Serikali kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernald Membe, jana ililazimika kuwaomba radhi mabalozi wa nchi wahisani wanaowakilisha nchi zao hapa nchini kwa kitendo cha Jeshi la Polisi alichokiita ni "cha kukurupuka" kilichosababisha mauaji hayo.Kauli hiyo ambayo ni ya kwanza kutolewa na serikali tangu kutokea kwa mauaji hayo ilitolewa na Membe wakati wa mkutano wake na mabalozi hao uliofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana.
Membe alilazimika kutoa kauli hiyo baada ya kupata kibano toka kwa mabalozi hao waliotaka kujua sababu ya polisi kuwafyatulia risasi za moto na kutawanya maandamano ya amani ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Wakitoa kauli yao juu ya mauaji hayo, mabalozi hao walisema Afrika inahitaji amani na Tanzania imekuwa taifa la kupigiwa mfano, lakini mauaji ya Arusha yameipa sura nyingine na kuathiri sifa yake ya kuwa kisiwa cha utulivu na amani.
"Tumesikitishwa na mauaji hayo ya Arusha, Tanzania ambayo inasifika kama kisiwa cha amani duniani kote na kuendelea kuwa mshauri wa masuala ya amani barani Afrika, nayo imeingia doa. Hili limetusikitisha sana," alisema mwakilishi wa mabalozi hao.
Mabalozi hao pia walitaka kujua sababu za serikali kuwa kimya bila kutolea ufafanuzi kwa muda wote tangu mauaji hayo yalipotokea.
Akionekana kutikiswa na hoja za mabalozi hao, Membe alisema polisi wanapaswa kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili, lakini katika suala la Arusha, walikurupuka na kuamua kuwafyatulia risasi waandamanaji na hivyo kusababisha mauaji ya watu watatu na wengine kadhaa kujeruhiwa vibaya.
Membe aliwaahidi mabalozi hao kuwa serikali inatarajia kutoa kauli yake nzito hivi karibuni na kauli hiyo itatolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, huku akiwahakikishia kuwa Tanzania itaendelea kuwa kisiwa cha amani na utulivu.
"Tunawaomba radhi wote kwa tukio la mauaji lililotokea mjini Arusha, lakini tunawaahidi kwamba serikali itatoa tamko lake hivi karibuni ili kuhakikisha tukio la aina hiyo halijitokezi tena nchini," alisema Membe.
Waziri Membe alitumia nafasi hiyo kuliasa Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa uadilifu na kuacha kufanya maamuzi ya kukurupuka ambayo yanaweza kuleta maafa kama ilivyotokea Arusha.
"Serikali imechukua mawazo yenu kama changamoto kwetu, hivyo tunaahidi kwamba ufafanuzi wa mauaji unatarajiwa kutolewa siku chache zijazo," alisema Waziri Membe.
Wakati serikali ikiomba radhi kwa kufanya mauaji hayo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) leo kinafanya mazishi ya "kishujaa" kuwaaga watu wawili waliofariki kwa kupigwa risasi katika maandamano hayo ya Januari 5 mwaka huu.
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, aliyeambatana na mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mjini hapa jana alisema shughuli za kuwaaga marehemu hao zitafanyika katika viwanja vya NMC kama ilivyokuwa imetangazwa awali.
Taratibu za utoaji heshima za mwisho na ibada za kuwaaga marehemu hao ambao ni Ismai Omary (40) na Denis Michael Shirima (30) zitaanza saa 4 asubuhi.
Pia kutaendeshwa mchango wa hadhara kwa ajili ya kukusanya fedha za kusaidia familia zilizoachwa na mashujaa hao.
Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai na kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni alisema majeneza ya marehemu hao yatafunikwa na bendera za CHADEMA.
Alisema viongozi wa chama hicho wilaya na mkoa walikutana na uongozi wa polisi mkoani hapa na wamekubaliana kuwa shughuli hiyo ifanyike kwenye viwanja hivyo ambavyo awali vyombo vya habari (si Tanzania Daima) viliripoti kuwa shughuli hiyo imekatazwa kufanyika kwenye viwanja hivyo.
Aidha, taarifa nyingine za uhakika zilisema viongozi wa Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha mapema jana walikwenda nyumbani kwa muasisi wa CHADEMA, Mzee Edwin Mtei, na kumsihi awashawishi viongozi wa chama hicho wasitishe mpango wao wa kufanya shughuli kubwa ya mazishi katika viwanja vya NMC na badala yake waache mazishi hayo yafanywe nyumbani kwa marehemu hao.
"Leo walikwenda kwa Mzee Mtei na kumuomba asaidie kuwazuia CHADEMA wasiiage miili NMC, wakidai eti wanaogopa kutatokea vurugu....," alisema mtoa taarifa wetu kwa sharti la kutotajwa jina lake.
Hata hivyo, Mbowe alipoulizwa kama polisi wamezuia kufanyika kwa maandamano hayo alisema hawajazuia na shughuli hiyo ya kuaga miili ya marehemu itafanyika kwenye viwanja vya NMC kama ilivyopangwa.
Alisema kwenye viwanja hivyo kutafanyika ibada kulingana na imani za marehemu hao pamoja na wananchi kutoa heshima zao za mwisho na CHADEMA watatoa tamko lao juu ya tukio zima lililopelekea msiba huo.
Alisema kutakuwa na msafara wa magari utakaoanzia chumba cha kuhifadhi maiti cha Mount Meru kuanzia saa mbili asubuhi; msafara ambao utapita barabara za Goliondoi kuelekea Sokoine mpaka viwanja vya NMC.
Mbowe alisema baada ya kumalizika kwa shughuli za ibada na kutoa heshima za mwisho, miili ya marehemu hao itaondolewa viwanjani hapo kwa kupitia barabara za Sokoine kuelekea Goliondoi kupitia AICC mpaka Sanawari ambako wataingia kwenye barabara kuu ya Moshi Arusha na kuelekea kijiji cha Laki Tatu kata ya USA River kutakakofanyikia mazishi ya Ismail.
Alisema mwili wa Shirima utapelekwa Rombo Mkuu mkoani Kilimanjaro ambako utahifadhiwa na kuzikwa siku inayofuata (Alhamisi) ili kutoa fursa kwa viongozi na wananchi kuweza kushiriki maziko hayo ambayo aliyaita ni ya kishujaa.
Kwa upande wake, Lema alisema mwili wa raia wa Kenya, Paul Njuguna Kayele, ambaye polisi walidai anaitwa George Waitara bado hawajajua utazikwa lini ila kwa sasa chama hicho kinaendelea kufanya mawasiliano na balozi mdogo wa Kenya pamoja na ndugu wa marehemu.
Mazishi hayo yatahudhuriwa na viongozi waandamizi wa CHADEMA akiwemo katibu mkuu wake Dk. Wilbrod Slaa huku akisema tayari wabunge 18 wameshawasili jijini hapa pamoja na madiwani wote wa chama hicho toka mikoa ya Kilimanjaro, Manyara na Arusha kushiriki msiba huo mzito.
CHADEMA imegharamia mazishi hayo kwa kutoa ubani wa sh 500,000 kwa kila familia ya marehemu mbali na gharama nyingine na shughuli hizo zinaratibiwa na kamati ndogo ya mazishi ya chama hicho inayoongozwa Magoma Derrick Jr.
Januari 5 mwaka huu CHADEMA ilifanya maandamano ya amani kumpinga meya na naibu meya wa jiji la Arusha kwa hoja kuwa hawakuchaguliwa kihalali kwani kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu, kanuni na sheria wakati wa kuendeshwa kwa uchaguzi huo.
Maandamano hayo ya amani yaliyokuwa yakiongozwa na Mbowe yalipofika eneo la Tangi la Maji, polisi waliyaingilia na kuanza kuwapiga wananchi kwa virungu, mateke huku wakitumia mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatawanya.
Aidha, polisi walienda kwenye eneo la NMC ulipokuwa ukifanyika mkutano wa hadhara na kuwatawanya wananchi kwa kutumia mabomu ya machozi, risasi za moto na maji ya kuwasha ambapo wananchi kadhaa walijeruhiwa.
Pia majira ya saa kumi jioni mara baada ya kumalizika mkutano polisi walitumia mabomu ya machozi, risasi za moto na maji ya kuwasha kuwatawanya wananchi ambapo pia walikuwa wakizunguka maeneo ya katikati ya mji wakirusha risasi za moto na mabomu ya machozi hali iliyosababisha wananchi wengi kujeruhiwa huku wengine mali zao zikiharibika vibaya.
Ingawa polisi ilisema waliofariki ni watu watatu, baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa walifariki watu 10.
Sent from my iPhone
0 comments