Hata hivyo, Mbowe aliweka bayana kuwa mazungumzo hayo yasiwe ya kuweka mbele maslahi ya kisiasa na wala yasijikite kwenye kauli zinazotolewa na Makamba na katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, John Chiligati na badala yake yaweke maslahi ya taifa mbele. Lakini jana Makamba alisema chama chake hakina jambo lolote la kuzungumza na Chadema na kwamba sasa siasa zinahamia bungeni.
Makamba,ambaye huzungumza kwa mifano ya vichekesho na pia kutumia vitabu vitakatifu vya Biblia na Qorani, alianza kunukuu kifungu kitabu cha Methali 18:18 katika Biblia kinachosema: “Kura hukomesha mashindano; hukata maneno ya wakuu. “Sisi wote tulikwenda kwenye uchaguzi, kura zikapigwa, aliyeshinda anajulikana na walioshindwa wanajulikana, sasa sisi tukutane na Chadema tuzungumze nini? Wao watafute watu wengine wa kuzungumza nao si CCM.” Kwa mujibu wa Makamba, kwa sasa siasa zinahamia bungeni na kwamba endapo Chadema wanataka siasa za nje ya Bunge, wasubiri tena mwaka 2015 wakati wa uchaguzi mkuu.
“Tutakutana bungeni kwenye kujadili sera, kwa sasa sisi tunaunda serikali,” alisema Makamba ambaye katika Bunge la Tisa alikuwa mbunge wa kuteuliwa na rais. Naye mkurugenzi mtendaji wa taasisi isiyo ya kiserikali ya kukuza demokrasia nchini inayoitwa Agenda Participation 2000, Moses Kulaba alipongeza uamuzi wa Chadema, lakini akaonyesha wasiwasi kama serikali itakuwa tayari kukaa na chama hicho. “Ni jambo jema kwa Chadema kukubali maridhiano, lakini serikali itakuwa tayari kuzungumzia mambo haya,” alisema Kulaba.
Kulaba alisema mapambano yaliyoanzishwa na Chadema yanatakiwa yawe chachu ya kudai mabadiliko ya katiba pamoja na tume huru ya Uchaguzi baada ya hii iliyopo kulalamikiwa tangu uchaguzi unaoshirikisha vyama vingi uliporejeshwa mwaka 1995. “Kilio cha kudai hivi vitu kilianza tangu mwaka 2000, sasa inatakiwa Chadema iwe chachu ya mabadiliko hayo. Zanzibar wamefanya mabadiliko ya katiba; uchaguzi umeenda vizuri hakuna malalamiko kwanini ishindikane Tanzania Bara,” alihoji Kulaba.
“Tume ya Uchaguzi ni chombo muhimu sana, lakini pamoja na malalamiko ya miaka yote, kutoka mwaka 1995 mpaka leo, (Jaji Lewis) Makame amekuwa mwenyekiti wa tume hiyo,” alisema Kulaba. Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Bashiru Ally, alisema bado Chadema haijaweka bayana madai yao ili wananchi waweze kuwaelewa. Bashiru alisema baada ya waangalizi wa uchaguzi kutoa ripoti zao kamili, itakuwa ni wakati muafaka wa kujua kilichotokea katika uchaguzi huo.
![](http://www.blogger.com/img/icon18_edit_allbkg.gif)
0 comments