Watu wasiopungua kumi wameuwawa kufuatia shambulio kaskazini magharibi ya Pakistan
Wimbi la mashambulio yanayotajikana kufanywa na wafuasi wa itikadi kali wa Al-Qaida, linaendelea kuitikisa Pakistan.Hii leo watu wasiopungua sabaa wamejeruhiwa gari liliporipuliwa karibu na jengo la polisi mjini Islamabad.
Ripoti ya mwanzo iliyochapishwa na polisi ilizungumzia juu ya watu wanane waliouwawa kufuatia shambulio hilo.
„Tumepata bahati kwasababu watu takriban wote walipelekwa kulinda kikao cha bunge“ amesema hayo afisa mmoja wa polisi Ehsan Khan alipohojiwa na shirika la habari la Ufaransa AFP,akithibitisha hata hivyo watu sabaa wamejeruhiwa.
„Hakuna aliyeuwawa na tunaamini lilikua shambulio la mtu aliyeyatolea mhanga maisha yake.“Amethibitisha kwa upande wake mkuu wa polisi ya mjini Islamabad,Asghar Gardezi.
Shambulio hilo lililengwa ofisi kuu ya polisi,nje kidogo ya mji mkuu Islamabad-mahala kunakokutikana kituo cha mazoezi na nyumba za familia za maafisa wa kijeshi.Maelfu ya askari polisi wanaishi au wanafanya kazi katika eneo hilo.
Rais Asif Ali Zardari na waziri mkuu Yousuf Raza Gilani wametoa taarifa inayoshadidia msimamo wa Pakistan katika kuwapiga vita magaidi.
Kuna ripoti za hivi punde zinazozungumzia juu ya shambulio la pili lililotokea kaskazini magharibi ya pakistan na kugharimu maisha ya watu wasiopungua 10.
Pakistan inazongwa na wimbi la mashambulio yasiyokua na mfano,yanayosemekana kufanywa na wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislam-Al Qaida.Mashambulio hayo yamegharimu maisha ya zaidi ya watu 1300 katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja kote nchini Pakistan.
Jeshi la Pakistan kwa upande wake,limeanzisha opereshini kubwa tangu miezi miwili iliyopita katika maeneo ya kikabila ya kaskazini magharibi,yanayopakana na Afghanistan ambako wanamgambo wa Al Qaida na wataliban wanasemekana wamepiga kambi.
Madege ya kivita yamehujumu ngome na kituo cha mazoewi cha wanamgambo wanaoongozwa na Mollah Fazlullah,kaskazini magharibi ya Pakistan.
Wanamgambio zaidi ya 20 wameuwawa,miongoni mwao wakiwemo wakuu wao kadhaa.Lakini Mollah Fazlullah ametoroka-afisa mmoja wa kijeshi amesema.Mollah Fazlullah aliongoza madhambulio ya mwaka jana katika bonde la Swat.
Wataalam wanakubaliana, ukanda huo wa kikabila kaskazini magharibi ya Pakistan umegeuka uwanja mpya wa vita dhidi ya magaidi wanaofuata itikadi kali ya dini ya kiislam.Na jeshi la Marekani linalowaandamana wataliban nchini Afghanistan,linafyetua makombora takriban kila siku dhidi ya wanamgambo wa Al Qaida katika maeneo hayo,licha ya malalamiko ya serikali Islamabad.
Shambulio la leo la Islamabad limetokea katika wakati ambapo viongozi wa ngazi ya juu wa kijeshi na wa idara za upelelezi wamekua wakijibu masuala ya wabunge na serikali bungeni mjini Islamabad.
Itafaa kukumbusha hapa kwamba,shambulio kama hilo lilitokea pia september 20 iliyopita, kikao kama hicho kilipoitishwa mjini Islamabad.Wakati ule watu 60 walipoteza maisha yao lori liliporipuliwa ndani ya hoteli mashuhuri ya Marriot mjini humo.
0 comments