Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Posho za wabunge zawa kaa la moto

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
VIONGOZI WA DINI,WASOMI,WANANCHI WAJA JUU, KAULI TATA ZA SPIKA MAKINDA, KATIBU WA BUNGE ZACHEFUA WENGI
Waandishi Wetu
NYONGEZA ya posho za vikao iliyothibitishwa juzi na Spika Anne Makinda kwamba imeanza kutolewa Bunge lililopita, imeleta balaa, baada ya wabunge, wasomi, wanaharakati na viongozi wa dini, kuipinga na kumtaka Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah kuwajibika kwa kile walichoeleza kuwa ameudanganya umma.Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti kuhusu posho hizo ambazo Serikali katika Mpango wake wa Maendeleo wa Miaka Mitano uliopitishwa katika Bunge la Bajeti, ilitangaza kuzipunguza, watu hao wa kada tofauti walishangaa uamuzi huo mpya wa Bunge kuziongeza.


Mbunge wa Jimbo la Ubungo (Chadema), John Mnyika alisema ongezeko hilo linatakiwa kusitishwa kwa kuwa mchakato wake umefanyika kinyume na taratibu na kwamba halina uhalali wala halijazingatia uhalisia wa maisha ya wananchi na uchumi wa nchi.


Mnyika alifafanua kwamba kauli ya Spika Makinda kwamba nyongeza hiyo inatokana na kupanda kwa gharama za maisha mkoani Dodoma haina ukweli, wala mantiki na ina mwelekeo wa upendeleo.


Akamtaka Rais Jakaya Kikwete kutolea kauli kuhusu jambo hilo.


Alisema utetezi wa Spika Makinda kuhalalisha kupandishwa kwa posho hizo, hauna maana na kwamba kama sababu ingekuwa kupanda kwa gharama ya maisha, ingepandishwa posho ya kujikimu (subsistence allowance) ambayo imebaki pale pale Sh 80,000.


Mnyika alisema alikuwepo kwenye mkutano wa Novemba 8, 2011 na hakuna uamuzi wowote ambao ulifikiwa wa kuiomba Serikali ipandishe posho za vikao na yenyewe.


Alisema kilichotokea siku hiyo ni kwamba katika kuchangia maelezo ya Serikali na ya Bunge kuhusu masuala mbalimbali yaliyojiri baada ya mkutano wa nne wa Bunge na mpangilio wa Mkutano wa Tano wa Bunge, wabunge walipewa fursa ya kujadili taarifa hizo.


Alisema wabunge hawajawahi kupatiwa nakala ya muhtasari au kumbukumbu za vikao vya Kamati ya Uongozi au vya Tume ya Bunge ambavyo vimekaa na kupitisha nyongeza ya posho ya vikao kutoka Sh70,000 mpaka Sh200,000, kama Spika alivyonukuliwa na vyombo vya habari.




Viongozi wa dini wanena


Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilani alisema ongezeko hilo la posho limekuja ghafla na kwamba kiwango hicho ni kikubwa na hakiendani na hali halisi ya uchumi wa nchi.


“Watanzania wengi wanalalamika maisha magumu sasa wabunge wanapoongezewa posho kwa kiwango kinachofikia Sh 200,000 watambue kwamba kuna wananchi wanaohitaji msaada, hizo nyongeza za posho zingeweza kuwasaidia kwa namna moja ama nyingine ambapo ongezeko la posho hizo zingeweza kuwasaidia” alisema Kilaini.


Kwa upande wake, Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaji Alhad Mussa Salumu alisema kwamba haoni tatizo posho za wabunge kuongezeka na kwamba kutokana na majukumu yao mazito ya kuwahudumia wananchi.


“Ni jambo jema, lakini wabunge watambue kwamba wananchi waliowachagua wana matatizo mengi ya kiuchumi sasa wanaposikia wabunge wameongezewa posho lazima nao watahoji, lakini kinachotakiwa ni kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kutatua matatizo ya wananchi wao,”alisema Alhad Salumu.




Mbatia, Kafulila waja juu


Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema mfumo mzima wa utoaji wa posho nchini ni wa kifisadi.
Mbatia alisema kuwa kuna haja ya kuutizama upya mfumo huo ambao umeacha pengo kubwa kati ya mwenye nacho na asiyekua nacho.
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, alisema suala la kupishana kauli kwa viongozi wawili wa taasisi moja, ni udhaifu mkubwa kwa taasisi hiyo.


“Suala la posho inatakiwa litazamwe upya katika mihimili yote ya dola, panapokuwa hakuna kanuni ya kuweka uwiano miongoni mwa mihimili hii, ”alisema Kafulila na kuongeza.
“Inatakiwa itazamwe upya, hili suala la posho lipatiwe ufumbuzi kabisa, ukiangalia huko serikalini kuna mashirika ya umma ambayo wanalipa posho za Sh400,000 mpaka 500,000, mishahara wanalipa Sh10milioni mpaka 15 milioni,” alisema Kafulila:


Wasomi
Profesa Ruth Meena alisema ni jambo la kusikitisha kuwa viongozi wa Bunge wanapishana kauli juu ya suala hilo la posho.
“Inasikitisha sana hawa wawakilishi wetu kujiongezea posho wakisema kuwa gharama za maisha zimepanda, kwenye hali kama hii ya sasa hakuna njia yeyote utakayoweza kutumia kuhalalisha ongezeka kama hili,” alisema Profesa Meena.


Dk Biassio Ndenjenje kutoka Chuo cha Usafirishaji Tanzania (NIT) alisema, ingekuwa vyema fedha hizo za kuwalipa wabunge posho, zikatumika kwa ajili ya kutatua matatizo ya sekta ya elimu na afya kuliko kuwaongezea wabunge posho.


Maandamano ya kupinga posho
Taasisi ya Kimataifa ya JDPA Foundation (JPF), inayoendesha Kituo cha Haki za Binadamu, Demokrasia na Utawala Bora Afrika, imetishia kuitisha maandamano yasiyokuwa na kikomo nchi nzima kuanzia Disemba 15 kupinga posho hizo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Praygod Mmassy alisema wamechukua hatua hiyo kutokana na wabunge kujiongezea posho huku wananchi wakiwa wanaishi maisha magumu.


Wananchi waponda posho


Baadhi ya wananchi nao walikuwa na maoni tofauti ambapo Prisca John wa jijini Dar es Salaam alisema kuongezwa kwa posho za wabunge kunadhihirisha wazi jinsi ufisadi ulivyokithiri kwa baadhi ya watendaji ambao alidai wanajitizama wenyewe kuliko kutazama wananchi waliowachagua.


Naibu Waziri Theu azitetea


Akizungumza na waandishi wa habari jana katika maonesho ya miaka ya 50 ya Uhuru yanayofanyika Viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Fedha, Gregory Theu alisema Hazina wanaheshimu kauli ya spika na si vinginevyo.
“Spika kama kasema zimeanza kulipwa sisi hatuna cha kusema. Iwapo wameanza kulipwa ama bado sisi sio jukumu letu hilo na tutaheshimu kauli hiyo na si vinginevyo,” alisema Theu.


Utata wa kauli


Juzi sakata hilo la posho lilichukua sura mpya, baada ya Spika Makinda, kutangaza kuwa wabunge wameshaanza kulipwa viwango vipya vya Sh200,000 badala ya Sh 70,000 za awali, akipingana na Katibu wake, Dk Kashililah, aliyekanusha wabunge kuanza kulipwa.


Wakati Dk Kashililah akitoa taarifa rasmi kukanusha taarifa za wabunge kuongezewa posho hizo, Makinda juzi aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa tayari posho hizo zimeanza kulipwa.


"Mbunge huyu alikuwa anapata Sh 70,000 kwa hiyo tumemwongezea 130,000 na hupati unless (isipokuwa) umefanya kazi ya Bunge na amesaini asubuhi na jioni. Hujafanya hivyo hupati hizo hela,"alisema Makinda.


Wiki iliyopita gazeti hili liliripoti taarifa za ndani kwamba posho za wabunge zimepanda kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000 hivyo kufanya bajeti ya posho hizo kwa mwaka kufikia Sh28 bilioni.


Kutokana na ongezeko hilo, taarifa hizo zilisema kila mbunge atakuwa akilipwa Sh80,000 kama posho ya kujikimu (per diem) anapokuwa nje ya jimbo lake, posho ya vikao (sitting allowance) Sh200,000 na mafuta ya gari Sh50,000 kila siku, sawa na Sh330,000 kwa siku huku mshahara jumla kabla ya makato ni Sh2.3 milioni na ukikatwa unabaki Sh 1.7milioni.


Wakati taarifa hiyo inaripotiwa, Dk Kashililah alisema hawezi kuzungumzia jambo hilo kwa sababu yeye si msemaji wa Bunge na akashauri atafutwe Spika wa bunge. 

Lakini, baada ya mjadala wa takriban juma moja wa wanaharakati, wabunge na wasomi kupinga nyongeza hiyo ya posho, Dk Kashililah aliibuka na kukiri kuwa wabunge wanataka waongezewe posho za vikao, lakini mapendekezo hayo, hayajaanza kutekelezwa.


Kwa mujibu wa Katibu huyo Bunge, mapendekezo ya kutaka posho za wabunge zipande, yaliibuka katika mkutano wa wabunge mjini Dodoma Novemba 8 mwaka huu, lakini hadi sasa hayajaanza kutekelezwa.


"Suala la mabadiliko ya posho za vikao vya Bunge lilijitokeza katika Mkutano wa wabunge, Novemba 8, 2011 walipoiomba Serikali iangalie upya suala hilo kwa lengo la kuboresha,” alisema Dk Kashililah katika taarifa hiyo na kuongeza:


”Hadi tunapotoa tangazo hili (jana), Serikali haijatoa taarifa iwapo posho hiyo imeongezeka kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000."



0 comments

Post a Comment