Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Mmiliki Dowans atinga Ikulu Dar• AANDIKA BARUA NZITO TANESCO, AZURU MITAMBO YAKE

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

Miliki wa Dowans, Suleiman Al Adawi akikagua
mitambo yake Ubungo Dar es Salaam jana
habari kamili soma pembeni.

MMILIKI aliye na hisa nyingi katika kampuni za Dowans Holdings SA na Dowans Tanzania Ltd, Sulaiman Al Adawi, amehitimisha ziara yake nchini jana baada ya kukutana na Makamu wa Rais, Mohammed Gharib Bilal, ofisini kwake jana.
Kabla ya kukutana na Bilal ambaye ndiye aliyekuwa akikaimu nafasi ya urais kutokana na Rais Jakaya Kikwete kuwa nje ya nchi kikazi, mfanyabiashara huyo (pichani) alikutana na uongozi wa juu wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO).
Habari za uhakika ambazo Tanzania Daima Jumatano imezinasa kutoka vyanzo vya kuaminika serikalini zinaeleza kuwa wakati wote akiwa katika mazungumza na Dk. Bilal na hata baada ya kumaliza mkutano wao, Adawi alikataa katakata kupigwa picha.
Chanzo cha kuaminika cha habari hizo kilieleza kwamba katika mazungumzo yao Dk. Bilal na Adawi walijadili masuala yaliyokuwa yakielezea kuhusu uwekezaji na matatizo yale yanayoikabili kampuni yake ya Dowans.
Habari zaidi zinaeleza kuwa siku mbili kabla ya kuzungumza na Dk. Bilal, bilionea huyo wa Dowans ambaye taarifa za kuwapo kwake nchini zimeibua maneno mengi, alikutana na Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, William Mhando.
Ilielezwa kwamba katika kikao chake na Mhando, aliwasilisha barua ambayo ilionyesha utayari wa kampuni yake kujadiliana na TANESCO na kupunguza kiwango cha fidia cha dola za Marekani milioni 64 (sawa na shilingi bilioni 94) ambacho shirika hilo la umma linapaswa kuilipa Dowans kutokana na hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro (ICC).
Habari za uhakika zinaeleza kwamba Dowans walikuwa tayari kusamehe zaidi ya dola za Marekani milioni 40 kwa TANESCO na wakati huo huo kukaa chini na shirika hilo kwa ajili ya kuingia mkataba mwingine na shirika hilo ambao wanadai utakuwa nafuu zaidi kuliko ilivyo kwa wazalishaji wengine wanaoliuzia umeme shirika hilo.
Hata hivyo, habari kutoka ndani ya TANESCO na ndani ya Dowans zinaeleza kwamba hadi kufikia jana mchana, mkataba huo ulikuwa haujatiwa saini na hivyo kusababisha mmiliki wa kampuni hiyo kuondoka nchini jana jioni na kuliacha suala hilo kwa wasaidizi wake.
Wakati hayo yakiendelea jana hiyo hiyo uongozi wa juu wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, na viongozi wengine wa juu wa wizara hiyo walikuwa na kikao kizito na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini wakijadili kuhusu suala zima linalohusu mgawo wa umeme na uwezekano wa kuendelea kutumia mitambo ya Dowans.
Kikao hicho ambacho kilikuwa kikifanyika katika Ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam kilipokea pia taarifa za hali ya uchumi nchini wakati huu taifa linapokabiliwa na mgawo mkali wa umeme.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa, Waziri Ngeleja aliwaeleza wabunge kwamba, makadirio yanaonyesha kuwa taifa limekuwa likipata hasara ya shilingi bilioni nne kila siku kutokana na mgawo huo unaotokana na upungufu wa maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme na kuongezeka kwa kasi kwa matumizi ya nishati hiyo muhimu.
Katika mazingira ya kushangaza, Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, William Mhando, alikanusha katakata taarifa za vyombo vya habari vya jana ambavyo vilieleza kuhusu kuwashwa kwa mitambo ya Dowans baada ya kufikiwa kwa maafikiano mahususi katika ya kampuni hiyo na shirika lake.
Wakati Mhando akiwaeleza wabunge hayo, taarifa za uhakika ambazo Tanzania Daima Jumatano ilizipata kutoka ndani ya TANESCO zilieleza kuwa, uongozi wa shirika hilo la umma uliagiza kuzimwa kwa mitambo ya Dowans usiku wa kuamkia jana, majira ya saa 7:00.
”Hawa jamaa (TANESCO) waliwaamuru Dowans wazime mitambo yao majira ya saa 7:00 usiku wa kuamkia leo (Jumanne). Taarifa zinaeleza hilo lilifanyika baada ya waandishi wa vyombo kadhaa vya habari kupata habari za uhakika za kuwashwa kwa mitambo hiyo,” kilieleza chanzo cha habari kutoka ndani ya shirika hilo.
Mbunge mmoja ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Nishati, alilieleza gazeti hili kwamba, walipigwa butwaa na kushangazwa na woga wa TANESCO kushindwa kusimamia maamuzi yake ya kuwasha mitambo ya Dowans.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika maeneo ya mitambo hiyo jana ambayo majira ya saa 7:00 mchana ilitembelewa na mmiliki wake, Adawi zilionyesha ukimya wa hali ya juu tofauti na ilivyokuwa kwa siku nzima ya juzi.
”Hawa jamaa wa TANESCO ni watu wa hovyo. Hivi wakiulizwa mbona hali ya mgawo wa umeme kwa siku mbili zilizopita (Jumapili na Jumatatu) kwa jiji la Dar es Salaam ilikuwa nafuu kuliko ilivyokuwa jana asubuhi watajibu nini?” kilihoji chanzo kimoja cha habari.
Habari zaidi kutoka ndani ya kikao cha kamati ya Bunge ya Nishati na Madini inayoongozwa na Mbunge wa Bumbuli, January Makamba, ziliieleza Tanzania Daima Jumatano kwamba, katika siku mbili ya kikao chao mjadala kuhusu ama kuwashwa au kutowashwa kwa mitambo ya Dowans kama suluhisho la mgawo wa umeme ndiyo uliotawala mazungumzo.
Wabunge kadhaa ambao ni wajumbe wa kamati hiyo, walilieleza gazeti hili kwa masharti ya majina yao kutotajwa gazetini kwamba katika kikao chao cha juzi walichokutana na viongozi wa Shirikisho la wenye Viwanda (CTI) na wawakilishi wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) jambo hilo liliibua mjadala mkali.
Mbunge mmoja alimkariri Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda wa Saruji cha Dar es Salaam akilalamika kwamba walikuwa wakipata hasara ya shilingi milioni 20 kwa siku kutokana na matatizo ya kukatikakatika kwa umeme.
Hoja za mkurugenzi huyo ziliungwa mkono na wawakilishi na viongozi wa CTI na TPSF ambao waliishauri serikalina TANESCO kutafuta njia za kisheria zitakazowezeshwa kutafutwa kwa mbinu za haraka za kulinusuru taifa kutokana na hatari za kuendelea kwa mgawo wa umeme.
Mbunge mwingine aliyezungumza na gazeti hili alisema, Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka ndiye mbunge pekee aliyesimama na kuonya kuhusu hatua zozote za kuwashwa kwa mitambo ya Dowans pasipo kwanza kupata baraka za Bunge.
Sendeka alikaririwa akisema kwamba, uamuzi wowote wa kuiwasha mitambo ya Dowans kwa sasa utakuwa ni kwenda kinyume cha maazimio ya Bunge ambayo pamoja na mambo mengine yalipendekeza kuvunjwa kwa mkataba kati ya TANESCO na kampuni hiyo.
Hoja hiyo ya Sendeka, ilipingwa na wawakilishi wa CTI ambao kwa maelezo yao walisema kulikuwa na njia mbalimbali katika hali ya dharura kama ilivyo sasa ambazo zinaipa uwezo TANESCO na serikali kuachana na mivutano ya kisiasa na kisheria na kulinusuru taifa kwa kuiwasha mitambo ya Dowans inayoweza kupunguza tatizo la umeme kwa kiwango cha kuzalisha megawati 112.
Tags:

0 comments

Post a Comment