Dk Slaa, ambaye atahitimisha kampeni zake mkoani Mbeya keshokutwa, aliwaambia maelfu ya wafuasi na mashabiki wa Chadema waliofurika kwenye viwanja vya Mwembeyanga kuwa atalazimika kupiga kura kwenye jimbo lake la Karatu kwa kuwa ndiko alikojiandikisha kwa shughuli hiyo.
Wakizungumza kwenye mikutano ya hadhara mjini Bagamoyo, Gongo la Mboto, Vingunguti na Mwembeyanga jijini Dar es Salaam, Dk Slaa na Marando Kikwete, CCM na wagombea wengine watapata shida Oktoba 31 kutokana na kutowaonea huruma Watanzania.
Akihutubia umati wa watu waliofurika kwenye mkutano wa kampeni kwenye mji mkongwe wa Bagamoyo, Dk Slaa alimshangaa Kikwete akidai kuwa hana huruma na umaskini wa watu wa nyumbani kwao, akidai kuwa alipiga makofi kushangilia wakati akisomewa taarifa ya matumizi ya zaidi ya Sh3.2 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa matundu manne ya vyoo vya shule za kata tano.
Dk Slaa alisema ni ajabu rais wa nchi kubariki umatumizi ya fedha hizo kwa ujenzi wa matundu ya choo akisema fedha hizo zinaweza kujenga zaidi ya zahanati 100 bila wananchi kutoa hata shilingi.
Shule hizo zilizojengewa matundu manne ya choo , ambayo kila matundu manne zilitumika Sh 700 milioni ni shule ya msingi Mbaruku, Kiromo, Kiharaka na Kongo ambazo kila moja.
"Nilishangaa sana kumuona Kikwete akishangilia na kupiga makofi alipokuwa akisomewa taarifa ya utekelezaji kwenye Jimbo la Bagamoyo. Huu ni ubadhirifu wa fedha za serikali kwa kujenga matundu manne ya choo katika shule za kata tano kwa kutumia Sh700 milioni kwa matundu manne," alisema Dk Slaa.
"Yaani kama kweli wewe una uchungu; unakubali na kusheherekea na kupongeza matundu manne ya choo kujengwa kwa fedha hizo, huo ni ufisadi na ndiyo maana aliweza kumyanyua Basil Mramba aliyekaa Segerea na kumtangaza kuwa ndiyo anafaa kweli. Huyo jamaa hawezi uongozi na hawezi kupiga vita ufisadi kwa sababu ufisadi uliopo wilaya ya nyumbani kwake anafumbia macho; unafikiri huo mwingine ataufanyia kazi," alihoji Dk Slaa.
Alisema Kikwete ambaye alikuwa mbunge kwa vipindi viwili na rais kwa miaka mitano, lakini sasa anaomba tena kura nyumbani kwao ambako alidai kuna umasikini wa kupindukia. Alisema licha ya kuwa mji wa kitalii, bado wananchi wa Bagamoyo wanaishi kwenye nyumba za mbavu za mbwa.
"Kila wakati huwa mnasikia kuwa Kikwete anakwenda nyumbani kwao Bagamoyo kupumzika. Anapumzika mahali ambapo wananchi wake ni masikini... mtu anayeshindwa kuendeleza kwao, unafikiri ana uwezo wa kuongoza sehemu nyingine? Nasema kuwa Kikwete hawezi kuongoza," alisema Dk Slaa.
Dk Slaa alisema kama Kikwete anafurahia uchafu wa ufisadi, basi bila shaka hata ule ufisadi wa mabilioni ya fedha yanayotokea ngazi ya taifa huwa anafahamu na anafumbia macho.
Katika mkutano wa Mazese, Dk Slaa alisema serikali yake itahakikisha inarudisha fedha zote zilizochukuliwa kifisadi na kuwekwa kwenye akaunti za nje ili zirudi kusomesha bure watoto na nyingine zitumike katika kuboresha maisha ya Watanzania waliokata tamaa.
"Nasema mimi sina utani na maisha ya Watanzania wote. Nikiingia Ikulu, lazima nitawakaba koo wale mafisadi wote waliojichotea fedha za umma na kuziweka kwenye akaunti za nje ili ziongeze kwenye idadi ya fedha za kusomesha bure watoto na nyingine ziingie kwenye huduma za jamii," alisema Dk Slaa.
Katibu huyo wa Chadema pia alirejea ahadi yake ya kupunguza bei ya simenti hadi Sh5,000 na vifaa vya ujenzi akisema hilo linawezekana kwa kuwa amepania kuwawezesha Watanzania waishi kwenye nyumba bora.
Akiwa Mwembechai ambako aliweka historia kwa kutangaza orodha ya watu aliowatuhumu kuwa ni mafisadi Novemba 15 mwaka 2007, Dk Slaa alitamba kuwa hadi sasa bado yuko huru licha ya Kikwete kusema angemfikisha mahakamani kwa kutaja orodha hiyo.
Dk Slaa, aliyemaliza mkutano wake wa kampeni saa 12:05, alisema Chadema imeifanya Novemba 15 ya kila mwaka kuwa siku ya kumbukumbu ya mafisadi, ikiwa ni njia mojawapo ya kukumbuka kuibuliwa kwa kashfa tofauti ambazo ni pamoja na wizi wa fedha za EPA, ununuzi wa rada, ndege ya rais na sakata la makampuni ya uchimbaji madini.
Mgombea huyo wa urais, ambaye alielezea kitendo cha magari ya abiria kupisha msafara wake wakati akielekea kwenye mkutano huo kuwa kinaonyesha anakubalika kwa kila hali, aliwaahidi wananchi hao kuwa atakigeuza Chuo cha Sanaa cha Bagamoyo kuwa Chuo Kikuu cha Michezo na kukipandisha hadhi chuo cha Malya.
Alisema kuwa inashangaza kuona kuwa masuala la mpira yanahusu klabu mbili tu za Simba na Yanga na kwamba chuo hicho cha michezo kitafundisha walimu ili makocha wa michezo wazalishwe ndani ya nchi na kuibua vipaji vingi.
Mbunge huyo wa zamani wa Karatu aliwakumbusha wananchi kutokubali kuingia kwenye mtego wa kupandishwa hasira wakati wa uchaguzi akiwashauri kuwa watakapochokozwa, wawapuuze wachokozi kwa kuwa hiyo ni njia kuu ya kumpuuza mtu.
Lakini alisema CCM ndio inayoweza kusababisha vurugu kwenye uchaguzi wa mwaka huu kwa sababu ni chama cha kigaidi ambacho kimeunda kambi ya kuwafundisha vijana wao mbinu za kupigana.
Dk Slaa aliwataka wananchi kulinda kura zao kwa utulivu bila kufanya vurugu za aina yoyote na kwamba kila mwananchi ana wajibu wa kulinda kura yake isipotee na isichachuliwe na CCM.
Akizungumza katika jimbo la Segerea Dk Slaa alimsafisha mgombea ubunge wa jimbo hilo, Fred Mpendazoe kuwa alikuwa mbunge namba moja wa CCM kukemea na kupiga vita ufisadi na kudai kuwa mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango ni mnafiki.
Naye Marando, ambaye alirusha tuhuma nzito dhidi ya viongozi wakuu wa CCM na makada wake wakati Chadema ilipozindua kampeni zake jijini Dar es salaam zaudu ya miezi miwili iliyopita, jana alisdema kuwa Kikwete atahukumiwa na Mungu kutokana na kitendo cha kuwaachia huru watuhumiwa wa ufisadi kwenye kashfa ya wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA).
Alikuwa akizungumzia kashfa ya wizi wa fedha hizo uliofanyika kati ya mwaka 2005/06 kwenye Benki Kuu ya Tanzania. Hadi sasa zaidi ya watu 20 wameshashtakiwa kwa kuhusika kwenye wizi huo, lakini rais alitoa ahueni ya kutowapandisha kizimbani watu ambao waliitikia wito wa kuzirejesha fedha hizo kabla ya Novemba mosi.
Marando alisema kuwa kitendo hicho ni sawa na kuunga mkono ufisadi na kuwageuka wananchi na kwamba CCM imewatetea wanachama wake kwa ajili ya kuficha madhambi yao, jambo ambalo linawafanya wananchi wa hali ya chini kuishi katika mazingira magumu ya maisha.
"CCM inawatetea wanachama wake kwa madai kuwa hawajafanya kosa kwenye kashfa ya EPA; Mungu atamuhukumu Kikwete kutokana na vitendo hivyo kwa sababu yeye ndio mwenye jukumu la kuwahukumu wananchi hao,"alisema Marando.
Alisema ili kutatua tatizo wananchi wanapaswa kufanya maamuzi ya mwisho kwa kumpigia kura Dk Slaa, ambaye anawania kuongoza serikali ya awamu ya tano.
Alisema mkakati uliopo ni kuhakikisha kuwa wabunge wanafanya kazi ya ubunge na mawaziri wanafanya kazi ya uwaziri ili mambo yaweze kwenda sawa.
Alifafanua kuwa ahadi zote za barabara, maji na umeme alizotoa Kikwete zitatekelezeka kutokana na kodi za wananchi wenyewena kuwataka kusimamia utekelekeza wa ahadi hizo.
Naye katibu Mwenezi wa Chadema, Jimbo la Ukonga, Ernest Njooka jana ametoa mpya baada ya kumpigia debe mgombea udiwani Kata ya Gongolamboto kwa tiketi ya CUF, Bakari Shingo ili wananchi waweze kumchagua.
Mgombea huyo alitoa kauli hiyo jana kwenye viwanja vya Kampala, maeneo ya Gongo la Mboto, Dar es Salaam muda mfupi kabla ya Dk Slaa kuhutubia mkutano wa kampeni kwenye viwanja hivyo.
“Katika kata hii ya Gongolamboto tumeamua kumnadi mgombea wa CUF kupitia mkutano huu kwa kuwa anakubalika na wananchi, ndio maana hatukuwa na sababu ya kumsimamisha mgombea wa Chadema... kura zote kwa kata hii kupitia udiwani mpigieni Shingo,” alisema Njooka.
Imeandaliwa na Patricia Kimelemeta, Hussein Issa, Pamela Chilongola na Musa Mkama.
0 comments