Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Shibuda atupwa rumande

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter John ShibudaIKIWA imesalia wiki moja kabla ya kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu, kada wa zamani wa CCM aliyehamia Chadema, John Shibuda anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani Maswa baada ya wafuasi wa chama chake kumshambulia dereva wa gari la CCM na kusababisha kifo chake.

Shibuda, ambaye aliwahi kutangaza kuwa angegombea urais kwa tiketi ya CCM kabla ya kujiengua na baadaye kuhamia upinzani, anagombea ubunge wa Jimbo la Maswa Magharibi kwa tiketi ya Chadema.

Habari ambazo zimepatikana kutoka wilayani Maswa na kuthibitishwa na kamanda wa polisi wa mkoa, zinasema kuwa Shibuda pamoja na watu wengine 12 wanashikiliwa baada ya dereva huyo wa gari la CCM aliyetajwa kwa jina la Steven Kwilasa Masanja, 26, kutoka Malampaka kufariki kutokana na kupigwa na mawe ambayo yalimpasua kichwa.

Vurugu hizo zimeripotiwa kutokea Oktoba 21 majira ya saa 10:00 alasiri kwenye Kijiji cha Kizungu katika eneo ambalo liko mita chache kutoka uwanja ambao Shibuda alikuwa akifanya mkutano wake wa kampeni za ubunge.
Kamanda wa polisi mkoani Shinyanga, Daudi Siasi aliiambia Mwananchi kwa njia ya simu toka wilayani Maswa kuwa wafuasi wa Chadema waliokuwa wakiutangaza mkutano wa Shibuda kwa kutumia gari la matangazo, walikutana na gari la wafuasi wa CCM wakati wakielekea kwenye mkutano wao na ndipo vurugu kubwa zilipozuka.
Alisema wafuasi hao walishambuliana na hatimaye kusababisha kifo.


Alisema jeshi lake linawashikilia watu 12, akiwemo Shibuda, kwa ajili ya upelelezi na kwamba yeye binafsi amekwenda wilayani humo kwa ajili ya kusimamia zoezi zima la uchunguzi.

“Kwa maelezo ya awali ni kuwa inaelezwa wafuasi hao wa CCM walipofika eneo hilo ambalo ni mita chache toka eneo ambalo Shibuda alikuwa akifanya mkutano, waliteremka kwa ajili ya kukojoa na gari la Chadema lilisimama na wafuasi hao wakaanza kushambuliana,” alieleza kamanda ingawa hakuweza kufafanua wafuasi hao wa CCM walikuwa wakitoka wapi na kwenda wapi.

Alisema katika vurugu hizo, Steven Kwilasa ambaye dereva wa mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Robert Kisena, alipoteza maisha baada ya kushambuliwa kwa mawe pamoja na kuchomwa na kitu chenye ncha kali, na kwamba wafuasi wa Chadema walikuwa wakitumia gari aina ya Toyota.

Kamanda Siasi alisema kuwa mbali na kuuawa kwa dereva huyo, wafuasi wengine wanne wa CCM waliokuwa kwenye gari hilo aina ya Toyota Hilux Surf, walijeruhiwa katika mapambano hayo na kuwataja kuwa ni Msaada Mangulu mwenye umri wa miaka 33, Sita Mashara, 32, Alexernder Edward, 43, pamoja na William Simon, 32, ambaye ni mdogo wa mgombea huyo wa CCM na kwamba hali zao zinaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu na kuruhusiwa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Maswa.

Kutokana na vurugu hizo, Shibuda ambaye alikuwa akiendelea na mkutano wake, alifuatwa na maofisa wa polisi na kuwekwa chini ya ulinzi na hadi jana alikuwa akiendelea kushikiliwa kwa mahojiano.
Akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu, Shibuda alisema bado anashikiliwa kudai kuwa kushikiliwa kwake kunatokana na maagizo ya CCM kwa vile wanataka kutumia njia hiyo kummaliza kisiasa licha ya kuwa wanatambua kuwa wakati tukio hilo alikuwa jukwaa akiendelea na kampeni.

“Hapa ninapoongea nawe niko polisi niliomba kuongeea na viongozi wangu wa chama, lakini nikueleze kilichotokea. Niliagiza gari litangaze mkutano wangu wa kampeni; wakiwa njiani walitaka kugongwa na gari la CCM, sasa katika kuyumba na kukwepa mmoja alidondosha kofia hivyo wakasimamisha gari na akaenda kuwaomba watu wa CCM wampe," alisema Shibuda.

"Lakini badala yake wakavamiwa na kuanza kuwapiga, na yeye kuona hivyo akapiga mayowe na wananchi wakaja kuwasaidia na kuwapiga hapo. Mpaka sasa sijui kama kuna mtu amekufa, nasikia hivyo.”
Alisema kushikiliwa kwake kunaonyesha ni jinsi gani ambavyo jeshi hilo linatumiwa na CCM kumkandamiza kwa kuwa eneo alilokuwa akihutubia yeye lilikuwa mbali na eneo la tukio, lakini amepata taarifa kutoka kwa baadhi ya maofisa wa polisi kuwa wamepewa maelekezo na vigogo wa juu wa CCM kuwa asiachiwe.

Mgombea wa CCM, Robert Simon Kisena alisema kuwa wafuasi wake walishambuliwa wakati wakiwa njiani kuelekea Kijiji cha Mwigulu, lakini walipofika eneo la tukio walisimama kujisaidia na ndipo walipofika wafuasi wa Chadema. Baada ya kuwapita kidogo, walisimamisha gari lao na kulifuata gari la CCM na kudai kofia zao.
“Sasa kukazuka mabishano na wakati hilo likiendelea watu wengine sita wakiwa na mapanga walitoka katika gari hilo na kuwavamia wangu na ndipo walipomshambulia dereva ambaye alishindwa kukimbia pamoja na wengine waliojiokoa,” alieleza mgombea huyo wa CCM.

Katika hatua nyingine, mgombea huyo wa CCM alifika kituo cha polisi na kusababisha sokomoko baada ya kumshambulia kwa mateke na kumuangusha chini mkuu wa kituo cha polisi wilaya ya Maswa (OCD), Peter Ndunguru akimtuhumu kuwa wamemwachia Shibuda.

Akizungumza kwa njia ya simu, OCD Ndunguru alisema mgombea huyo wa CCM aliambatana na viongozi wa chama hicho na kuuliza alipo Shibuda, na walipojibiwa kuwa yupo rumande mgombea huyo alimrukia OCD huyo na kuanza kumshambulia kwa mateke kiasi cha kumuangusha chini.
“Alinirukia na kunipiga,” alieleza OCD.

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga amethibitisha tukio hilo, akisema kuwa kulitokea kutokuelewana kati ya afisa wake na mgombea huyo, lakini akadai kuwa hilo ni jambo binafsi ambalo analiacha mikononi mwa OCD mwenyewe.

“Suala la Kisena na OCD ni jambo la kawaida kiutendaji na wala siwezi kulizungumzia... kwa sasa hapa ninashughulika na suala zito la mauaji," alisema kamanda huyo w aShinyanga.
"Suala hilo lilitokana na kutoelewana kati yao... kama OCD anaweza kumfungulia mashitaka ni yeye lakini sisi hatuna haja naye. Lakini nadhani tutawashauri wayamalize kwa kuwa ni ya kawaida kiutendaji.”
Tags:

0 comments

Post a Comment