Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Bei ya Umeme juu

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
SERIKALI imehadharishwa kuwa makini na kusudio la ongezeko la bei ya umeme lililotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), ili kuokoa wananchi wa
chini dhidi ya ugumu wa maisha.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, wadau mbalimbali walisema ingawa
ongezeko hilo linaelezwa kuwa halitahusu wananchi wa hali ya chini, lakini kiuhalisia lazima wananchi wataathirika.
Chama cha NCCR-Mageuzi kupitia kwa Mkuu wa Idara ya Kampeni na Uchaguzi, Faustine
Sungura, kilisema jana kuwa hakikubaliani na kusudio hilo la kuongeza bei ya umeme, kwa vile
litaongeza gharama za uzalishaji wa bidhaa viwandani na kusababisha mfumuko wa bei.
“Ongezeko hili si tu kwamba litamfanya raia wa kawaida kuendelea kuishi katika mazingira
magumu, lakini pia litasababisha uharibifu wa mazingira kwa watu wa kawaida kuendelea kutumia nishati ya mkaa na kuni.
Alisema mbali ya kusababisha ugumu wa maisha, ongezeko hilo litafanya bidhaa za Tanzania
kwenye soko la Afrika Mashariki zikose wanunuzi kutokana na gharama kubwa za uzalishaji
wakati Kenya imeshusha gharama za umeme kwa asilimia tano.
Madai mengine ya NCCR Mageuzi ni kwamba ongezeko hilo haliendani na nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma na hivyo litawaathiri na kwamba linatokana na Tanesco kuogopa kudai malimbikizo ya madeni yake yanayokaribia Sh bilioni 300 kutoka kwa wadeni wake. Chama hicho kimesema kitapinga ongezeko hilo kwenye Tume ya Ushindani.
Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndugulile (CCM), alisema ingawa hatua hiyo haikwepeki kutokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji umeme, lakini si suluhisho la kudumu la matatizo ya ukosefu wa fedha yanayoikabili Tanesco.
Alisema ukubwa wa gharama za uzalishaji umeme, unafanya Tanesco ishindwe kuhimili gharama za uzalishaji umeme peke yake na hivyo kuhitaji wadau wengine wakiwamo wananchi kuchangia, lakini akasema hatua hiyo inatokana na kutegemea zaidi umeme wa dharura ambao ni aghali.
“Ni lazima sasa tuachane na mfumo huu wa kutegemea umeme wa mafuta, ambao ni gharama sana. Ni vizuri sasa tukatekeleza ahadi zetu za kuwa na miradi mikubwa ya umeme kama ule unaotokana na gesi, makaa ya mawe na njia nyingine mbadala.”
Alisema ingawa inadaiwa kuwa ongezeko hilo halitawahusu wananchi wanaotumia chini ya uniti 50 kwa mwezi, lakini bado wananchi hao wa chini watakutana na ongezeko la bei kwenye bidhaa zitakazozalishwa, ambazo zitapanda bei ili kufidia ukubwa wa bei ya umeme.
Mchumi na Mbunge wa zamani wa Tabora Mjini, Siraju Kaboyonga, alisema ongezeko hilo la bei ya umeme ingawa halitawaathiri wananchi wa chini moja kwa moja, lakini bado litawaathiri kupitia upande mwingine.
Alisema hata kama mwananchi wa kawaida hatakumbana na bei kubwa ya umeme kwenye Luku atakayonunua, lakini atakumbana nayo kwenye bidhaa kwa vile wenye viwanda watapandisha bei ili kufidia nakisi ya gharama za umeme.
Alisema hata hivyo, suala hilo halikwepeki, kwa sasa kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji ambao unaifanya Tanesco kuwa na mzigo mkubwa wa uzalishaji umeme.
“Kwanza niwapongeze Ewura, kwani wamefanya kazi nzuri sana.Tanesco wao walitaka
ongezeko la karibu asilimia 155, ombi ambalo lilikuwa kubwa sana. Kutokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji umeme, suala la bei ya umeme kupanda lilikuwa ni la lazima na ndiyo maana nasema Ewura wamefanya kazi nzuri kwa kuruhusu ongezeko la asilimia 40.29 ambalo si kubwa sana.
“Nasema si kubwa sana, kwani hivi sasa mfumuko wa bei umefikia asilimia 20. Ukiangalia ongezeko hilo la asilimia 40 ni sawa na kusema kilichoongezeka baada ya ile asilimia 20 ya mfumuko wa bei ni asilimia 20 nyingine ambayo hii nayo haikwepeki, kwani Tanesco
wanatumia fedha nyingi sana kuzilipa hizi kampuni binafsi zinazozalisha umeme tunaouita wa
dharura.
“Hili suala la kupanda kwa mfumuko wa bei si la Tanesco, ni la Wizara ya Fedha (Hazina) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wao Tanesco wanaathirika kama wanavyoathirika watu wengine,
hivyo ni lazima watafute namna ya kukabiliana na ukubwa wa gharama za uzalishaji.
“Ikumbukwe kwamba gharama za umeme huu aghali unaozalishwa na Songas, Simbion Power, IPTL na kampuni nyingine zote zinatupwa kwa Tanesco. “Labda ili kuokoa ugumu wa
maisha kwa wananchi, Serikali sasa ianze kutoa ruzuku kwa Tanesco ili kufidia ukubwa wa gharama za uendeshaji, jambo ambalo naona pia lina ugumu, kwani Serikali inaonekana haina uwezo huo na ndiyo maana pia inadaiwa kiasi kikubwa cha fedha na Tanesco.”
Alisema Tanesco pia inakabiliwa na changamoto ya kuongeza wigo wa wateja, ili kutoa unafuu kwa wateja waliopo, kwani pamoja na kupanda kwa gharama za uendeshaji, bado wigo wa wateja umeendelea kuwa mdogo na hivyo kuwabebesha mzigo mkubwa.
“Tanesco ipeleke umeme vijijini, ili kuongeza idadi ya wateja. Hivi sasa Watanzania tupo kama milioni 40, ukiondoa watoto, wazee na watu kama hao, unabakiwa na kama watu milioni 20.
Katika idadi hii ya Watanzania, wateja wa Tanesco ni kama asilimia 40 tu ya watu hao, idadi hii ni ndogo sana kubebeshwa gharama za umeme huu aghali,“ alisema Kaboyonga.
Nako Mwanza, Grace Chilongola, anaripoti kwamba wakazi, wameeleza kutoridhishwa kwao na
ongezeko hilo, kwa madai kuwa ni matokeo ya Tanesco kushindwa kukusanya madeni yake na hivyo kuwatwisha mzigo wananchi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao walihoji namna vyanzo mbadala vinavyoisaidia nchi katika kuepusha wananchi wake na mzigo mkubwa wa gharama za umeme.
Mbena John alihoji kwa nini gesi ya Songosongo ambayo inachimbwa nchini isitumike kuwapunguzia wananchi makali ya maisha kwa kushusha bei na badala yake mafuta yamekuwa yakitumika na kuwafanya wananchi kuzidi kudidimia kutokana na ugumu wa maisha.
Alisema kupanda kwa gharama za umeme kutasababisha mfumuko wa bei kuongezeka zaidi, hasa kwa bidhaa za viwandani na kuwafanya wananchi kuwa katika mazingira magumu zaidi.
Alisema wakati umefika kwa Serikali kuangalia vyanzo mbadala vya gesi na makaa ya mawe kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wananchi wake.
Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje, alisema kupanda kwa gharama za umeme kwa asilimia 40 ni dhahiri kuwa gharama za maisha kwa wananchi wa kawaida zitakuwa juu.
Juzi Ewura ilitangaza kuidhinisha kupanda kwa bei ya umeme kwa asilimia 40.29 kuanzia kesho, ambapo ongezeko hilo halitagusa wateja wa hali ya chini wanaotumia chini ya uniti 50.

0 comments

Post a Comment