Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Halmashauri Dar zampinga Magufuli

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

AGIZO la Waziri wa Ujenzi John Magufuli la kuweka alama za x mabango yote yaliyoko kandokando ya barabara na kutaka yaondolewe imepingwa vikali na halmashauri zote za jiji na kuamua kulifikisha suala hilo katika ofisi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Raphael Ndunguru, alisema wanajaribu kuangalia suala hilo kisheria ili kuona waliotekeleza hayo wana mamlaka yapi.
Alisema walikutana katika kikao cha pamoja na manispaa za Ilala na Temeke na kuzungumzia chanzo hicho cha mapato kwa halmashauri na yamewekwa kwa kuzingatia kanuni na taratibu.
Ndunguru alisema mwanzoni mwa wiki iliyopita waliamua kulifikisha suala hilo kwa Waziri Mkuu kwa kuwa halmashauri hizo ni sehemu ya serikali hivyo walistahili kukutana na wizara hiyo ili kujadiliana.
“Hatukutendewa sawa mabango yale hayawezi kuchangia kutokea kwa ajali wala si uchafu bali yanapendezesha mji …..lakini kitendo cha kuyaweka alama ya x ndicho kilichosababisha uchafu na tumekubaliana kutoyaondoa kabisa,” alisema.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusuf Mwenda, alisema wanatarajia kutoa tamko kwa kuwa si kitendo cha kiungwana kilichofanywa cha kuweka alama ya x, kwani mabango hayo ndicho chanzo kikuu cha mapato.
“Kama kulikuwa na tatizo basi sisi ni sehemu ya idara ya serikali tungekaa na kujadiliana na si kuweka uchafu kama walivyofanya,” alisema.
Pia Mkurugenzi Mtendaji wa ZEK Group International, Edwin Sannda, wa kampuni zinazojihusisha na uwekaji mabango ya matangazo nchini, amemshauri Waziri Magufuli kusitisha agizo lake la kutaka mabango yaliyoko kandokando ya barabara kuong’olewa badala yake akutane na wadau wote ili kujadiliana juu ya mfumo unaofaa kwa nia ya kuepuka usumbufu na athari ambazo zimeanza kujitokeza.
Mwishoni mwa mwaka jana, Dk. Magufuli alitoa maelekezo kuwa hataki kuona katika hifadhi ya barabara mabango ya matangazo kwa madai kuwa ni chanzo cha ajali.
Agizo hilo lilifuatiwa na uwekaji alama ya X kwenye mabango na mengine kuondolewa au kuharibiwa bila wahusika kupewa notisi au kushirikishwa.
Tags:

0 comments

Post a Comment