Pages

Thursday, April 14, 2011

Wenje achafua hali ya hewa Bungeni Dodoma, Werema hoi


 Ezekia Wenje

UKUMBI wa Bunge jana ulitawaliwa na maneno na misemo mikali kiasi cha kumfanya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema kumshauri Spika wa Bunge, Anne Makinda aamuru askari wa Bunge wamkamate na kumtoa nje ya ukumbi, Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekia Wenje.

Hatua hiyo ilitokana na kitendo cha Wenje kudai kuwa Kamati ya Bunge ya Uongozi, ilifanya uamuzi kinyume cha Kanuni za Bunge na kukiita kitendo hicho kwamba ni dark market (mambo yasiyofuata utaratibu).Kauli hiyo ilitokana na hatua ya Spika Makinda kuwasilisha majina matatu ya wagombea wanaotakiwa kuchaguliwa kuwa wenyeviti wa Bunge, huku kanuni zikitaka kuwasilishwa kwa majina sita ili yapigiwe kura.

Majina yaliyowasilishwa yalikuwa ni ya George Simbachawene (Kibakwe), Jenista Mhagama (Peramiho) na Sylivester Mabumba (Dole) kwamba ndiyo wanaotakiwa kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo.Baada ya kutaja majina hayo, Wenje aliomba mwongozo wa Spika kwa kutumia kanuni ya kumi na moja akisema uamuzi huo unaonyesha kuwa Kamati ya Uongozi, haikufuata utaratibu. Alisema hayo kwa kutumia neno la Kiingereza, ‘dark market.’

Kauli hiyo ilionekana kumuudhi Makinda na wabunge wa CCM. Kundi kubwa la wabunge wa chama hicho lilisimama na kumtaka Spika kumfukuza Wenje ndani ya ukumbi wa Bunge.Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Raya Ibrahim Khamisi alikoleza moto huo baada naye kuomba mwongozo wa Spika akimweleza kiongozi huyo wa Bunge kuwa alitaka kuendesha uchaguzi bila ya kufuata Kanuni za Bunge.

Raya aliomba mwongozo huo baada Makinda kuwaeleza wabunge kuwa uchaguzi wa wenyeviti wa Bunge ungefanyika kwa kupigia kura majina matatu ya wabunge waliopitishwa na Kamati ya Uongozi.

Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, toleo la 2007 kanuni ya 11, uchaguzi huo utafanyika kwa kupigia kura majina sita na kati ya hayo, matatu yatakayopata kura za juu yatathibitishwa na Bunge kuwa wamechaguliwa.

Kanuni ya 11 (1) (a) inasema: Karatasi ya kupigia kura itakuwa na majina sita ya wabunge ambao wamependekezwa na Kamati ya Uongozi kupigiwa kura kutoka miongoni mwa wenyeviti na makamu wa wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge. Kununi ya 11(b) inasema: Kila mbunge atapiga kura kwa kuchagua majina matatu katika orodha hiyo; na
(c) Wagombea watatu watakaopata kura nyingi kuliko wengine ndiyo watakuwa wamechaguliwa kuwa wenyeviti wa Bunge.
Makinda alisema walipitisha majina hayo matatu baada ya Kamati ya Uongozi ambayo inashirikisha kiongozi wa upinzani na naibu wake kujiridhisha kuwa wengine kwenye kamati hiyo hawakuwa na sifa.

Raya aliomba mwongozo wa Spika na akasoma kanuni ya 11 ya Bunge kifungu (a) na (b), vinavyoonyesha kupingana na wazo la Spika la kutaka wabunge hao wachaguliwe bila kuvunja kanuni hiyo kwanza.Hoja ya Raya iliungwa mkono na kambi ya upinzani huku wabunge wa kambi hiyo wakianza kusimama mmoja baada ya mwingine kupinga wenyeviti hao kuchaguliwa kwa kura ya ndiyo na hapana, au ikubalike kuwa kanuni ya 11 ivunjwe kabla ya kufanya hivyo.

“Raya, naomba unielewe kazi ya kukaa hapa mbele siyo mchezo na inahitaji mtu ambaye ni ‘very strong’ (madhubuti), kwa hiyo sisi tumekubalina hivyo na itakuwa hivyo halafu kitu kingine ni kwamba ninyi huwa mnakimbilia mbele zaidi hata kabla Spika hajafika huko,” alisema Makinda na kuongeza:
“Tatizo jingine ninyi wa Chadema ni kwamba huwa mmejipanga kwamba huyu akazungumze hiki na huyu akazungumze kile kwa hiyo mnakurupuka sana wakati mwingine.”

Majibu hayo hayakuonekana kutuliza hali ya hewa katika ukumbi wa Bunge kwani wabunge waliendelea kutupiana maneno kama sokoni, hali iliyomlazimu Jaji Werema kusimama na kusema kwamba amevumilia kiasi cha kutosha na hivyo uvumilivu wake umefika mwisho.“Mheshimiwa Spika, nimevumilia kwa muda mrefu na vya kutosha sasa ni wakati wa kuchukua hatua tena kali, hivyo naomba Sajent of Arms itumike hapa,” alisema Jaji Werema.

Baada ya Jaji Werema kumaliza, Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Zitto Kabwe, alisimama na kutoa ufafanuzi wa maneno aliyotumia Wenje na kuomba mbunge huyo asiadhibiwe.Kauli ya Zitto iliamsha hisia za wabunge wengi, kwa pamoja walisimama Livingston Lusinde, Peter Selukamba, Ferister Bura na Halima Mdee ambaye alipewa nafasi ya kuzungumza na kusema kambi rasmi ya upinzani bungeni haitakubali kupiga kura za ndiyo na hapana kwa nafasi ya wenyeviti hadi kanuni ya 11 itakapovunjwa hata kama Wenje atafukuzwa.

Wabunge wa CCM walianza kuzungumza bila ya utaratibu baada ya kuomba nafasi kwa Spika na kunyimwa, huku wengi wakipiga kelele za Wenje kuondolewa bungeni na wengine wakisema: “Apelekwe kwa Babu akanywe kikombe.”
Majibizano hayo yaliendelea kwa zaidi ya dakika 10, huku Spika akionekana kupandwa na jazba na wakati huo alikuwa akilumbana na kila upande, wakiwamo wabunge wa CCM ambao walikuwa wakipiga kelele za kutaka Wenje afukuzwe ndani ya ukumbi.

Baadhi ya maneno yaliyosikika kutoka kwa wabunge wa CCM, ni: “Hawana adabu, wamezoea kukurupuka...” huku wengine wakisema kama wanamtetea Wenje basi watoke nje wote, lakini uchaguzi lazima ufanyike. Kwa upande wa upinzani kusika maneno ya “CCM hawana adabu, CCM mnafanya fujo...” huku Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbles Lema, akizungumza kwa sauti ya juu na kusema; “Fungeni milango tupigane.” Kwa upande wa upinzani, Zitto alisimama na kuanza kuwakemea wabunge akiwataka kunyamaza ingawa na yeye alitumia nafasi hiyo kuzungumza kwa jazba na kusema: “Hatoki mtu hapa.”

Baada ya kuona hali imekuwa tete, Spika alilazimika kukubaliana na hoja ya Raya na alimsimamisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi ambaye aliomba Bunge likubali kuvunja kanuni ya 11 ili kuruhusu wenyeviti hao kuchaguliwa licha ya kuwa akidi ya wagombea haitimii. Baadaye wabunge hao walikubaliana kuvunja kanuni hiyo na kupiga kura ya ndiyo au hapana kwa wabunge hao watatu.

Kufuatia hali hiyo, wabunge wa upinzani wakiongozwa na wabunge wa Chadema walipiga makofi kwa wingi wakiashiria ushindi kwani kile walichokuwa wakikihitaji ndicho kilichofanyika. Hata hivyo, Makinda kabla ya kutangaza kukubaliana na wazo hilo, alimwambia Wenje kuwa awe na adabu ndani ya vikao na kumwomba afute kauli yake huku akimbembeleza kuwa kufuta kauli siyo dhambi.Wenje alisimama na kusema kauli aliyoitumia ya dark market anaifuta na badala yake iingie kwenye kumbukumbu neno white market.

No comments:

Post a Comment