Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - UDSM hali ni tete. vita kati ya wanafunzi na polisi yazuka

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Je, huu ni wema wa ukatili?
WALITAKA KWENDA IKULU KUMUONA JK, VURUGU ZASABABISHA MWANAFUNZI KUJIFUNGUA MTOTO AKIWA AMEFARIKI

POLISI mkoani Dar es Salaam jana walilazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi, maji ya kuwasha na risasi kuwakabili wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) ambao walikuwa wakijibu mapigo kwa kuwarushia mawe polisi hao.

Wanafunzi hao walikuwa wakifanya maandamano kuelekea Ikulu, wakishinikiza nyongeza ya fedha ya posho wanayopewa na Serikali kutoka Sh5,000 hadi Sh10,000 kwa siku.

Mapambano hayo yaliyodumu kwa zaidi ya saa moja, maandalizi yake yalianza kusukwa kuanzia saa moja asubuhi jana kwenye Hosteli za Mabibo na ilipofika saa mbili asubuhi, wanafunzi walikuwa wamefika UDSM sehemu ya Mlimani.

Wakiwa katika safari ya kuelekea Ikulu, walipita Chuo Kikuu cha Ardhi kuwashawishi wanafunzi wajiunge nao ili kujenga nguvu zaidi wakisema wanataka wakamuone Rais Jakaya Kikwete, kwani ndiye mwenye uwezo wa kuamuru waongezewe posho yao ya kila siku ili ilingane na hali halisi ya maisha ya sasa.

Wakati harakati hizo zikiendelea, polisi walikuwa wamepata taarifa na wakawa wamejipanga eneo la Savei, tayari kuyasambaratisha maandamano hayo.

Katika maandamano hayo, wanafunzi walikuwa wamebeba mabango kadhaa yakiwa na ujumbe tofauti unaoshutumu Serikali kwa mambo mbalimbali, huku pia wakiimba nyimbo zinazosisitiza wapatiwe fedha zinazotolewa kwa kampuni ya Dowans ili wakabiliane na maisha magumu kutokana na fedha kidogo wanazopewa za kujikimu.

Nyimbo nyingine zilikuwa zikiwashutumu viongozi serikalini ambao wanajihusisha na ubadhilifu wa fedha huku wakiwa wamesomeshwa bure katika enzi za Serikali ya Awamu ya Kwanza.

Wakalinganisha mazingira hayo ya elimu ya bure kwa vigogo hao kwenye awamu hiyo ya kwanza na  mateso ya mazingira magumu wanayoyapata sasa huku wao wakiendelea kujilimbikizia mali na kuwabana kiasi kwamba wanashindwa kusoma.

"Kama siyo juhudi zako Nyerere mafisadi wangesoma wapi?" waliimba moja ya kibwagizo kwenye nyimbo zao, wakati wa maandamano.

Wakati wakiendelea na maandamano hayo, walikuwa wanazuia magari ya Serikali, yenye namba za STK kupita barabarani kwa kuwaamuru madereva kubadili njia.

"Hawa ndio mafisadi wenyewe. Kama hutaki kugeuza gari tutakushughulikia. Mnanunua magari ya kifisadi sisi tunakufa njaa, ipo siku tutagawana fedha yetu hiyo," mmoja wa wanafunzi hao alimueleza dereva wa gari la serikali huku akiungwa mkono na wenzake ambao walizomea na kutukana.

Mapambano na Polisi

Maandamano yalipofika eneo la Savei yalikutana na kundi la polisi likiwa limetanda pamoja na magari madogo nane na magari ya maji ya kuwasha yalikuwa mawili.

Askari hao walikuwa wakikagua mabasi yote ya daladala yaliyokuwa yanatoka Barabara ya Savei kuingia Sam Njoma kwa kuwashusha chini vijana wote waliowahisi ni wanafunzi wa UDSM.

Hatimaye msururu mkubwa wa maandamano ya wanafunzi hao ilikumbana na askari hao na wakawa wanaamriwa kurudi na kutawanyika, lakini yao waliwatia moyo wenzao, wakisema "twendeni, hawawezi kutufanya kitu."

Polisi walipoona wanafunzi wanawajia kwa kasi bila woga wala kujali amri yao wala vifaa kama vile bunduki, mabomu ya machozi na maji ya kuwasha,  waliamua kurudi nyuma kuwakimbia.

Kuona hivyo, wanafunzi hao walionekana kuwa na nguvu zaidi kwa kusonga mbele, huku wengine wakizomea ndipo askari mmoja aliporushia bomu la kutoa machozi.

Baadhi ya wanafunzi walisita kuendelea, lakini walipovurumishiwa mengine, walikimbia huku wawili wakianguka papo hapo na kukamatwa na kuwekwa kwenye gari la polisi.

Mabomu hayo yaliwafanya wanafunzi kukimbia kurudi walikotoka na wengine kutawanyika kuelekea kwenye baadhi ya nyumba na vichaka katika eneo hilo.

Kukimbia huko kuliwafanya wanafunzi hao kujipanga upya japokuwa si kwa wingi kama ilivyokuwa awali ambapo baadhi waliamua kufunga njia kwa kupanga mawe makubwa barabarani mbele ya Chuo cha Ardhi.

Katika eneo hilo, waliweka ngome yao wakisema liwe liwalo hawatakubali askari yoyote avuke, huku wakijikusanya katika kundi kubwa zaidi na kuimba nyimbo za kushutumu Serikali na wakati huo huo askari walikuwa wakisogea polepole kuwafuata.

Askari hao wakiongozwa na  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela wakiwa wanawasogelea, wanafunzi nao wakijiandaa kwa kubeba mawe ya kuwarushia kama njia ya kukabiliana nao.

Kuona hivyo, askari hao waliwavurumishia maji ya kuwasha na kupiga hewani risasi za moto ili kuwatawanya, lakini wao waliwajibu kwa kuwarushia mawe.

Baada ya kupambana kwa muda mrefu, gari moja la kumwaga maji ya kuwasha liliishiwa maji na wanafunzi hao wakatumia nafasi hayo kuongeza kasi ya kuwarumisha mawe polisi.

Baada ya muda mfupi, gari lingine la maji ya kuwasha liliwasili ili kuongeza nguvu, lakini wanafunzi walionekana kuwa na nguvu ya kukabiliana nao kiasi cha kuwafanya askari  kurudi nyuma.

Hali hiyo iliwafanya polisi kuamua kuongeza vikosi vingine vya askari ambapo walikuja na kasi kubwa zaidi ya kurusha mabomu mengi ya kutoa machozi ambapo baadhi yalielekezwa kwenye Chuo Cha Ardhi na kuwafanya wanafunzi waliokuwepo kuanza kukimbia hovyo.

Hali hiyo iliwatawanya kabisa wanafunzi hao na kusalimu amri ya kufanya maandamano kuelekea Ikulu ambayo ipo karibu kilomita zaidi ya 10 kutoka eneo la Mwenge.

Kauli ya RPC Kenyela

Kamanda Kenyela alisema walivunja maandamano hayo kwa sababu waandamanaji hawakufuata taratibu zinazotakiwa, za kuwa na kibali.

Alielezea kuwa hali hiyo wasingeweza kuiruhusu kwa sababu ingeweza kuhatarisha amani katika makazi ya watu na mali zao.

Alisema Jeshi la Polisi lilipata taarifa za kiintelijensia kwamba wataandamana hadi Ikulu.

"Tulipata taarifa za kiintelijensia kwamba wataandamana hadi Ikulu jambo ambalo ni kinyume na taratibu za nchi pia hata amani isingekuwepo katika makazi ya watu kwa hiyo tutaimarisha ulinzi wa kutosha kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayetoka maeneo ya chuo," alionya Kenyela.

Kenyela alisema kuwa wanafunzi hao wanatakiwa kuzungumza na uongozi wa chuo ili kupata namna ya kumaliza matatizo yao kuliko kufanya maandamano yasio na kibali.

Mwanafunzi ajifungua, mtoto afa
Wanafunzi watatu kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), wamejeruhiwa vibaya na kulazwa hosptalini huku mmoja wao akijifungua  mtoto mfu, kutokana na  vurugu hizo.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Yunus Mgaya aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa katika vurugu zilizotokea juzi, mwanafunzi mmoja aliyekuwa mjamzito, aliumia na hatimaye kujifungua mtoto ambaye hata hivyo alikuwa tayari amefariki.

Alisema  baada ya tukio hilo, mwanafunzi huyo alipelekwa katika Kituo cha Afya kilichoko katika hosptalini chuoni hapo, kupatiwa matibabu na kwamba hadi jana alikuwa bado amelazwa.

“Katika vurugu za leo (jana) zilizohusisha wanafunzi hao na polisi, wanafunzi wawili wameumia, mmoja baada ya kukatwa na kitu chenye ncha kali na amekimbizwa katika Hosptali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi. Mwanafunzi mwingine, alianguka na kuumia sehemu ya usoni na kushonwa katika kituo chetu,”alisema Mgaya.

Alisema katika vurugu za jana, baadhi ya wanafunzi walikamatwa na polisi na kupelekwa kituoni kwa kosa la kufanya maandamano yasiyo rasimi na kusababisha vurugu huku taarifa za kipolisi zikionyesha kuwa wanafunzi waliokamatwa ni zaidi ya arobaini.

Akisimulia tukio hilo, Mgaya alisema maandamano ambayo jana yaliwalazimu polisi kutumia nguvu kuyatawanya, yalianza juzi mchana chuoni hapo.

Alisema kuwa, siku ya kwanza ya maandamano kikundi kidogo cha wanafunzi kilikutana eneo liitwalo  ‘Revolution Square’ na kuanza kuhamashisha wanafunzi wengine kuandamama kwa lengo la kuishinikiza Serikali kuongeza fedha za kujikimu kutoka Sh5000 hadi Sh10,000.

Alisema kikundi hicho baada ya kushindwa kuafikiana na wanafunzi wengine kiliondoka na kwenda ‘Cafeteria’ namba moja na namba mbili na kufanya fujo kwa kupiga kelele na kuwapiga wenzao waliokuwa wakila chakula, kuvunja vyombo na kuchukua soda zilizokuwamo ndani na kunywa.

“Walipotoka hapo walikwenda kwenye madarasa ya ‘Arts’ (sanaa), huko walifanya vurugu kwa kuwafukuza wenzao waliokuwa wakisoma pamoja na walimu, wakiwatisha kwa kutumia fimbo,”alisema Mgaya.
Alisema baada ya hapo wanafunzi hao walielekea kampas ya uhandisi kwa lengo la kushawishi wanafunzi wa huko wawaunge mkono katika jitahada zao.

Kwa mujibu wa Mgaya, baada ya ushawishi wao kutofanikiwa, wanafunzi hao walifanya vurugu baina yao na wanafunzi wa huko na kusababisha uharibifu wa mali katika eneo la kantini iliyokopo eneo hilo.

Alisema mara baada ya vurugu hizo, wanafunzi hao walifunga safari kuelekea Ubungo Plaza kwa lengo la kumuona Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kumkabidhi madai yao.

Alisema kabla ya kufika Ubungo, wanafunzi hao walipata taarifa za waziri mkuu kutokuwapo Ubungo Plaza, ndipo walisimama na kuanza kushambulia magari yaliyotumika kubeba wanafunzi wa chuo hicho.

Akizungumza madai ya wanafunzi ambayo pia alikiri kuwa ni ya msingi.

Profesa Mgaya alisema tayari kuna taarifa za kuaminika kuwa upo mkakati wa kuangalia uwezekano wa kuongeza fedha hizo, ambao uko katika hatua za mwisho.

“Ni dhahiri kwamba tangu kiwango hicho kipandishwe mwaka 2007/2008, gharama halisi za maisha vyuoni zimepanda.

Hivyo basi kuna taarifa za kuaminika kwamba kupitia Bodi ya Mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya Juu, mchakato kubaini gharama halisi za maisha umeshakamilika na majadiliano yanaendelea kati ya bodi hiyo na wawakilishi wa Serikali za wanafunzi katika vyuo mbalimbali ili maamuzi stahiki yafanyike,”alisema Mgaya.

Mgaya alisema baada ya kufikiwa kwa makubaliano hayo, ongezeko hilo litaingizwa kwenye bajeti na kuanza kutolewa kwa wanafunzi wote vyuoni na kwamba hali hiyo itasaidia kupunguza matatizo ya wanafunzi.

“Kwa mantiki hiyo, hakuna sababu ya wanafunzi kusababisha vurugu na hali ya uvunjifu wa amani vyuoni, kwa  kisingizio cha kudai mabadiliko ya viwango vya fedha za kujikimu,”alisema Mgaya.

Wanafunzi wakamatwa
POLISI jijini Dar es Salaam imewakamata wanafunzi 42 wa UDSM na ARU kwa tuhuma za kufanya maandamano kuelekea Ikulu bila kibali.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Suleiman Kova aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa awali wanafunzi waliokamatwa walikuwa 60, lakini baadaye walichujwa na kubakia 42.

"Mchujo bado unaendelea ili kuwabaini waliohusika kuyaandaa maandamano hayo waliyosema kuwa yana lengo la kushinikiza kuongezwa fedha za kujikimu.

Kova alisema wanafunzi hao walikamatwa baada ya kutoka nje ya maeneo ya vyuo vyao na kujiandaa kuanza maandamano hayo ya kuelekea Ikulu.

Alisema walikamatwa kutokana na maandamano hayo kutokuwa halali kwa kuwa hayakuwa na baraka za polisi, chuo wala uongozi wa serikali ya wanafunzi.

“Kuna baadhi ya wanafunzi wamekula njama, ndiyo walioshinikiza maandamao hayo. Hii inatokana na baadhi yao kuonekana wakiwalazimisha wanafunzi wengine kuandamana bila hata ridhaa yao,’’ alisema Kova.

Lakini Kamanda Kova alieleza kuwa polisi imefanikiwa kuzuia maandamano hayo kabla hayajafika katikati ya jiji ambako yangeweza kuleta uvunjifu wa amani na kusababisha msongamano mkubwa wa magari.

Awali habari zilizolifikia gazeti hili zimeeleza kuwa maandamano hayo yalianza asubuhi baada ya wanafunzi wanaoishi Hosteli ya Mabibo kuandamana na kwenda kuungana na wenzao wanaoishi katika mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam kisha kuwafuata wengine wa chuo cha Ardhi.

Kwa mujibu wa habari hizo, polisi pia lilikamata mabango manane yaliyokuwa yamebebwa na waandamaji hao yenye maneno mbalimbali ya kushinikiza madai yao hayo.

"Pia tumekamata rundo la mawe makubwa na madogo ambayo yalikuwa na lengo la kuwapiga askari na makubwa yalilenga kuzuia magari barabarani," alisema Kamanda Kova.
Tags:

0 comments

Post a Comment