Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Mabomu yamfukua gerezani aliyefungwa maisha Ukonga

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
AMA kweli kufa, kufaana. Wakati maelfu ya wakazi wa Gongo la Mboto wakipagawa kwa taharuki ya milipuko ya mabomu, mfungwa aliyekuwa akitumikia kifungo cha maisha katika Gereza la Ukonga, alitumia fursa hiyo kutoka gerezani na kutokomea kusikojulikana.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili zimeeleza kuwa mfungwa huyo ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, alitoroka baada ya kukata bati la paa la gereza hilo, kutoka nje na kutokomea wakati walinzi wakiwa pia wanapigwa bumbuwazi kwa tukio hilo.  “Walikuta mashuka na mashati yamefungwa pamoja, inaelekea aliyatumia kama kamba ya kupandia juu kukata bati kisha kutoroka.

Sijui alitumia nini kukata bati!,”chanzo cha habari hizi kilieleza kwa sharti la jina lake kutoandikwa gazetini.  Lakini Kamishna wa Magereza nchini, Augustino Nanyaro, alipoulizwa kuhusu tukio hilo alijibu, “Sina taarifa, lakini hata ikiwa ni kweli ametoroka, ukitangaza kwenye gazeti kuna faida gani?,”  Pamoja na mwandishi wa habari hii kumuelimisha kamishna huyo faida ya kutangaza habari hizo kuwa ni pamoja na kuihusisha jamii katika kumtafuta, aliendelea kusisitiza “sidhani kama jamii itasaidia lolote, hata hivyo kuna taratibu zake.

Endapo nitaletewa taarifa hizo kutoka ngazi ya mkoa nitatangaza tu.”  Habari zaidi zinasema kuwa mfungwa huyo alitoroka baada ya askari wanaokuwa ndani ya vizimba vilivyo juu ya kuta zinazozunguka gereza hilo, kushindwa kuhimili milio ya mabomu na kukimbia.

Kwa mujibu wa habari hizo wakati hayo yakiendelea, wafungwa wengine walishirikiana kukunja nondo za kwenye milango ya vyumba wanamofungiwa, na walitoka nje na kukaa uwanjani.  “Jamani hakuna mwenye nia ya kutoroka, tuacheni tutoke humu ili kama ni kufa kwa mabomu tufie uwanjani,”chanzo cha habari kililieleza gazeti hili kikimkariri mmoja wa wafungwa hao akiwaeleza askari wa zamu.  Zoezi hilo la wafungwa kufungua milango kwa mtindo wa kukunja nondo na kutoka nje, liliendelea mpaka ikabaki milango mitatu tu ambayo haikufunguliwa kwa mtindo huo.  Kamishna Nanyaro alikiri wafungwa hao kutoka gerezani na kukaa nje uwanjani wakati wa milipuko hiyo, lakini akaeleza kuwa walifunguliwa milango na sio kukunja nondo.

“Kulikuwa na kamtafaruku kadogo, wakafunguliwa wakae uwanjani siyo kweli kwamba walivunja milango,” Nanyaro alieleza.  Alipotakiwa kueleza taarifa kwamba mtafaruku huyo umetokana na bomu kuingia gerezani, kamishna Nanyaro alijibu, "Hapana, yalikuwa mambo mengine tu. Kwanza mabomu hayakuanguka ndani ya gereza,  walichokuwa wakisikia wafungwa ni vishindo vya mabomu nje ya Gereza lakini si ndani ya kambi  ya magereza,” Nanyaro alisema.  Awali taarifa zilieleza kwamba bomu moja lilijikita ndani ya Gereza, kwenye ukuta wa eneo linalofahamika kwa jina la Guantanamo. 

Aidha mazingira ya ndani ya gereza hilo yalielezwa kuwa si salama hata kwa askari wanaolinda wafungwa gerezani, kwamba maeneo mengi ya ndani ya gereza yamegubikwa na giza kutokana na kutowekwa taa zilizokuwepo zilipoungua.  Baadhi ya makazi ya askari ndani ya kambi hiyo pia yameathiriwa na milipuko ya mabomu ambapo Mwananchi lilishuhudia gari moja dogo aina ya saloon likiwa limesambaratishwa, chumba kimoja cha kulala watoto cha nyumba moja ya askari pia kiliungua moto na baadhi ya mali kuteketea baada ya kipande cha bomu kudondokea chumbani humo.

Usiku wa kuamkia Alhamisi, wiki iliyopita mabomu yaliyokuwa kwenye ghala la kuhifadhia silaha ndani ya kikosi cha 511 cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania, (JWTZ), Gongo la Mboto na kusababisha madhara kwa mali na maisha ya watu. Mwisho.    
Tags:

0 comments

Post a Comment