mara nyingine nilimtaka anieleze kilichotokea kinagaubaga naye aliniambia hivi, “Nilimpelekea fomu za kunirejesha chuoni ili azijaze naye amenijibu kwamba ‘nenda kampelekee baba yako mpumbavu kama wewe akakujazie, mimi sishughulikii masuala ya watoto wapumbavu wanaogoma vyuoni”. Kwa upande wangu, sikuona kama uamuzi wa mzee wetu ulikuwa wa busara, hasa ikizingatiwa kwamba tatizo hilo si lake peke yake, bali linawahusu wanafunzi wote, bila kujali kama yeye alishiriki au hakushiriki. Kutokana na ukweli huo, ingawa nilikuwa katika nafasi nzuri ya kumsaidia mdogo wangu, nililazimika kuwasiliana na mzee wetu ili kujua kama kuna lingine lililojitokeza zaidi ya hayo niliyoelezwa ili napate kujua mahali pa kuanzia, naye alinipa majibu yaleyale. Nilipojaribu kumshawishi, mzee alikataa katu na kuniambia nisirudie kumuuliza juu ya suala hilo la kipuuzi na kuongeza kwamba yeye hawezi kumshughulikia mwanafunzi aliyegoma. Alisema hawezi kufanya hivyo kwani yeye hakushiriki kumshawishi agome na wala hakuwahi kumwambia kuwa hana uwezo wa kulipia kiasi cha ada kinachopaswa kukamilishwa na mzazi au mlezi wa mwanafunzi. Baada ya kupata majibu hayo kutoka kwa baba sikuwa na uamuzi mwingine zaidi ya kumsaidia mdogo wangu aweze kurejea chuoni. Nilisoma masharti yaliyopo katika fomu hiyo na kuijaza kisha niliisaini na kumwambia airejeshe chuoni pamoja na fedha anayodaiwa pindi wakati wa kufanya hivyo utakapofika.Ukweli ni kwamba tukio hilo lilinipa fundisho kubwa ndio maana nikaamua kuandika makala haya. Hiyo inatokana na ukweli kwamba wapo wanafunzi wengi ambao wamekumbwa na tatizo kama hilo lakini mpaka sasa hawajapata ufumbuzi. Wapo wanafunzi walioanza kulia kama mdogo wangu alivyokuwa akilia tangu siku ya kwanza baada ya vyuo vikuu kufungwa na mpaka sasa wanalia. Kibaya zaidi ni kwamba hawana la kufanya, kwani hakuna wakuwasaidia mpaka sasa.Ninapowaangalia wanafunzi hawa namkumbuka mwalimu wangu wa masomo ya Sosholojia na Saikolojia, hayati Profesa Samuel Mshana, alipotufundisha kwamba uamuzi utokanao na makundi una madhara makubwa. Alitufundisha kwamba tunapoishi na watu tukiwa kama kundi moja, tunapaswa kuchukua tahadhari kubwa, kwani tunaweza kudhani sote tunafanana, kumbe katika hali halisi hatufanani hata kidogo.Hivyo ndivyo ilivyotokea kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, ambao wakati wakijiandaa kugoma walikuwa wakidhani kuwa ni wamoja, lakini baada ya kufukuzwa, wamebaini kuwa wanatofautiana kwa kiasi kikubwa. Hivi sasa kila mmoja anakufa kivyake. Ukweli ni kwamba baada ya kufukuzwa, kila mwanafunzi ameshika njia yake na kwa bahati mbaya zaidi wale wenzangu na mimi wanaotokea katika familia masikini mambo si shwari kwa upande wao hata kidogo. Hili ni kundi la wanafunzi ambalo kwa sasa hawana nauli ya kurejea makwao, wanahangaika mitaani wakisubiri chuo kifunguliwe ili warudi kwenye neema. Wanafunzi hao sasa wamejifunza kuwa wenzao waliowarubuni kugoma, walikuwa hawana nia njema nao, kwani mwisho wa siku wameachwa peke yao. Walitakiwa kujua ukweli kuhusu hilo, chukua mfano wa mdogo wangu. Ukweli ni kwamba kama ningekuwa naishi mbali, inawezekana kabisa kwamba ndoto ya safari yake ya kupata shahada ya kwanza ingeishia njiani, kutokana na mgomo huo.Anaeleza kwamba hakuwahi kushiriki katika mgomo huo au kuunga mkono hata siku moja, lakini naye amefukuzwa kwa sababu ya mkumbo. Niandikavyo makala haya, wapo wanafunzi wengi ambao wapo tayari kurejea vyuoni kwa masharti yaliyowekwa, lakini hawana pa kuanzia. Hao ni wanafunzi waliokuja Dar es Salaam kwa mara ya kwanza kujiunga na chuo, kwa nauli za mkopo vijijini kwao. Hao ni wanafunzi ambao kipato cha familia zao, kinatokana na kilimo cha msimu, hivyo baadhi yao wamekutwa na hicho kilichowakuta wakati wazazi wao hawana kitu mfukoni. Baadhi yao ambao wamefanikiwa kurejea makwao kwa nauli zilizotokana na posho kidogo wanayopewa chuoni, hivi sasa wanahaha kupata nauli ya kurejea chuoni. Wakati wao wapo katika hali hiyo, wenzao wanaotoka katika familia za kitajiri waishio Dar es Salaam, wanakwenda na kurudi chuoni kila siku wakitumia magari ya kifahari ya wazazi wao. Kwa wakati huu, wanafunzi hao wanapaswa kutambua kuwa si wamoja hata kidogo. Wanapaswa kutambua kuwa umoja walionao, ambao unasimamiwa na Serikali ya Wanafunzi unaishia katika mipaka ya chuo. Lakini, inapotokea mwanafunzi mmoja mmoja anapatwa na tatizo mtaani, umoja huo hauwasaidii kitu. Ingawa wanafunzi wengi wanalaani hatua iliyochukuliwa na serikali ya kuwasimamisha masomo mpaka mwezi ujao, kwangu mimi nadhani hilo ni fundisho kubwa kwao kwa siku za baadaye.Wanafunzi wengi sasa wametambua kuwa maisha si lelemama hata kidogo! Wametambua kuwa serikali ikisema haina fedha ya kugharamia asilimia 100 ya masomo yao, maana yake ni nini. Kwa sasa, wanafunzi hao wanajua kazi iliyopo katika kutafuta fedha. Kwa sasa wanatambua serikali ilivyo na majukumu makubwa ya kuwasomesha na kuwapatia fedha za kujikimu. Wanajua kwamba fedha za matumizi, ambazo baadhi yao wamekuwa wakidai kuwa ni kidogo, kwa sasa ni nyingi, kwani upatikanaji wake mwanafunzi akiwa mtaani ni mbinde.Kutokana na ukweli huo, ni wazi kwamba tabia za uamuzi utokanao na mkumbo zitapungua kwa kiasi kikubwa katika vyuo vikuu, hasa vilivyokumbwa na dhahama ya kufungwa. Hiyo inatokana na ukweli kwamba hivi sasa kila mwanafunzi, amebaini kuwa yupo peke yake. Wanafunzi wanapaswa kutambua kuwa huo ndio ukweli, hivyo pindi watakaporejea vyuoni uamuzi wao katika masuala ya kitaaluma, haupaswi kuathiriwa na uchochezi wa makundi fulani. Huo ni ushauri wa bure kwa wanafunzi wanaotokea kwenye familia masikini.Kama hawaamini, wanapaswa kujiuliza kwamba tangu walipoondolewa vyuoni, ni lini uongozi wa Serikali za Wanafunzi uliwatafutia wafadhili wa kuwapatia fedha za kujikimu katika kipindi hiki kigumu?
    Tags:

    0 comments

    Post a Comment