Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - BoT: Noti mpya zachakachuliwa

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter


BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imekiri kuwa noti mpya ilizozitoa kuanzia mwezi uliopita zimeanza ‘kuchakachuliwa’ na wahalifu kwa kutengeneza noti bandia.
Hayo yalisemwa jana na Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya dukuduku na maswali mbalimbali toka kwa wananchi kuhusiana na noti hizo mpya.
Akizungumzia suala la kuwapo kwa noti bandia za toleo jipya, Ndulu alisema ‘wajanja’ wameishaanza kujaribu kutengeneza noti mpya kabla ya wananchi kuzifahamu vyema.
“Mimi mwenyewe tayari nimeiona moja...wanaotengeneza noti bandia hata dola ya Marekani wanatengeneza. Wajanja lazima watajaribu tu hasa katika kipindi hiki lazima watatumia fursa hiyo kabla watu hawajazijua haraka noti za toleo jipya,” alisema.
Gavana huyo aliwaasa wananchi kuwa makini katika kuzielewa alama zilizoko kwenye noti hizo za shilingi 500, 1,000, 2,000, 5,000 na 10,000.
Akielezea jinsi ya kuzitambua noti halali, Ndulu alisema kuwa kuna mstari ambao umepita pembeni, ukiuchezesha kuna lensi inayocheza ambayo imeshonewa ndani ya karatasi.
Alisema teknolojia hiyo ya lensi hiyo kuonekana ikichezacheza haiwezi kuonekana au kuigwa na wahuni wanaotengeneza noti bandia.
Alifafanua kuwa ukiiweka kwenye mwanga utaona picha ya Mwalimu Nyerere na nyuma ya noti kuna alama ya twiga inayobadilika rangi, mambo ambayo hayawezi kufanyika katika katika noti bandia.
Alisema wao kama BoT wamejipanga kutoa elimu kwa kina zaidi na kwamba mkakati huo wataendelea nao wakati wowote ambapo elimu inahitajika.
Gavana huyo alisema hatua ya BoT kubadili fedha kila baada ya miaka mitano hadi saba ni moja ya njia ya kuweka alama bora zaidi za usalama ambazo ni ngumu kuzighushi.
Pia ubadilishwaji huo husababishwa na maendeleo ya teknolojia ya uchapaji wa noti katika kuongeza uhai wa noti katika mzunguko.
Katika hilo alisema hata Marekani au Uingereza zimekuwa zikibadili noti zake kwa sababu hizo.
Akijibu maswali na madukuduku kadhaa ambayo yamekuwa yakiulizwa tangu kutolewa kwa noti mpya, Ndulu alisema miongoni mwa maswali waliyopokea ni malalamiko kuwa noti mpya zikisuguliwa kwenye karatasi nyeupe zinaacha rangi na zikiloa hutoa rangi.
Akitolea ufafanuzi suala hilo alisema kuacha rangi noti zinaposuguliwa kwenye karatasi nyeupe ni jambo la kawaida kwani noti zote zilizochapishwa kwa teknolojia maalumu inayojulikana kwa kitaalamu kama ‘Intaglio Printing’ hufanya hivyo.
Alisema aina hiyo ya uchapishaji inazifanya noti kuwa na hali ya maparuzo zinapopapaswa.
Kwa mujibu wa maelezo yake, teknolojia hiyo imetumika ili kuimarisha kingo za noti kwa lengo la kupunguza uwezekano wa kuchanika au kuchakaa kwa haraka.
“Hata dola au euro ukizisugua kwenye karatasi zinatoa rangi na kitendo hicho kinathibitisha kuwa noti hiyo ni halali…noti ya bandia haiwezi kuacha rangi ukisugua,” alisema Ndulu.
Aliongeza, “Kuna watu wanasema ukiloweka inatoa rangi, sasa ni hivi rangi iliyotumika kutengenezea haichuji, kiwandani zinapotengenezwa zinapitia kwenye jaribio kama kuzipitisha kwenye mashine ya kufulia, kuziloweka na zikitolewa hazitoi rangi.
Pamoja na watu kudai kuwa noti mpya zinaonekana kutokuwa imara kwa sababu ya wepesi wake, gavana huyo alisisitiza kwamba noti hizo mpya ni bora zaidi kuliko zile za zamani kwa kuwa zimewekewa dawa inayojulikana kitaalamu kama ‘Anti Soiling Treatment’ inayozuia zisichafuke au kuchanika kwa haraka.
Pia alisisitiza kuwa noti za zamani bado ni halali na zitaendelea kuwa katika mzunguko pamoja na zile mpya mpaka zitakapotoweka kwenye mzunguko kwa sababu ya uchakavu wake.
Alisema huenda noti hizo za zamani zikatoweka katika mzunguko kati ya miezi 12 hadi mwaka mmoja na nusu hadi pale BoT itakapoutangazia umma.
Kuhusu upatikanaji wa noti mpya nchi nzima, Ndulu alisema kuwa ipo akiba ya kutosha ya noti hizo mpya na kwamba Benki Kuu inaendelea na mchakato wa kuziingiza kwenye mzunguko kwa kupitia benki za biashara.
Hata hivyo, alisema kutokana na mtandao wa baadhi ya matawi ya benki hizo kuwa ni mpana imechukua muda mrefu kwa baadhi ya maeneo kufikiwa na noti hizo.
Mbali na hilo Ndulu pia amewatoa hofu wale wote wanaofikiri kuwa umbile dogo la noti mpya kuwa ni upungufu wa thamani na kusisitiza kuwa zina thamani licha ya kuwa na umbile hilo.
Aidha, akijibu swali ambalo wananchi wamekuwa wakijiuliza kuwa kwa nini BoT haikutoa noti kubwa zaidi ya 10,000 ili kurahisisha malipo katika biashara, Ndulu alisema kuwa BoT hawakuona haja ya kutoa noti yenye thamani kubwa zaidi kwa sasa kwani malipo makubwa yanahimizwa kufanywa kupitia njia nyingine za kibenki.
Pia alisema uchumi wetu bado haujatuelekeza kutengeneza noti kubwa zaidi ya hapo.
Akigusia gharama iliyotumika kuchapishia toleo jipya la noti mpya, Ndulu alisema ni pungufu ya asilimia 30 ukilinganisha na ile iliyotumika kuchapishia zile za zamani.
Kuhusu tatizo la kukwama kwa pesa ama kushindwa kutoka katika baadhi ya mashine za ATM, Ndulu alisema kuwa mabenki yapo kwenye utaratibu wa kuziwezesha mashine zao ziweze kusoma noti hizo mpya.
Alisema kwa sasa wenye mabenki wanazifanyia marekebisho mashine zao za ATM kwa kuziwekea programu zitakazokuwa na uwezo wa kusoma fedha hizo mpya.
Akiichambua hali ya uchumi, gavana huyo alisema kwa sasa hali ya uchumi ni nzuri na kwamba nchi ina uwezo wa kulipa huduma kwa miezi sita bila kutegemea sehemu yoyote.
Ndulu alisema kwa fedha za kigeni tu kuna kiasi cha zaidi ya dola bilioni 3.8, kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa na nchi yoyote ndani ya Afrika Mashariki.
Akizungumzia grafu ya uchumi, alisema kwa mwaka 2010 katika robo ya kwanza uchumi ulikua kwa asilimia saba, wakati robo ya pili ulikuwa kwa asilimia 7.1 na robo ya tatu ulikuwa kwa asilimia 6.2.
Alisema, dhahabu pekee imeongoza kwa kuingiza bilioni 1.4 wakati sekta ya utalii ambayo ilikuwa juu ya dhahabu imeingiza kiasi cha bilioni 1.3.
Kwa upande wa mauzo ya nje ya bidhaa, alisema yameingiza milioni 900, mazao ya kilimo yaliingiza milioni 400 wakati huduma za bandari zilifanikiwa kuingiza milioni 380.
Katika hilo alisema uwezo wetu wa kuzalisha fedha za nje umekua sana ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Alipoulizwa kama tatizo la umeme limeathiri vipi uchumi katika kipindi cha robo ya mwaka huu, Ndulu alisema suala hilo litatolewa ufafanuzi na waziri husika hivyo asingependa kumuingilia.
Lakini alisisitiza, “Tutakua kiuchumi zaidi ya mwaka 2010.”
Hata hivyo, takwimu na maelezo hayo ya Gavana Ndulu yanayosifia hali nzuri ya uchumi, vinapingana na hali halisi ya kupanda kwa gharama za maisha, hususan bei za vyakula mbalimbali ambazo zimepanda
Tags:

0 comments

Post a Comment