You Are Here: Home - - PROF. SHAYO WA CHAMA CHA DEMOKRASIA MAKINI AMEFARIKI
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
MWANASIASA na msomi aliyegombea urais wa Tanzania mwaka 2005, Profesa Leonard Shayo, amefariki dunia.
Profesa Shayo ambaye pia alikuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Hisabati katika wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, alifariki dunia jana saa 5.30 mchana katika hospitali ya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Profesa Shayo ambaye alikuwa mmoja wa wataalamu wachache wa Hisabati na Sayansi pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia Makini (MAKINI) ambacho kilimsimamisha kugombea urais mwaka huo.
Kwa mujibu wa mdogo wake, Bw. Habibu Mandari, Profesa alilazwa Ijumaa iliyopita baada ya kuzidiwa akiwa mjini hapa kikazi.
"Profesa aliugua ghafla na alipopelekwa hospitalini, waligundua kuwa na shinikizo la damu, kisukari na homa ya mapafu. Walifanikiwa kuishusha sukari lakini Mwenyezi Mungu aliamua kumchukua," alisema Bw. Habibu.
Alisema mwili wake umehifadhiwa kwenye mochari ya hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, kabla ya kusafirishwa kwenda nyumbani kwake Sinza, Dar es Salaam kwa ajili ya mipango ya mazishi.
Profesa Shayo katika kampeni za urais mwaka 2005 alikuwa kivutio kikubwa kwa wapiga kura, kwani tofauti na wagombea wengine, yeye aliendesha kampeni akitumia gari dogo na kipaza sauti bila wapambe.
Katika uchaguzi huo, mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete, alishinda kwa kuzoa kura zaidi ya milioni tisa kati ya 10,590,016 zilizopigwa, huku marehemu Shayo akiambulia kura 17,O33.
Wengine ni Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF aliyepata 1,317,220, Bw. Freeman Mbowe wa CHADEMA aliyepata kura 671,780, Bw. Augustino Mrema wa TLP kura 84,131, Mchungaji Christopher Mtikila wa DP (39,990), Bw. Edmund Mvungi wa NCCR-Mageuzi(56,423).
Wagombea wengine walikuwa ni mwanamke pekee Bibi Anna Senkoro wa PPT Maendeleo (18,741), Bw. Paul Kyara wa SAU (16,380) na Dkt. Emmanuel Makaidi wa NLD (21,525).
Marehemu Shayo alizaliwa katika kijiji cha Mamba Kotela na kukulia Rombo mkoani Kilimanjaro. Ameacha mjane na watoto wanne, watatu wakiwa ni wa kike.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikowahi kufanyakazi marehemu, Profesa Rwekaza Mukandala, alishitushwa na kifo hicho na kumwombea marehemu alazwe mahali pema peponi na kuahidi kutoa taarifa baadaye kupitia kwa wasaidizi wake kwani hakuwa amepata taarifa kuhusu kifo hicho.
0 comments