IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
KAIMU Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Ltd (MCL), Theophil Makunga, leo atafikishwa mahakamani kama mshtakiwa wa tatu katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya FreeMedia, Absolom Kibanda.
Makunga ameunganishwa katika shtaka hilo kama mchapaji wa gazeti la Tanzania Daima Jumatano, linalodaiwa kuandika habari ya uchochezi dhidi ya Serikali Novemba 30 mwaka huu.
Makala inayodaiwa kuwa ni ya uchochezi ilibeba kichwa cha habari ‘Waraka maalum kwa askari wote.’ Polisi inadai kuwa waraka huo umelenga kuwachochea polisi kuisaliti Serikali.
Makunga aliliambia gazeti hili tayari alihojiwa na polisi jana kwa saa tatu, kuanzia saa 4:15 asubuhi na baada ya hapo alielezwa leo atafikishwa mahakamani kujibu shitaka lake.
“Wameniambia wananipeleka mahakamani kama Kaimu Mkurugenzi wa Mwananchi na hati ya mashtaka inasema ni kwa uchochezi wa askari wasitii amri halali ya Jamhuri ya Muungano,”alisema Makunga.
Wakati Makunga akihojiwa na polisi jana, Kibanda alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu shtaka hilo.
Mbali ya Kibanda, kesi hiyo namba 289/2011, pia inamkabili Mwandishi wa Safu ya Kalamu ya Mwigamba inayochapishwa kila Jumatano na gazeti la Tanzania Daima, Samson Mwigamba (36) ambaye jana hakuweza kufika mahakamani.
Ilielezwa mahakamani hapo jana kwamba, Mwigamba hakuweza kufika kwasababu alikuwa mkoani Arusha kwenye kesi nyingine iliyokuwa ikitajwa jana.
Wakili wa Serikali, Elizabeth Kaganda alidai mahakamani hapo kuwa Novemba 30 mwaka huu, katika gazeti la Tanzania Daima toleo namba 2553, Kibanda na Mwigamba, waliandika makala inayowashawishi askari na maofisa wa majeshi hapa nchini kuacha kutii Serikali iliyopo madarakani.
Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo kinyume na Sheria ya Kanuni ya Adhabu Kifungu namba 46 (b), 55 (10) (a) na Kifungu cha 35 cha sheria hiyo.
Hata hivyo, Kibanda alikana mashitaka hayo na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Katika kesi hiyo, Kibanda anatetewa na mawakili Isaya Mambo, Juvenalis Ngowi, Nyaronyo Kicheere, John Mhozya na Deograthias Ringia.Kiongozi wa mawakili hao Ringia, aliiomba mahakama kumpa dhamana mteja wao kwa sababu mashitaka yanayomkabili kisheria yanadhaminika.
Hakimu Mkazi Stuart Sanga alitoa masharti ya dhamana ambayo ni pamoja na kuwa na hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh 5 Milioni, wadhamini wawili wa kuaminika watakaosaini dhamana ya maneno ya Sh5 milioni kila mmoja, kuwasilisha mahakamani hati yake ya kusafiria na kuripoti polisi kila mwezi.
Mshtakiwa huyo alitimiza masharti hayo kwa kutoa hati na kudhaminiwa na Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwanahalisi, Saed Kubenea na mfanyakazi wa Benki ya Posta, Ahobokile Mwajoka.Kabla ya kufikishwa mahakamani hapo, Kibanda alishikiliwa na kuhojiwa polisi kwa saa kadhaa katika Makao Makuu Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam.
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Mkurugenzi wa Mwananchi kizimbani leo
0 comments