Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Makinda: Nitawaondoa wabunge watakaopokea takrima, posho mbili

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda
akiwa na huzuni wakati Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Said Meck Sadick anamsomea taarifa kuhusu milipuko
ya mabomu katika kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
 Gongo La Mboto. Makinda ametembelea kambi ya waathirika,
Mzambarauni jijini humo
SPIKA wa Bunge, Anna Makinda, amesema atawaondoa kwenye Kamati za Kudumu za Bunge, wabunge watakaobainika kupokea posho mara mbili kutoka taasisi au mashirika ya umma.

Pia, Makinda alieleza msimamo wake kuwa, ni kutowavumilia na kuwachukulia hatua za nidhamu wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge, watakaopokea takrima kwenye ziara zao.

Alitoa onyo hilo jana wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani, alipokuwa akifungua semina ya mafunzo kwa wabunge wa kamati za Bunge zinazosimamia mapato na matumizi ya fedha za umma.

Semina hiyo inayozihusisha Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Hesabu za Serikali ( PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imeratibiwa na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Spika alisema itakuwa kosa kubwa kwa wabunge kupokea posho mara mbili au takrima wanapofanya ziara kukagua uendeshaji mashirika mbalimbali na idara za serikali na kwamba, hatua hiyo inazorotesha utendaji wa kamati.

"Kitendo cha kupokea posho mara mbili au takrima kinaathiri kwa kiwango kikubwa usimamizi na ukaguzi wa mashirika haya, maana wabunge wakipokea posho za Bunge na zile zinazotolewa na mashirika yanayokaguliwa hushindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo,” alisema Makinda na kuongeza:

“Katika hili wabunge watakaobainika nitawachukulia hatua za nidhamu ikiwamo kuwatoa kwenye kamati zao.’’

Alisema atatumia Kanuni za Bunge zinazozuia wabunge kupokea takrima yoyote wanapotembea mashirika wakati tayari ziara zao zinakuwa zimelipwa na Bunge.

Alisema licha ya wabunge kukumbwa na vishawishi vingi, ofisi yake itajitahidi kwa kadri itakavyowezekana kuboresha maslahi ya wabunge awamu kwa awamu ili kuwaondoa kwenye hali hiyo.

“Nafahamu kwamba posho zenu hazitoshelezi, lakini naomba kwa sasa mkubaliane na hali halisi kwa kuzingatia mazingira halisi ya wakati huu,’’ alisema.

Awali, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, alisema kamati ya PAC, LAAC na POAC zinakabiliwa na changamoto mbalimbali na kwamba, ili ofisi yake ifanye kazi kwa ukamilifu anategemea ufanisi wa kamati hizo.

“Baadhi ya changamoto za kamati hizi ni muda wa kutosha kufanya kazi za ukaguzi, wataalamu wa kutosha kuziwezesha kufanya utafiti wa kina kufuatilia utendaji wa serikali na taasisi zake, licha ya ukosefu wa fedha na vitendea kazi vya kutosha kuziwezesha kutimiza majukumu ipasavyo,’’ alisema Utouh.

Hata hivyo, Utouh alisema kamati za Bunge, Bunge lenyewe na ofisi ya CAG, vinahitaji uhuru wa fedha na utendaji ili viweze kufanya kazi kwa ufanisi.
Tags:

0 comments

Post a Comment