Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - NSSF kujenga nyumba 792 jijini Mwanza

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MFUKO wa Taifa wa Hifadhi za Jamii (NSSF) unatarajia kujenga nyumba 792 mkoani hapa kuanzia Machi mwaka huu katika eneo la Kiseke na Bugarika jijini hapa.


Ujenzi wa nyumba hizo ni sehemu ya miradi minne inayotarajiwa kuwekezwa mkoani hapa na mfuko huo yakiwemo majengo ya biashara na kwa ajili ya kuwauzia wanachama wake na wananchi kwa ujumla.


Mkurugenzi wa Uwekezaji wa NSSF, Yakobo Kidula aliliambia gazeti hili juzi kuwa kwa kuanzia, watajenga nyumba 287 katika eneo la Bugarika.


Hata hivyo, aliiomba halmashauri ya jiji la Mwanza kuwapatia viwanja vya umma kwa ajili ya ujenzi wa zahanati, shule na maeneo ya michezo katika maeneo waliyowapatia viwanja ili wananchi waweze kupata huduma za jamii kwenye maeneo hayo.


Pia aliiomba halmashauri ya jiji kutengeneza miundombinu ya maeneo hayo ikiwemo ya barabara ili nyumba hizo ziweze kuuzwa kwa gharama nafuu kwa wananchi.


“Iwapo miundombinu ya uhakika haitawezeshwa na halmashauri, wananchi watabebeshwa mzigo mkubwa usio wao wakati ni jukumu la serikali na halmashauri kuhakikisha miundombinu ya kudumu inakuwepo,” alisema Kidula.


Aliitaja miradi mingine itakayowekezwa katika Jiji la Mwanza kuwa ni pamoja na ujenzi wa hoteli ya kitalii katika eneo la Kapripointi na ujenzi wa huduma za kibiashara ‘shopping mall’ katika eneo la Ghana Kota.


Kwa upande wake Waziri wa Kazi, Gaudensia Kabaka baada ya kutembelea miradi hiyo alisema
barabara katika jiji hili ni kikwazo cha maendeleo hivyo ni lazima suala hilo liangaliwe kwa umakini.


Alisema Mwanza imekuwa ikibadilishwa na Mifuko ya hifadhi kutokana na kuwa na jukumu la
kuwekeza fedha za wanachama ili kuboresha maisha yao.


“Vikwazo visivyo na sababu havitakiwi, eneo likikaa kwa muda mrefu bila kuendelezwa halina faida na iwapo pakiendelezwa thamani yake inaongezeka, hivyo serikali kupitia halmashauri haina budi kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wa ndani hususani Mifuko ya hifadhi za jamii ili kuongeza thamani ya ardhi,”alisema Waziri Kabaka.


Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe akizungumzia miundombinu ya barabara katika eneo la Bugarika alisema barabara zipo tayari na kuwataka NSSF waanze ujenzi bila hofu.

0 comments

Post a Comment