Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Risasi zarindima mazishi ya waathirika wa mabomu

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
SHUGHULI ya kuaga miili ya ndugu wanne waliouawa kwa milipuko ya mabomu iliyotokea katika Kambi ya JWTZ, Gongo la Mboto jana iliingia dosari baada ya mtu mmoja ambaye hakutambulika kupiga risasi nne hewani.

Sakata hilo la aina yake lilitokea wakati wa kuaga miili ya ndugu hao waliouawa kwa kuangukiwa na ukuta wa nyumba iliyolipuliwa na mabomu katika eneo walilokuwa wakiishi, Gongo la Mboto Mzambarauni jijini Dar es Salaam.

Watu waliokuwa katika shughuli ya kuwaaga ndugu hao, Rose Nyajiego (36), watoto wake Clementina Nyajiego (3), Stellah Nyajiego, mwenye umri wa miezi mitatu na Neema Gati (14) ambao walisafirishwa jana jioni kwenda wilayani Rorya mkoani Mara kwa maziko, walikimbia hovyo wakidhani mlio wa bastola hiyo ni mlipuko wa bomu.

Ndugu hao waliouawa ni wa familia ya Jacob Nyajiego, Mfanyakazi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).

Walifariki baada ya kuangukiwa na ukuta baada kombora kulipua nyumba waliyokuwa wamesimama kwa nje wakiwa katika harakati za kukimbia milipuko ya mabomu.

Mwananchi lilishuhudia watu waliokuwa karibu na mtu huyo aliyepiga risasi hewani katika msiba huo ambao ulihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa wakitimua mbio hovyo.

Tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya viongozi wa serikali akiwemo, Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga, Mbunge wa Ukonga (CCM),  Eugene Mwaiposa pamoja na  Dk Slaa kuondoka eneo hilo.

Gazeti hili lilimshuhudia mtu huyo aliyekuwa amevaa suruali na shati nyeupe akichomoa bastola na kupiga risasi moja hewani na kuiweka katika mfuko wake wa suruali hali iliyowafanya watu waliokuwa  karibu yake kutimua mbio bila kujua wanakokimbilia.

Baada ya dakika mbili mtu huyo huku akiwa anaelekea sehemu alipoegesha gari lake alichomoa tena bastola hiyo na kupiga tena risasi nyingine tatu hewani huku akisema “Ndio naaga hivyo”,  hali ambayo ilizua tafrani kwa watu waliokuwa wamesimama karibu yake.

Baada ya kupiga risasi hizo mtu huyo alimpa bastola mwenzake aliyekuwa amevaa fulana ya bluu na suruali nyeusi ambaye aliiweka mfukoni na kisha wakapanda katika gari na kutokomea kusikojulikana.

Sakata hilo  hilo la aina yake liliacha gumzo kwa watu waliofika katika msiba huo ambao walikaa  vikundi na kuanza kuzungumzia tukio hilo huku wengine ambao walikuwa wamekimbia wakirejea eneo hilo kwa hofu kubwa.

“Tulidhani ni mabomu yamelipuka tena, huyu jamaa naona hana akili sawasawa, au amelewa nini, ”alihoji mmoja wa watu hao.

Wakati mtu huyo akipiga risasi hewani kuna baadhi ya vijana walikuwa wakimshabikia kwa kumfuata kwa nyuma wakimtaka azidi kupiga risasi hewani.

“Tena bwana, piga mzee tusikie, si mchezo, piga bwana, mwanangu bastola si mchezo, jamaa mkali kweli, anatisha, ”walisikika wakisema vijana hao ambao baada ya mtu huyo kuondoka walikwenda kukaa karibu na eneo ulipokuwa msiba huo huku wakicheka.

Hatahivyo,  shughuli ya kuaga miili hiyo ilimalizika salama na miili ilipakizwa katika magari tayari kwa safari ya kuelekea katika maziko.

Dk Slaa aibuka msibani

Shughuli ya kuaga miili hiyo pia ilihudhuliwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa ambaye alitoa rambirambi ya Sh 300,000 huku akiwataka waliopoteza ndugu zao kuwa na moyo wa uvumilivu.

“Ninatoa Sh300,000 kama rambirambi, ninachotaka kuwaeleza ni kwamba hawa wametangulia na sisi tutafuata kwa hiyo ndugu na jamaa wote tuwe wavumilivu hii ni mipango ya Mungu,”alisema Dk Slaa ambaye alikuwa ameandamana na mchumba wake, Josephine

Mbali na hilo, Dk Slaa pia alitoa dawa na mashuka yenye thamani ya Sh 1.6 milioni kwa waathirika wa milipuko hiyo ya mabomu.


Mtikila awavaa Dk Mwinyi, Mwamunyange

Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Christopher Mtikila, amemvaa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Davis Mwamunyange, akieleza kuwa anakusudia kuwafungulia kesi ya jinai.

Mtikila pia amesema kesi hiyo itamjumuisha Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),  Luteni Jenerali Abdurahmani Shimbo.

"Lakini pia ninatafuta wanasheria makini wa kupitia vifungu vya sheria kwa lengo la kuona uwezekano wa kumwondolea kinga Rais Kikwete (Jakaya) ili naye ajumuishwe kwenye kesi hiyo," alisema Mtikila alipokuwa akizungumza na gazeti hili jana.

Mtikila alisema anakusudia kuwafungulia kesi ya jinai watendaji hao wa serikali kwa uzembe uliosababisha vifo vya watu, uhalibifu wa mali na kulitia hasara taifa.

“Nipo tayari kwenda kuwafungulia kesi ya mauaji, kusababisha vifo, kuingizia hasara serikali na kutokuwa waaminifu na kazi zao, Dk Hussein Mwinyi, Abdurahmani Shimbo, Davis Mwamunyange, na Kikwete,” alisema Mtikila.

Hata hivyo Mtikila alifafanua kuwa kesi hiyo ni nzito na inahitaji fedha nyingi hivyo akawataka wanaharakati na wananchi walioguswa na tukio hilo, kumwongezea nguvu ya fedha ili atekeleze mpango wake huo.

"Ili kupata wanasheria ambao hawatachakachuliwa, zinahitajika Sh50 milioni. Nawaomba wananchi wenye uchungu na nchi hii, wawe na moyo wa kuchangia ili tufungue kesi hiyo,”alisema Mtikila.

Mtikila alieleza kuwa viongozi hao wa jeshi wanastahili kuwajibika kwa kuwa wanafahamu kila kitu kinachohusu jeshi ikiwemo elimu ya mabomu na silaha zingine lakini, wamefanya uzembe na kusababisha mauaji ya watu wasiokwa na hatia.

Kwa mujibu wa Mtikila, Dk Mwinyi anapaswa kuwajibika kwa kukubali kuiongoza wizara ambayo hana taaluma nayo.

"Hakupaswa kukubali kupokea wajibu asioweza kuutekeleza. Hazijui silaha na hawezi kuliongoza jeshi na hakustaili kuwekwa katika wizara hiyo.”

Aliendelea “Shimbo naye anatakiwa kuwajibika kwa kuwa aliwadanganya wananchi kuwa mabomu yaliyolipuka Mbagala mwaka (2009), hayatatokea tena, wakati sasa tunayaona yanatokea Gongola Mboto na Watanzania wanakufa, huku ni kutokuwa makini.”

Kuhusu Rais Kikwete Mtikila alisema, "Kikwete alipaswa kujiuzulu kipindi kile kile mabomu yalipolipuka. Alipaswa kulitangazia taifa anaachia ngazi na sio kujikosha kwa kuwadanganya wananchi kuwa anaunda tume ya kuchunguza milipuko."

Aliendelea "...lakini maadamu hakutaka kujiuzulu, nitatumia wanasheria kuangalia uwezekano wa kutumia vifungu vya sheria kumfutia kinga ya kutoshtakiwa ili naye ashtakiwe."

Kwa mujibu wa Mtikila serikali haiko makini kwa kuwa inacheza na maisha ya watu hivyo wananchi wanapaswa kufanya maandamano ya kuitaka iwajibike kwa milipuko ya mabomo ya Mbagala na Gongo la Mboto.

Aidha, Mkitila aliwataka wananchi wote nchini waandamane kumshinikiza Rais Kikwete ajiuzulu kutokana na uzembe wa serikali yake uliosababisha milipuko hiyo.

“Maandamano ndio njia pekee ya kumwondoa Kikwete madarakani. Nawaomba wananchi, kwa vile ameshindwa kujiuzulu mwenyewe, nguvu ya umma pekee ndio itamwondoa kama walivyofanya wenzetu nchini Misri na Tunisia,” alisema Mtikila.

Lakini tofauti na Mtikila, Chama Cha Kijamii (CCK), kimeibuka na kutaka Waziri wa Ulinzi, Dk Hussein Mwinyi, ajiuzulu na Rais Jakaya Kikwete kumfukuza kazi Jenerali Davis Mwamunyange kutokana na milipuko hiyo ya mabomu.

Katibu Mkuu wa CCK, Renatus Muabhi  aliimbia Mwananchi jana kuwa viongozi hao wanapaswa kuwajibishwa  kutokana na uzembe pamoja na kushindwa kujali maslahi na maisha ya Watanzania.

“Pia wawajibishwe kutokana na kuwa  katika uongozi wao matukio makubwa mawili ya milipuko ya mabomu yametokea na kusababisha vifo vya watu wengi huku wengine wakipata ulemavu,’’ alisema Muabhi. Hatua ya kung’ang’ania kuendelea kuwa madarakani  haileti hisia nzuri kwa JWTZ,’’ alisema.

Katibu huyo alisema kujiuzulu kwa Dk Mwinyi kutamaanisha kuwa amefikia uamuzi huo baada ya kuhisi tukio hilo si zuri na halikustahili kutokea.

Kuhusu Jenerali Mwamunyange, Muabhi alisema kufukuzwa  kwake kutasaidia kurejesha imani, hisia na msingi mzuri kwa JWTZ.

“CCK inashauri serikali kuanza kujenga maghala mapya na ya kisasa ya kuhifadhia silaha mbali na makazi ya watu,’’ alisema.

Kauli ya Mtikila na Muabhi zimetolewa siku kadhaa baada ya watu wa kada mbalimbali ikiwamo kambi ya upinzani bungeni, kutaka viongozi hao wajiuzulu.
Tayari Mashirika yapatayo 50 yanayotetea usawa wa kijinsia, haki za binadamu, na ukombozi wa wanawake kimapinduzi (FemAct) imetoa kauli kuwa inakusudia kuunda tume ya kuchunguza tatizo hilo na kutoa msimamo wake kuhusu watendaji waliohusika, kama itaonekana kuna uzembe.

"...Mallya amesema Femact inafanya uchambuzi yakinifu na tayari imeunda kikosi kazi kitakachofanya uchambuzi huo kutaka kujua ni kwanini masuala hayo yanaendelea na baada ya hapo Femact itatoa tamko kamili kuhusu tukio hili na ikibainika kuna uzembe itadai uwajibikaji kwa viongozi wanaohusika,"alisema Mkurugenzi wa TGNP, Usu Mallya.

Mallya ilisema hayo juzi wakati viongozi wake walipokuwa katika ziara ya kuwatembelea waathirika wa milipuko ya mabomu hayo eneo la Gongo la Mboto kwa lengo la kuwapa pole wahanga wa tukio hilo, kuwajulia hali wagonjwa, kutoa mkono wa pole kwa familia zilizopoteza ndugu na jamaa zao na kupata taarifa sahihi juu ya tukio hilo kutoka kwa wahanga wenyewe.

“Ukiangalia kwa karibu utagundua kuwa walioadhirika kwa kiasi kikubwa ni wanawake, wazee, watoto na walemavu, akina mama hasa wajawazito wameadhirika zaidi, ni lazima jamii nzima ilione hili na tuchukue hatua za dhati za kusadiana,”alisema Mkurugenzi wa TGNP, Usu Mallya.

Mkurugenzi wa The Leadership Forum Hebron Mwakagenda, amesema wanaharakati wanashindwa kuelewa ni kwanini majanga yanapoteokea serikali inakimbilia kuunda tume ambazo hata hivyo ripoti zake zinaishia kuwa siri.

Mwakagenda amehoji ilipo ripoti ya milipuko ya Mbagala na kusema kuwa tume zinapoteza muda na fedha za wananchi kwenye vikao badala ya kutafuta dawa ya tatizo.

“Kwenye majanga hatuundi tume tunaunda kikosi kazi, na kinatakiwa kutoa ripoti yake hadharani siyo kuiweka kabatini, vikao vipungue  viongozi wajitokeze kuwasaidia wananchi walioadhirika” amesema Mwakagenda.

Kampuni zajinadi kwenye maafa

Kampuni na taasisi zinazotoa misaada kwa waathirika wa milipuko ya mabomu ya Gongolamboto, jana waligeuza eneo hilo kuwa la kujitangaza kibiashara.

Kampuni na taasisi hizo zilikwenda katika eneo maalum kwa ajili ya upokeaji wa misaada la Gongolamboto Mzambarauni kwa malengo mawili, kutoa misaada, lakini pia kutambulisha biashara na shughuli wanazofanya.

Mwananchi, ilishuhudia maofisa wa Lions Club, wakipiga picha za makabidhiano ya misaada hiyo huku wakiwa na bango lenye maandishi makubwa ya maeneo wanayofanya kazi.

Maofisa hao walionekana wakihaha kuwatafuta waandishi wa habari ili wapigwe picha wakimkabidhi Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Meck Sadick misaada yao.

Katibu wa Lions Club, Mustafa Kudrat, alitoa vyakula na nguo vyenye thamani ya Sh 7 milioni.

Kwa upande wa kampuni ya kuuza nguo ya Mariedo, wao walifika wakiwa na gari lenye nembo ya kampuni hiyo na kukabidhi misaada ya nguo, chakula na maji huku picha zikipigwa kuonyesha uelekea wa nembo yao wakiwa na Kaimu Mkuu wa mkoa.

Wao pia walionekana wakiwa na waandishi wao wa habari ambao walifika katika eneo hilo maalum kwa ajili ya kazi hiyo tu.

Kwa upande wa kampuni ya udalali ya Yono kabla ya kutoa msaada huo, Mkurugenzi wake Scholastica Kevela, akaeleza historia ya kampuni  na shughuli inazofanya na kisha wasaidizi wake wakaanza kugawa kadi za mawasiliano (business card) kwa waliohudhuria shughuli hiyo.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo alimkabidhi  Kaimu Mkuu wa mkoa, vyakula na sabuni vyenye thamani ya Sh 700,000.

Taasisi ya Memon Jamaat, ilitoa  nguo za mitumba na vyakula vyenye thamani ya Sh 5 milioni.
Nao wanafunzi wanachama wa CCM wa vyuo vya elimu ya juu, walichangia fedha taslim Sh 420,000.

Akizungumza, Meck Sadick, alishukuru kwa misaada hiyo na kuahidi kuwa itatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwafikia walengwa.

Aliziomba taasisi na kampuni nyingine kuendelea kusaidia waathirika hao kwa kutoa misaada ya hali na mali.

Habari hii imeandaliwa na Fidelis Butahe, Felix Mwagara, Sadick Mtulya na Raymond Kaminyoge.
Tags:

0 comments

Post a Comment