IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
MFANYABIASHARA maarufu nchini na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mustapha Jaffar Sabodo, kwa mara nyingine amejitokeza hadharani kukichangia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kiasi cha sh mil. 100.
Sabodo amesema fedha hizo zitasaidia harakati za upinzani nchini kuwakomboa Watanzania na kuimarisha demokrasia, hasa katika wakati huu wa mfumo wa vyama vingi.
Hii ni mara ya pili kwa kada huyo wa CCM kutoa kiasi hicho, ambapo Julai 12, mwaka huu aliichangia CHADEMA ili iweze kushiriki kikamilifu katika kampeni na hatimaye Uchaguzi Mkuu.
Sabodo alikabidhi hundi ya sh mil. 100 jana nyumbani kwake Upanga, jijini Dar es Salaam kwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, aliyeambatana na viongozi wa kitaifa, akiwamo mbunge wa Viti Maalumu anayemaliza muda wake, Suzan Lyimo na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Anthony Komu.
Akikabidhi hundi hiyo, Sabodo alisema licha ya kuwa mwanachama wa siku nyingi wa CCM angependa kuona upinzani na demokrasia ya kweli inaimarika nchini huku akisisitiza kuwa CHADEMA ni chama makini ambacho kitawakomboa Watanzania.
Sabodo ni mmoja wa wazee wanaoheshimika katika jamii kutokana kutokuwa na misimamo ya kuyumbishwa, ambapo mara kadhaa amekuwa akiikosoa serikali pindi anapoona mambo hayaendi kama inavyotakiwa.
Mfanyabiashara huyo amekuwa akiikosoa serikali kwa kukiuka misingi ya utawala bora, iliyojengwa na mwasisi wa taifa hili, hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
“Mimi ni mwanachama wa CCM, lakini napenda kuona demokrasia inakua, huku kambi ya upinzani ikiimarika na kuwa na wabunge wengi bungeni ili kushamirisha maendeleo nchini.
“Leo ninawachangia CHADEMA kwa mara ya pili na ninatambua umakini wenu katika siasa za hapa nchini na hasa bungeni.
“Nitaendelea kuwa mwanachma halisi wa CCM na nitaendelea kukiunga mkono, lakini bila upinzani kama CHADEMA, CCM italala na haiwezi kuwa makini,” alisema Sabodo.
Sabodo alikuwa ni miongoni mwa marafiki wa hayati Mwalimu Nyerere enzi za uhai wake, ambapo mara kadhaa alikuwa akishiriki kwenye shughuli mbalimbali za kijamii pamoja na kutoa michango yake.
Katika kuonyesha kuwa CCM inahitaji kuwa na chama mbadala, mfanyabiashara huyo alisisitiza kuwa kuongezeka kwa wabunge wa upinzani bungeni ni jambo muhimu ili kutoa upinzani kwa ajili ya kusukuma maendeleo ya wananchi.
Alisema hali ilivyo sasa, ni lazima upinzani uimarike ili kuisukuma serikali kuwaletea maendeleo wananchi wanaoonekana kukata tamaa na serikali yao.
Akizungumza katika makabidhiano hayo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Mbowe, alimshukuru Sabodo na kusema msaada huo ni wa kihistoria katika mfumo wa siasa za vyama vingi nchini.
Alisema imekuwa vigumu kwa wafanyabiashara wakubwa wa kada ya Sabodo kuchangia kwa uwazi, tena kiasi kikubwa cha fedha na kutaka hatua hiyo kuigwa na wafanyabiashara wengine.
“Kwa kweli tunashukuru sana, hii ni historia mpya katika siasa za vyama vingi nchini, ni wajibu wa wafanyabiashara wakubwa kuona umuhimu wa kusaidia vyama vyote makini nchini bila ubaguzi wala woga, mzee umeonyesha njia, naamini itakuwa ni mfano kwa wengine wenye uwezo,” alisema Mbowe.
Alisema umefika wakati kwa wafanya biashara kuacha woga wa kuchangia vyama vya upinzani, kwani kufanya hivyo ni kudumaza demokrasia, hasa katika mfumo wa vyama vingi nchini.
Alisema fedha hizo zitalenga zaidi kutekeleza mipango endelevu ya kuimarisha chama, kwa kuwasaidia wagombea wa nafasi mbalimbali pamoja na kuwalipa mawakala nchi nzima katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Jumapili wiki ijayo.
Katika hatua nyingine, CHADEMA imechangia sh mil. 10 kwa klabu ya Lions ili kusaidia matibabu kwa watoto 10 wanaosafirishwa kwenda Afrika Kusini kwa matibabu ya moyo.
Akizungumza katika sherehe za kuwaaga watoto hao, Mbowe alisema mchango huo ni sehemu ya kuisaidia jamii, hasa watu wanaosumbuliwa na maradhi ya moyo.
Naye, Mwenyekiti wa Lions Club, Frank Goyayi, alisema chama hicho ni mfano wa kuigwa na vyama vingine vya siasa nchini katika kuisaidia jamii, hasa katika kuunga mkono juhudi za Lions Club.
You Are Here: Home - - Kada CCM afanya kufuru Aichangia CHADEMA MAmilioni• MBOWE: WAFANYABIASHARA WACHANGIE UPINZAN
0 comments