Mwangwi wa kinachosasambuliwa sasa kwenye kile kituo cha habari cha Qatar, Al-Jazeera, inachokiita "Nyaraka za Palestina", una mshindo mzito kwa wahusika wakuu wa mazungumzo ya Mashariki ya Kati, Marekani ikiwa katikati.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Philip Crowley, amesema kwamba nyaraka hizi zinaifanya kazi ya nchi yake kuwa ngumu zaidi, ingawa ana matumaini kuwa Marekani itafanikiwa kuwapatanisha Waisraeli na Wapalestina.
"Hatukatai hali inakuwa ngumu zaidi ya vile ambavyo tayari ilishakuwa, lakini vikwazo kama hivi havitaweza kulibadilisha lengo letu la pamoja. Tunaamini makubaliano yanawezekana na ni ya lazima." Amesema Crowley.
Umoja wa Mataifa wawasifu viongozi wa Palestina
Naye mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika mazungumzo ya Mashariki ya Kati, Robert Serry, amesema kwamba baadhi ya maoni yanayotolewa kutokana na nyaraka hizi, yanapeleka ujumbe usiofaa, lakini amewasifu viongozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa alichokiita "kujitolea kwao kwa ajili ya haki kamili za watu wao."
Kundi la Hamas, ambalo ni hasimu mkubwa wa kundi la Fatah na Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, limesema kwamba, nyaraka hizi zinaonesha usaliti wa akina Abbas kwa Wapalestina wenzao kwa kushirikiana na adui yao, Israel.
"Wapatanishi hawa walikuwa hawapatani kwa maslahi ya haki za Palestina, bali kwa kile ambacho Israel ingeliweza kukikubali na Marekani kukiunga mkono. Na hicho sicho kitu ambacho Wapalestina wanakitarajia. Naamini hii ndiyo hoja muhimu na hii ndiyo sababu ya kuwasaliti watu wao." Amesema mwakilishi wa Hamas nchini Lebanon, Osama bin Hamdan.
Miongoni mwa mambo ambayo mkuu wa ujumbe wa upatanishi wa Palestina, Saeb Erakat, ametajwa kuyaridhia, ni kukubali kurejea nyumbani wakimbizi laki moja tu kati ya wakimbizi milioni tano wa Kipalestina, wanaoishi uhamishoni katika nchi kadhaa za Kiarabu hivi sasa.
Erakat yuko tayari kutoa zaidi
Pia Erakat na timu yake wanapendekeza kuundwa kwa kamati ya pamoja kati ya Palestina na Israel kusimamia moja ya sehemu tukufu sana kwa Waislam, Haram Al Sharif, katika mji wa Jerusalem, jambo ambalo lilikataliwa kabisa wakati wa uongozi wa muasisi wa harakati za ukombozi za Palestina, Marehemu Yasser Arafat, kwenye mazungumzo ya Camp David ya mwaka 2000.
Nyaraka hizi ambazo zinakuja hata joto la nyaraka za mtandao wa Wikileaks halijapoa, zinaonesha kuwa utawala wa Mamkala ya Ndani ya Palestina, uko tayari kuridhia na kutoa zaidi kwa Israel kuliko vile ambavyo iko tayari kujitolea kwa ajili ya amani ya Mashariki ya Kati.
Moja ya kauli zinazotajwa kuonesha hali hiyo, ni ile ya Erakat kusema kuwa Wapalestina wako tayari kuwapa Waisraeli 'Yerushalayim kubwa zaidi katika historia ya Kiyahudi.' Yerushalayim ni jina la mji wa Jerusalem, ambao ni mtukufu kwa Wayahudi, Waislam na Wakristo.
0 comments