IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
JESHI la Polisi mkoani Shinyanga linamshikilia mgombea ubunge katika Jimbo la Maswa Magharibi kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Simon Kisena, kwa kosa la kumpiga ngwala Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Maswa (OCD), Peter Ndunguru.
Habari zinasema Kisena alimpiga ngwala ODC Nduguru baada ya kushindwa kuelewana katika mahojiano baada ya mgombea huyo kupata taarifa za dereva wake kushambuliwa na watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Daudi Siasi, alisema Kisena alifanya kitendo hicho Oktoba 21, mwaka huu kufuatia vurugu zilizowahusisha wafuasi wa CHADEMA na CCM na kusababisha kifo cha mtu mmoja aliyetajwa kwa jina la Steven Kwirasa (26).
Alisema Kisena alikamatwa jana mchana na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na kupelekwa moja kwa moja mahabusu.
Kukamatwa kwa mgombea huyo kunaongeza idadi ya watu wanaoshikiliwa kufikia 14, akiwamo mgombea ubunge wa CHADEMA, John Shibuda na wengine 12 kwa kile kilichodaiwa kuhusika kwenye tukio hilo.
Inadaiwa wakati Shibuda akiwa kwenye mkutano wa kampeni katika Kijiji cha Kizungu, gari lake liliondoka kwa ajili ya kuelekea kijiji kingine kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mkutano mwingine.
Alisema katika tukio hilo, dereva wa mgombea ubunge wa CCM, Steven Kwilasa (26) aliyekuwa anaendesha gari lenye namba za usajili T 917 BBH alishambuliwa kwa mawe na kipigo hadi kifo.
Alisema kutokana na hali hiyo, wafuasi wanne wa CCM walijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili, ambapo mgombea wa CCM hakuwa eneo la tukio hilo.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, alisema jeshi hilo limeunda tume ya maofisa wanne kwa ajili ya kuchunguza chanzo cha vurugu hizo.
Alisema mara baada ya uchunguzi huo, uamuzi wa kumpa dhamana Shibuda ndipo utatolewa, lakini kwa sasa hana namna zaidi ya kuendelea kushikiliwa.
“Ni kweli niko Maswa kwa ajili ya kuendelea na uchunguzi wa tukio hili… tumeunda tume ya maofisa wanne kwa ajili ya kuchunguza suala hili, tutatoa majibu pindi kazi hii ikikamilika,” alisema DCI Manumba.
You Are Here: Home - - Mgombea Ubunge ampiga Ngwala Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Maswa (OCD), Peter Ndunguru. Akamatwa
0 comments