IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
WANANCHI wa Manispaa ya Arusha, bila kujali itikadi zao za kisiasa, jana waliandamana kwa amani wakiwa peku huku wamevaa magunia kupinga ongezeko la posho za wabunge na kutishia kuandamana hadi mjini Dodoma iwapo Rais Jakaya Kikwete ataidhinisha ongezeko hilo.
Wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali, wananchi hao walisema ni udhaifu wa Rais kukubali posho hizo zianzwe kulipwa kwa wabunge kabla hajasaini kama sheria inavyoelekeza na kumtaka kuchukua hatua kali dhidi ya wote waliohusika na ukiukwaji huo wa sheria za nchi alizoahidi kuzilinda katika kiapo chake.
“Iwapo kweli tayari wabunge wamejilipa posho hizo bila Rais kuidhinisha na hadi sasa hakuna mtu amewajibishwa, basi atakuwa ameonyesha udhaifu mkubwa kiuongozi, tutaandamana nchi nzima kupinga posho hizi bila kujali itikadi zetu kisiasa,” alisema Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya maandamano hayo, Mawazo Alphonce
Wakizungumza na waandishi wa habari mara baada ya maandamano hayo ya kilomita Saba, Mawazo ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Wazalendo Associate ya mjini Arusha, na Katibu wake, John Mchasu walisema kitendo cha Spika wa Bunge, Anne Makinda kutetea posho hizo ni kielelezo cha ubinafsi unaoonyeshwa na viongozi nchini.
“Spika kutetea posho hizo kuwa zitasaidia wabunge wake kuacha kuwa omba omba imetia doa nishani aliyotunikiwa na ni kielelezo cha ubinafsi na matumizi mabaya ya rasilimali za taifa kwa kundi moja dogo kujihalalishia mgawo mkubwa wa keki ya Taifa huku kundi kubwa likibaki bila matumaini,” alisema Mawazo.
Mawazo ambaye ni diwani wa Kata ya Sombetini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema Spika alipaswa kuwakumbuka na kuwazungumzia makundi mengine yanayotaabika kwa kipato kidogo na ugumu wa maisha kama walimu, wauguzi, madaktari na omba omba waliozagaa kila sehemu nchini, badala ya kutetea posho za wabunge wenye kipato kinachokadiriwa kufikia milioni 12 kwa mwezi.
Alisema ubunge sasa siyo wito wala uwakilishi wa umma bali ni fursa ya kujitajirisha ndiyo maana siku hizi watu wanauza rasilimali zao kufanikisha kushinda ubunge na ndiyo maana wakishaingia bungeni wanaanza kutetea ongezeko la posho kama inavyoshuhudiwa hivi sasa.
Alihoji uhalali wa wabunge kudai nyongeza ya posho wakati malipo yao kwa siku mbili ni zaidi ya mshahara wa mwezi mzima wa mwalimu na watumishi wengine wa kada ya chini serikalini.
Alitaja baadhi ya ishara za ubinafsi na matumizi mabaya ya madaraka kuwa ni kitendo cha viongozi wengi, watoto wao, ndugu, jamaa na marafiki kuishi maisha ya anasa na ufahari mara tu baada ya kuingia madarakani akitoa mfano wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alivyoongoza kwa uadilifu kiasi cha kushindwa hata kujenga nyumba hadi alipojengewa na serikali baada ya kustaafu.
Kuhusu kuvaa magunia na kutembea peku kwenye lami lenye joto kali mchana Saa 7:00, Mawazo alisema ni ujumbe unaowakumbusha jamii kusimama imara kupinga na kuzuia malipo ya kufuru na posho zisizo na maelezo ya kutosha na kuongeza kuwa katika siku zijazo hali hii ikiendelea maisha ya watanzania yatakuwa magumu na hawatamudu kununua hata nguo wala malapa kutokana na viongozi kujigawia keki yote ya taifa.
Moja ya mabango yaliyobebwa na watoto walioshiriki maandamano hayo lilisomeka “Wakati wabunge wanadai posho zaidi, watoto hatuna madawati, tunakaa chini kwenye mavumbi hivyo tunalaani nyongeza hizo,”
Diwani huyo ambaye kabla ya kuhamia CCM alikuwa katika Chama cha Tanzania Labour alikoshinda udiwani wa Sombetini alisema wako tayari kuandamana hadi Dodoma hata ikibidi kuuawa kwa kupigwa risasi kwani hata wakifa watafia ukombozi wa jamii iliyochoka kimaisha kutokana na viongozi wengi kujali maslahi binafsi badala ya umma wanaouongoza.
You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Arusha waandamana kupinga posho za wabunge
0 comments