Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Wamachinga wa kigeni kuanza kukamatwa leo

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

WIZARA ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini leo wanaanza operesheni ya kuwakamata Wamachinga wa kigeni katika jiji la Dar es Salaam.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkakati wao wa kuhakikisha wafanyabiashara wa kigeni wanafanya kazi kwa mujibu wa vibali walivyopewa.
Alisema, wizara yake kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wataanza ukaguzi wa kina katika maeneo mbalimbali ya jiji hasa Kariakoo ambako ni kituo cha wafanyabiashara wengi.
Kwa mujibu wa waziri huyo, baada ya Kariakoo, operesheni hiyo itaendelea katika maeneo mengine ya nchi.
Alisema kutokana na makosa watakayokutwa nayo, Wamachinga hao wa kigeni watachukuliwa hatua kila mmoja kulingana na kosa lake.
Alisema wafanyabiashara wengi wa kigeni ambao wamekuwa wakiingia nchini kwa maelezo kuwa wamekuja kuwekeza, badala yake wamekuwa wakifanya biashara za Kimachinga.
Chami alisema serikali itazidi kufuatilia wafanyabiashara wote wanaofanya biashara kwa kukiuka taratibu walizopewa na kuhakikisha wanachukuliwa hatua kulingana na sheria za nchi ikiwa ni pamoja na kuwasimamisha kufanya shughuli zao katika maeneo yaliyoidhinishwa.
Katika hilo, Chami alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa pale wanapowaona raia wa kigeni wakifanya biashara ndogo ndogo ili waweze kuwafuatilia.
Mbali na wafanyabiashara hao wa kigeni, Waziri huyo wa Viwanda na Biashara alisema wizara yake itawafuatilia pia Watanzania ambao ni wafanyabiashara wanaokiuka sheria na vibali walivyopewa.
Wakati huo huo alisema serikali itaendelea kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara wote nchini hususan wajasiriamali wadogo ili kuwawezesha kumudu ushindani wa kibiashara.
Aliongeza kuwa wao kama serikali watahakikisha kunakuwa na Jukwaa la Wadau wa masuala ya uwekezaji na biashara ambalo litakuwa na jukumu la kujadiliana na kufanya tathmini ya masuala hayo kila baada ya kipindi cha robo mwaka.
Tags:

0 comments

Post a Comment